• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Rais Conde alivyochotwa na makomando wa kijeshi

Rais Conde alivyochotwa na makomando wa kijeshi

Na MASHIRIKA

CONAKRY, GUINEA

MAKOMANDO walizingira Ikulu katika eneo la Kaloum jijini Conakry na kufyatua risasi katika juhudi za kutaka kumkamata Rais Alpha Conde, 83.

Walinzi wa rais walifyatuliana risasi na makomando hao walioongozwa na Kanali Mamady Doumbouya, lakini walilemewa.

Makomando hao waliingia ndani ya Ikulu na kumkamata Rais Conde na kisha kuondoka naye.

Mapema asubuhi, serikali ilijaribu kuwaondolea hofu raia wa Guinea baada ya wizara ya ulinzi kusema kuwa jaribio la mapinduzi lilitibuliwa na walinzi wa rais ambao walifanikiwa kuwadhibiti makomando hao.

Baadaye, picha ya video ilichipuka mitandaoni ikionyesha Rais Conde akiwa mchovu na akiwa mchafu – ishara kwamba huenda alizabwa makofi kadhaa na kubururwa chini wakati wa kukamatwa.

Katika video hiyo, Rais Conde anaonekana akiulizwa na mmoja wa wanajeshi ikiwa aliteswa; lakini anakataa kujibu.

Baadaye, Kanali Doumbouya huku akizungukwa na wanajeshi wanane waliokuwa na bendera ya Guinea, alitangaza kuwa serikali ya Rais Conde ilipinduliwa.

Kanali Mamady Doumbouya aliyeongoza makomando wengine kumng’atua Rais Conde wa Guinea. Picha/ AFP

Makomando hao walitangaza kutupiliwa mbali kwa katiba, kufungwa kwa mipaka na marufuku ya kutokuwa nje usiku.Kanali Doumbouya pia aliwatimua magavana wote na nafasi zao kuchukuliwa na makamanda wa jeshi wa mikoa.

Alisema kuwa Rais Conde yuko salama kizuizini lakini hatima yake bado haijulikani.

Balozi wa mojawapo ya mataifa ya Ulaya, alinukuliwa na shirika moja la habari la kimataifa akisema kwamba Conde alinyakwa na makomando hao kufuatia hatua yake ya kutimua mmoja wa makamanda wa kikosi hicho.

Kanali Doumbouya aliambia mashirika ya habari ya Ufaransa kuwa mapinduzi hayo yaliungwa mkono na vikosi vyote vya wanajeshi.

Wanajeshi hao walitangaza kuundwa kwa kamati ya kitaifa ambayo imetwikwa jukumu la kushauriana na wanasiasa na mashirika ya kijamii kuhusiana na hatua inayofaa kuchukuliwa baada ya mapinduzi hayo.

“Hatutaruhusu tena mtu mmoja kuendesha siasa za nchi. Kila raia wa Guinea atahusishwa,” akasema Doumbouya.

Kanali huyo alisema kuwa makomando waliamua kupindua serikali kwa ajili ya masilahi ya raia wote milioni 12.7.

Alisema uchumi wa nchi hiyo haujakua tangu taifa hilo la Afrika Magharibi lilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wafaransa mnamo 1958.

Mapinduzi hayo yalifuatia siku chache baada ya bunge la nchi hiyo kupitisha hoja ya kuongeza bajeti ya Rais Conde na kupunguza bajeti ya watumishi wengine wa serikali, wakiwemo maafisa wa usalama.

Doumbouya alikuwa mwandani wa Conde na ndiye mkuu wa kikosi cha makomando. Alipewa mafunzo nchini Ufaransa na Amerika kwa lengo la kulinda Conde.

Makomando hao Jumatatu waliagiza mawaziri wote kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri huku wakionya kuwa ambao wangekosa kufika wangechukuliwa kuwa maadui.

Kanali Doumbouya alisema wanajeshi walitwaa mamlaka kwa lengo la kumaliza ufisadi na usimamizi mbovu ulioshuhudiwa wakati wa utawala wa Rais Conde.

Rais Conde ambaye amekuwa mamlakani tangu 2010, alichaguliwa kuongoza kwa muhula wa tatu mwaka jana. Alibadili katiba ya nchi hiyo ili kumruhusu kuwania kwa muhula wa tatu.

Japo Conde anasifiwa kwa kujaribu kuinua uchumi, amekuwa akishutumiwa kwa kukiuka haki za kibinadamu na kuhangaisha wapinzani wake.

Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Maendeleo la Mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) yamewataka wanajeshi hao kukabidhi raia hatamu za uongozi.

“Ninashutumu vikali hatua ya wanajeshi kutwaa serikali kwa risasi. Rais Conde aachiliwe mara moja,” akasema Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iviondoe vizingiti vya CBC

Kipa Ederson Moraes sasa kudakia Man-City hadi 2026