• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Kundi la kigaidi laua raia 138 Burkina Faso

Kundi la kigaidi laua raia 138 Burkina Faso

Na AFP

OUAGADOUGOU, Burkina Faso

WATU 138 wameuawa kaskazini mwa Burkina Faso na watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi moja la kigaidi.

Hili ndilo shambulio baya zaidi la kigaidi katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika tangu mwaka wa 2015, kulingana na maafisa wa serikali.

Mnamo Jumapili, Rais Roch Marc Christian Kabore alilaani shambulio hilo lililotekelewa karibu na eneo la mipaka ya nchi hiyo na nchi jirani za Mali na Niger. Ni katika eneo hilo ambako wapiganaji wa makundi ya al-Qaeda na Islamic State (IS) wamekuwa wakiwashambulia raia na wanajeshi.

“Watu wengi wamefariki kutokana na majeraha waliopata. Miili mingine zaidi imepatikana. Hata hivyo, idadi ya waliofariki ingali inasalia 138,” afisa mmoja wa serikali katika eneo hilo alisema Jumamosi.

Shambulio hilo lilitekelezwa Jumamosi jioni.

“Maiti hizo zilizikwa katika makaburi ya halaiki,” afisa huyo akasema, akiongeza “wengine wengi wamejeruhiwa” kufuatia shambulio hilo lililotekelezwa majira ya usiku.

“Sharti tuungane dhidi ya wapiganaji kama hawa wasio na maono,” Rais Kabore alisema huku akikashifu mauaji hao yaliyotelezwa katika kijiji cha Solhan.

Kiongozi huo pia alitangaza siku tatu ya maombolezo ya kitaifa, ambao utakamilika Jumatatu mwendo wa saa tano na dakika 59. Alisema magaidi hao waliwaua raia wa umri zote na kuteketeza makazi na masoko.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres pia alilaani mauaji hayo ambayo aliyataja kama ya “kikatili”.

“Guterres anakashifu vikali shambulio hili na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza juhudi za kusaidia mataifa wanachama wa UN katika vita dhidi ya ugaidi na mauaji yasiyokubalika,” msemaji wa Katibu huyo Mkuu Stephane Dujarric akasema kupitia taarifa.

Guterres alitoa hakikisho kwa Burkina Faso kuwa UN itaisadia kikamilifu.

Naye kiongozi wa upinzani nchini Burkina Faso Eddie Komboigo aliitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha kabisa “mauaji ya watu wetu”.

Alitaka hatua zote zichukuliwe kulinda maisha ya raia wa nchi hiyo inayozongwa na machafuko yanayosababishwa na magaidi.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Shelly-Ann Fraser wa Jamaica asajili muda wa pili bora...

New Delhi yalegeza masharti ya kudhibiti corona baada ya...