• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Raia wa Uganda wafurika Kenya kununua bidhaa

Raia wa Uganda wafurika Kenya kununua bidhaa

NA DAILY MONITOR

MAMIA ya raia wa Uganda wanavuka mpaka wa Busia kuingia nchini Kenya ili kununua bidhaa kama vile vitambaa na mavazi kwa bei nafuu kabla ya sikukuu ya Krismasi.

Bw David Basalirwa, ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Wilaya ya Bugiri Mashariki nchini Uganda, anasema yeye hupendelea kununua mavazi kutoka Kenya.

Bw Basalirwa anaeleza kuwa bei ni nafuu ikilinganishwa na masoko yaliyo karibu naye katika wilaya ya Iganga na miji mingine ya Uganda.

“Huwa ninanunua nguo nyingi Kenya kwa Sh1,000 (sawa na Sh24,000 za Uganda), lakini kwa pesa hizi hapa Uganda mimi hununua nguo moja pekee,” Bw Basalirwa akasema akiongeza kuwa unafuu wa bei ya mavazi Kenya unampa ‘faida nzuri’ akiyauza kwao Uganda.

Haya ni mabadiliko ya ghafla ikilinganishwa na awali kwani Wakenya wamekuwa wakifurika nchini Uganda kununua mavazi.

Hali hii tofauti imechangiwa kwa kiasi fulani na kudororoa kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu ya Dola ya Marekani ambapo pia sarafu za mataifa ya kigeni zimeanza kupata nguvu.

Mwaka 2022 Sh1 ya Kenya ilikuwa sawa na Sh35 za Uganda.

Lakini sasa imeshuka thamani ambapo Sh1 ni sawa na Sh24.5 za Uganda katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

Bi Debora Babirye, aliyesafiri kutoka Wilaya ya Namayingo hadi mjini Busia mpakani mnamo Jumatatu kununua mapazia Kenya, anasema bei hizi nzuri zinasukuma wafanyabiashara kufurika Kenya kununua nguo ili wapate ‘faida nzuri’ katika msimu wa sherehe.

Bi Babirye anasema alinunua jozi mbili za pazia kwa Sh400 (sawa na Sh9,000 za Uganda) na anatarajia kuuza kwa bei ya juu.

Naye Bw Ivan Wandera, mkazi wa Busime katika wilaya ya Busia anadokeza kuwa alivuka mpaka kununua suruali kwa bei ya chini.

“Nilinunua kila jozi ya suruali kwa Sh250 (sawa na Sh6,000 za Uganda). Bidhaa hizo huku zingenigharimu angalau Sh15,000 za Uganda hapa nyumbani (Uganda),” anaeleza.

Mfanyabiashara wa Kenya katika Wadi ya Burumba Busia-Kenya Bw James Wanjala, anasema kuwa ‘ameshangazwa’ na idadi kubwa ya raia wa Uganda wanaoingia nchini Kenya kununua bidhaa, akiongeza kuwa hajawahi kuwaona wakijaa katika maduka ya Kenya.

“Uchumi wa Uganda ni bora kuliko wa Kenya na raia wa Uganda wana pesa za kununua kwa bei yoyote,” akasema Bw Wanjala.

“Tuna chini ya juma moja kufika Krismasi na bado sijanunua chakula na nguo za watoto na mke wangu,” akaongeza.

Bw Baker Ssebanakitta, raia wa Uganda mkazi wa mpakani, anaeleza kuwa ameona Wakenya wakivuka mpaka kwenda Uganda kununua chakula na mavazi lakini raia wa Uganda aghalabu hununua mavazi.

Mkazi wa Busia-Kenya Bw Eddy Juma naye akasema alikuwa Uganda kununua “mavazi bora” licha ya bei ya juu.

Kwa moto uo huo Mkenya Bi Christine kutoka Kakamega anadokeza kuwa hupendelea kununua kitenge cha rangi tofauti na usanifu ambacho huvaliwa na wanawake wa Uganda kwa sababu ya “thamani yake nzuri.”

Mfanyabiashara wa malimali Uganda mpakani, Bw Ibrahim Wairagala, anaeleza kuwa mauzo yake yako chini yakilinganishwa na miaka iliyopita.

“Awali, Wakenya wangefurika madukani mwetu wakati wa Krismasi, lakini Krismasi hii, idadi iko chini,” alisema Bw Wairagara.

Mjasiriamali wa vitambaa, Bw Francis Magambo, analaumu kufifia kwa nguvu ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu nyingine kwamba kumeshusha biashara.

TAFSIRI NA LABAAN SHABAAN

  • Tags

You can share this post!

Krismasi: Wafugaji kuku waripoti kuongezeka kwa visa vya...

Krismasi: Hofu chang’aa itavuruga wengi Park Road

T L