• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Kifo cha Magufuli chamletea Harmonize dhiki kuu

Kifo cha Magufuli chamletea Harmonize dhiki kuu

NA WANGU KANURI

Mapenzi ya mtu kwa mwingine huthibitishwa kwa matendo. Hata hivyo, mapenzi haya kwa nchi huonyesha uzalendo wa mtu huku mapenzi kwa kiongozi ukilenga kufurahishwa na matendo ya kiongozi huyu kwa wananchi. Isitoshe, nyimbo hutungwa na wasanii kama njia ya kuyaonyesha mapenzi haya ya dhati kwa kiongozi fulani.

Huu ndio mkondo ambao msanii Harmonize wa nchi ya Tanzania alichukua alipopewa fursa ya kuwatumbuiza katika kikao cha umma, eneo la Likangala mnamo Oktoba 15 2019.

Kwa kuuchukua mdundo wa wimbo Kwang’waru ambao aliuimba akimshirikisha msanii tajika Diamond Platinumz, Harmonize alizirindima sifa tele kwa rais Magufuli.

Katika wimbo huo, Harmonize aliorodhesha kazi alizofanya rais Magufuli haswa katika ukuzi wa uchumi wa nchi hiyo. Wimbo huu ambao uliwavutia watu waliomiminika katika kikao hicho na wakajitosa kwenye ukumbi na kucheza dansi naye, ulimfanya rais Magufuli kuinuka na kupiga makofi huku uso wake ukionyesha tabasamu la moyo.

Kwenye maneno ya wimbo huo, Harmonize alitaja jinsi Magufuli alijenga barabara za juu ‘flyover’, daraja Kigamboni, pahala pa kutua kwa mandege, kuimarika kwa reli ya SGR kiasi cha kwamba mtu angeweza sinzia akisafiri.

Vile vile alionyesha jinsi rais Magufuli ni mwepesi wa kusamehe kielelezo kikiwa Papi Kocha ambaye aliachiliwa huru. Aliimba jinsi Magufuli, alizifufua nyanja zilizowacha kufanya kazi, akarudisha nidhamu serikalini kiasi cha kwamba ungeleta unjanja ungeondolewa.

Alionyesha kuwa kero ambazo ziligubika sekta ya madini, umeme na maji zimepungua huku elimu ikifanywa kuwa ya bure hivi kwamba kuwapa fursa watoto wa shule kubukua vitabu bila shida.

Isitoshe, vituo vya afya kwenye kila kata viliimarishwa, uchumi ukapandishwa juu, viwanda vikaboreshwa huku mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam ukikua kwa kasi. Aisee, kwa msanii huyu Magufuli uongozi aliufahamu kama tu alivyoimba.

Katika kipokeo cha wimbo huu msanii huyu alimpa moyo Magufuli kwa kumwambia kuwa wasiompenda wabane choo na wamwache Magu (ufupisho wa jina lake rais Magufuli).

Aliongeza kuwa rais Magufuli ni kigogo kutoka Chato na rais wa wanyonge. Akimalizia alimrai asimame imara ili Tanzania isonge mbele. Alimrai makamu wake mheshimiwa mama Samia Suluhu na Kaasim Majaliwa kusimama imara pia.

Kupitia kuwaburudisha watu waliojumuika marehemu Rais John Pombe Magufuli aliidhinisha uwaniaji wa Harmonize kwenye kiti cha ubunge katika eneo bunge la Tandaimba.

“Ningependa kumpongeza Harmonize, anatoka eneo gani? Tandaimba? Nani mbunge wa eneo hilo hivi sasa? Ningependa kuidhinisha uwaniaji wake Harmonize katika kiti cha ubunge cha Tandaimba,” rais Magufuli akasema.

Kifo cha rais huyu kimekuja kama pigo kwake msanii huyu ambaye kupitia video kwenye Instagram yake, Harmonize alionekana mwenye kusombwa na majonzi huku machozi yakimtoka bila kikomo.

Msanii huyu ambaye alitambulika na rais baada ya tumbuizo lake kwake, alionekana mwenye uchungu mwingi baada ya kufahamu kifo cha rais John Pombe Magufuli.

Rais John Pombe Magufuli alifariki Jumatano usiku katika hospitali ya Muzena iliyoko mji wa Dar es Salaam. Kama alivyoeleza umma makamu wa rais Bi Suluhu, mwendazake rais Magufuli aliaga kwa sababu matatatizo ya moyo.

You can share this post!

Utawala wa Magufuli ulivyoua demokrasia Tanzania

Mtangazaji wa zamani wa NTV afariki kutokana na corona