• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Mzozo Tunisia wazidi kutokota Rais akimtimua waziri wa ulinzi

Mzozo Tunisia wazidi kutokota Rais akimtimua waziri wa ulinzi

Na AFP

TUNIS, Tunisia

RAIS wa Tunisia, Kais Saied, amemfuta kazi waziri wa ulinzi siku moja tu baada ya kumtimua waziri mkuu na kuvunja Bunge.

Hatua hiyo imetumbukiza Tunisia – yenye demokrasia changa – katika mtanziko kikatiba, wakati huu inakumbana na changamoto za janga la Covid-19.

Ghasia zilizuka Jumatatu nje ya Bunge lililozingirwa na wanajeshi, baada ya Saied kumtimua Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kuamrisha vikao vya bunge kusitishwa kwa siku 30, hatua iliyotajwa na upinzani kama “mapinduzi ya serikali.”

Mnamo Jumapili, Rais alitangaza kufanya “maamuzi muhimu ili kuiokoa Tunisia, taifa na raia wa Tunisia,” kufuatia maandamano katika miji kadhaa kulalamikia jinsi serikali ilikuwa ikishughulikia janga la Covid.

Rais huyo, ambaye kikatiba anadhibiti jeshi, alionya dhidi ya kuchukua silaha akisema yeyote “atakayefyatua risasi hata moja, vikosi vyetu vitamimina mvua ya risasi.”

Mnamo Jumatatu adhuhuri, taarifa kutoka kwa afisi ya rais ilitangaza kuhusu kutimuliwa kwa Waziri wa Ulinzi Ibrahim Bartajina, kaimu waziri wa haki Hasna Ben Slimane, ambaye pia ni msemaji wa serikali.

You can share this post!

Zogo lakumba fidia ya wavuvi Lamu

Chipukizi wa Uingereza U-21 wapata kocha mpya