• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Shelly-Ann Fraser wa Jamaica asajili muda wa pili bora zaidi duniani katika mbio za mita 100

Shelly-Ann Fraser wa Jamaica asajili muda wa pili bora zaidi duniani katika mbio za mita 100

Na MASHIRIKA

MTIMKAJI Shelly-Ann Fraser wa Jamaica sasa ndiye mwanamke wa pili mwenye kasi zaidi duniani baada ya kusajili muda wa sekunde 10.63 katika mbio za mita 100 katika uwanja wa Olympic Destiny jijini Kingston mnamo Jumamosi.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34 ndiye bingwa wa dunia na mshindi mara mbili wa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 100 kwenye Olimpiki.

Marehemu Florence Griffith-Joyner aliyekuwa mwanariadha wa Amerika ndiye mwanamke wa pekee aliyewahi kukamilisha mbio za mita 100 kwa muda wa sekunde 10.49.

Muda ulioandikishwa na Fraser-Pryce mnamo Jumamosi ulimwezesha kuvunja rekodi bora ya awali ya dunia ya sekunde 10.72 iliyowekwa na Sha’Carri Richardson wa Amerika mnamo Machi 2021.

Hadi kufikia Jumamosi, Fraser-Pryce alikuwa akishikilia na Elaine Thompson-Herah rekodi ya kitaifa ya Jamaica katika mbio za mita 100 kwa muda wa sekunde 10.70. Alikuwa akijivunia muda bora wa sekunde 10.84 msimu huu aliposhuka dimbani kutifua kivumbi cha Jumamosi kilichokuwa kimeandaliwa na Chama cha Kitaifa cha Olimpiki nchini Jamaica kwa ushirikiano na Shirikisho la Usimamizi wa Masuala ya Riadha nchini Jamaica.

Fraser-Pryce alianza vyema mbio hizo huku pengo kubwa likitamalaki kati yake na Natasha Morrison na Kashieka Cameron walioambulia nafasi za pili na tatu kwa muda wa sekunde 10.95 na 11.39 mtawalia.

Fraser-Pryce aliyeibuka bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 100 mnamo 2008 na 2012, alikuwa akishiriki shindano lake la nne katika mbio hizo msimu huu.

“Kusema kweli sikutarajia kukimbia kwa kasi kiachi hicho hapa Kingston. Nashukuru Mungu kwamba nilitimka vizuri na kukamilisha mbio hizo salama. Aidha, sikuwa na presha kwa sababu nilipania tu kutumia mbio hizo kujipima kabla ya mchujo wa kitaifa utakaotumiwa kuteua kikosi kitakachowakilisha Jamaica kwenye Olimpiki zijazo za Tokyo, Japan,” akasema Fraser-Pryce.

“Iwapo nimeweza kusajili sekunde 10.6, basi ina maana kwamba nina uwezo wa kuimarisha zaidi maandalizi yangu, kuboresha muda huo kwenye mchujo wa kitaifa na hata kuvunja rekodi nchini Japan,” akaongeza.

Fraser-Pryce kwa sasa amevunja rekodi za kitaifa zilizokuwa zikishikiliwa na Waamerika Marion Jones (10.65) na Carmelita Jeter (10.64) katika mbio hizo za mita 100.

“Japo ufanisi huu unaridhisha zaidi, sitatosheka nao. Nalenga kuwa sehemu ya timu ya taifa na kufanya mambo makubwa zaidi kwenye Olimpiki,” akaongeza Fraser-Pryce.

Ni wanariadha watatu wa kwanza pekee kwenye mchujo wa kitaifa utakaondaliwa na Shirikisho la Riadha la Jamaica mnamo Juni 24-27 ndio watateuliwa kuwakilisha taifa hilo katika mbio za mita 100 kwenye Olimpiki za Tokyo zitakazofanyika kati ya Julai 23 na Agosti 8, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

BURUDANI: Aamini yupo pazuri kutinga upeo wa kimataifa...

Kundi la kigaidi laua raia 138 Burkina Faso