• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Denmark yasitisha kwa muda chanjo ya AstraZeneca

Denmark yasitisha kwa muda chanjo ya AstraZeneca

Na MASHIRIKA

COPENHAGEN, Denmark

TAIFA la Denmark limesimamisha kwa muda shughuli ya utoaji chanjo ya AstraZeneca baada ya ripoti kuibuka kuhusu visa vya kuganda kwa damu ya baadhi ya waliopewa chanjo hiyo.

Miongoni mwa walioathirika ni raia mmoja wa nchini hiyo, kulingana na taarifa iliyotolewa na maafisa wa nchi hiyo Alhamisi.

Hata hivyo, maafisa wa serikali ya Denmark hawakutoa idadi ya watu ambao waliathirika kwa kuganda damu baada ya nchini humo.

Lakini ripoti kutoka Austria ilisema kuwa taifa hilo limekoma kutumia chanjo hiyo huku maafisa wake wakichunguza kisa ambapo mtu mmoja anadaiwa kufariki kutokana na matatizo ya kuganda kwa damu. Mtu huyo pia alidaiwa kufariki kutokana na tatizo la mishipa ya damu.

Duru zilisema Alhamisi kwamba mataifa mengine sita ya Uropa yalisitisha shughuli ya utoaji wa chanjo hiyo ambayo imetengenezwa na taasisi ya Serum Institute ya India.

“Sisi na Shirika la Dawa Nchini Denmark tumebaini madhara ya chanjo hiyo,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya Denmark, Soren Brostrom katika taarifa.

Mamlaka hiyo ilieleza kuwa chanjo hiyo itasimamishwa kwa siku 14. Hata hivyo, haikutoa maelezo zaidi kuhusu mgonjwa ambaye aliathirika baada ya damu yake kuganda.

Hata hivyo, kampuni ya AstraZeneca ilijitetea dhidi ya madai hayo ikisema kuwa chanjo yake imefanyiwa ukaguzi na kuthibitishwa kuwa salama na “hakuna kisa ambacho kimethibitishwa cha madhara ya chanjo yetu.”

Kampuni hiyo ilisema kuwa imekuwa ikiwasiliana na Australia na inaunga mkono uchunguzi wao.

Mnamo Jumatano Shirika la Dawa Barani Uropa (EMA) lilisema hakuna ushahidi wa kuhusisha chanjo ya AstraZeneca na visa viwili ya watu kuganda damu nchini Austria.

Ripoti hii huenda ikasababisha hofu na taharuki nchini kwa sababu imeibuka wiki moja baada ya serikali kuanza mpango wa utoaji chanjo hiyo ya AstraZeneca.

Hii ni baada ya Kenya kupokea shehena ya kwanza ya dozi 1.02 milioni ya chanjo hiyo mnamo Machi 4, 2021. Wale ambao wanapewa chanjo hii kwanza ni wahudumu wa afya, maafisa wa usalama na walimu. Zoezi la kuwapata walimu chanjo hiyo ilianza Alhamisi.

Jumatano, Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi aliambia wabunge kuwa kufikia Jumanne jumla ya Wakenya 4,000 walikuwa wamepokea chanjo hiyo.

Tafsiri na Habari Zaidi: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Kagame ndiye kiongozi wa kwanza Afrika Mashariki kupata...

Vyama vya kisiasa vitakavyohusika na fujo vitafutiliwa...