• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Papa Francis akamilisha ziara yake Sudan Kusini

Papa Francis akamilisha ziara yake Sudan Kusini

Na AFP

JUBA, SUDAN KUSINI

PAPA Francis jana Jumapili alikamilisha ziara yake nchini Sudan Kusini kwa kuongoza ibada kubwa ya wazi baada ya kuhimiza viongozi kulenga kurejesha amani nchini humo.

Taifa hilo limezongwa na mapigano na umasikini huku raia wengi wakiishi katika mataifa jirani kama wakimbizi.

Ziara hiyo ya siku tatu ndio ya kwanza kwa Papa Francis kufanya Sudan Kusini, taifa lenye idadi kubwa ya Wakristo lililopata uhuru kutoka Sudan, mnamo 2011.

Baada ya nchi hiyo kupata uhuru ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya karibu watu 400,000 huku wengine zaidi ya milioni nne wakafurushwa makwao.

Licha ya mkataba wa amani kutiwa saini 2018 kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza Riek Machar, mapigano yangali yanashuhudiwa sehemu mbalimbali Sudan Kusini.

Watu bado wanahama makwao na kusaka hifadhi katika kambi za wakimbizi.

Papa Francis, ambaye binafsi amejaribu kuhimiza amani wakati wa vita, alipata mapokezi mazuri nchini Sudan Kusini.

Maelfu ya watu walihudhuria ibada hiyo katika eneo kulikojengwa mnara wa ukumbusho wa marehemu John Garang.

Mnara huo ulijengwa kwa heshima ya Rais huyo wa zamani na shujaa wa vita vya ukombozi wa Sudan Kusini aliyekufa mnamo 2005.

Mnamo Jumamosi, Francis alikutana na waathiriwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambao waliletwa jijini Juba kutoka kambi mbalimbali.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki pia alitoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini kurejesha “heshima” kwa mamilioni ya watu walioathiriwa na vita hivyo.

“Ni jambo la kuhuzunisha kwamba katika nchi hii, imekuwa ni jambo la kawaida kuwa mtu aliyepoteza makazi au mkimbizi,” akasema Papa Francis.

“Ningetaka kurejelea wito wangu kwa viongozi kwamba wasaidie kukomesha vita na watoe kipaumbele kwa mchakato wa kuleta amani. Raia wanafaa kuishi maisha yenye heshima. Mustakabali wa watu hauwezi kupatikana katika kambi za wakimbizi pekee,” akaeleza huku akishangiliwa.

Sudan Kusini ina jumla ya wakimbizi 2.2 milioni wa ndani kwa ndani na wengine milioni mbili walioko nchi za nje, hivyo kuwa taifa lenye changamoto kubwa la wakimbizi barani Afrika.

John Wiyual, ambaye ameishi katika kambi kubwa ya wakimbizi nje ya Juba tangu 2014, alisema hakubaliani na hakikisho kutoka kwa serikali kwamba nchi hiyo ni salama.

“Wanasema kuna amani—- lakini kuna mauaji katika majimbo yote,” akasema Wiyual mwenye umri wa miaka 42.

“Papa anaweza kutusikiza. Sisi ni raia na tunahitaji amani,” akaongeza.

Ziara ya Papa Francis ilifuatiliwa kwa ukaribu na jumla ya raia 12 milioni wa Sudan Kusini.

Viongozi wa kidini walitoa mchango mkubwa katika kulinda raia wakati wa vita vya uhuru na mapigano ya kikabiliwa ya kati ya 2013 na 2018.

Karibu watu 50, 000 walifurika katika mnara wa Garang Jumamosi jioni mwa maombi ya pamoja yaliyoongozwa na Francis.

  • Tags

You can share this post!

Harry Kane avunja rekodi ya Jimmy Greaves na kuwa mfungaji...

TALANTA YANGU: Dogo mkali wa kubofya piano

T L