• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Mlipuko Beirut mwaka 2020 wasababishia raia umaskini

Mlipuko Beirut mwaka 2020 wasababishia raia umaskini

Na MASHIRIKA

BEIRUT, Lebanon

MWAKA mmoja baada ya mlipuko kutokea jijini Beirut na kuwaua zaidi watu 200, familia zinaendelea kuteseka huku uchumi wa Lebanon nao ukizidi kuporomoka.

Tangu mlipuko huo uliotokea Agosti 4, viwango vya umaskini vinaendelea kuongezeka huku familia nyingi zikishindwa kumudu hata chakula kwa siku moja.

Mlipuko huo ulitokea wakati ambapo vilipuzi vilivyohifadhiwa vibaya vililipuka na kusababisha maafa na hasara kubwa.

Aidha zaidi ya watu 6,500 waliumia mno wakati wa mlipuko huo huku uchumi wa Lebabon ukiendelea kushuka na thamani ya sarafu ya nchi hiyo ikishuka kimataifa.

Hali hiyo imekuwa mbaya zaidi kutokana na uwepo wa janga la corona ambalo pia limeathiri nchi hiyo pakubwa.

Serikali ambayo pia imelemewa na ukosefu wa fedha imekuwa ikikumbwa na uhaba wa mafuta ya petroli, dawa na bidhaa muhimu ambazo zimechangia kupanda kwa bei ya bidhaa.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN), raia wa Lebanon wamekuwa wakitumia umeme kwa mgao huku wengi wakikosa maji safi ya kutumia nyumbani.

“Mamia ya watoto wanaendelea kulala njaa. Familia nyingi pia hazina umeme wa kuwasaidia katika kuhifadhi dawa na vyakula huku maradhi nayo yakizidi kuongezeka,” ikasema ripoti ya UN.

Ikaongeza: “Watoto wengi huenda wakakumbwa na utapia mlo iwapo wataendelea kukaa njaa na hata kukosa vyakula vya kutosha.”

Kudhihirisha kwamba hali inazidi kuwa mbaya, asilimia 47 za raia wapo katika hatari ya kufa njaa. Pia wanawake wanakosa sodo, mafuta ya kupikia na hata petroli.

Hali ni mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 kutoka Syria pia wamekuwa wakiishi Lebanon.

Asilimia 90 ya wakimbizi hao nao hawawezi kupata chakula wakitegemea misaada kutoka mashirika ya umoja wa Mataifa.

Familia za waathiriwa wa mlipuko huo nao wametoa wito walipwe fidia pamoja na uchunguzi wa ndani kuhusu kiini cha tukio hilo.

Wakosoaji nao pia wameshutumu serikali kwa kubuni jopo la kumchunguza aliyekuwa Waziri Mkuu Hassan Diab pamoja na mawaziri wanne ambao walilazimika kujiuzulu kutokana na mlipuko huo.

Bunge la Lebanon nalo limekuwa likijikokota kuhusu mlipuko huo na limekataa kuagiza baadhi ya mawaziri wafike na kujibu maswali yaliyoibuliwa kutokana na mlipuko huo.

You can share this post!

WASONGA: EACC itaje wazi watumishi wa umma wachapao siasa

Msimu wa talaka