• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Rais Samia Suluhu asutwa kwa ‘kuumbua’ wanasoka wa kike nchini Tanzania

Rais Samia Suluhu asutwa kwa ‘kuumbua’ wanasoka wa kike nchini Tanzania

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, TANZANIA

RAIS Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekashifiwa vikali kwa kutaja wanasoka wa kike nchini mwake kuwa na “vifua tambarare” na kutovutia wanaume wa kuwaoa.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa mwenyeji wa timu ya taifa ya Tanzania ya chipukizi wa kiume wasiozidi umri wa miaka 23 katika Ikulu ya Rais jijini Dar es Salaam.

Suluhu, 61, ndiye rais wa kwanza wa kike nchini Tanzania. Katika mahojiano yake ya hivi majuzi na BBC, alikiri kwamba idadi kubwa ya Watanzania walitilia shaka uwezo wake wa uongozi akiwa rais kutokana na jinsia yake.

“Hata wafanyakazi wangu serikalini walinipuuzilia mbali awali na kunitaja kama mwanamke kama yeyote mwingine tu. Lakini walikuja baadaye kuniamini na kutambua ukubwa na upekee wa uwezo wangu,” akasema.

Kauli yake ya hivi karibuni kuhusu wanawake hata hivyo imechemsha hasira za Watanzania huku Catherine Ruge ambaye ni Mbunge wa zamani na mkuu wa kitengo cha masuala ya wanawake katika chama pinzani cha Chadema akisema: “Matamshi ya Suluhu kuhusu wanawake ni dharau kubwa.”

Mtafiti wa masuala ya jinsia na uana pamoja na matatizo ya kiakili nchini Tanzania, @Sajokm alisema “ameduwazwa sana” na kauli ya Suluhu.

@bomba_mudolo aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter: “Wapi haki za wanawake wetu? Mama Samia anastahili kuwashajiisha wanawake wetu wa Kiafrika ili watambe katika talanta zao badala ya kuwaumbua.”

Kwa upande wake, Henry Ngogo aliuliza: “Hii ni sawa na kusema kwamba maisha hayana maana yoyote bila ndoa?”

Rais Samia alishikilia kuwa japo wanasoka wa kike wanavunia Tanzania tija na fahari tele kwa kushinda mataji mengi ya haiba, baadhi yao hawana kabisa nafasi ya kuolewa kwa sababu ya muonekano wao.

“Hata tukiwaleta hapa watunge foleni, kunao wenye vifua tambarare visivyoweza kabisa kuinua marinda yao kwenye sehemu za juu kwa sababu hawana matiti ya kuonekana. Unaweza kudhani ni wanaume. Inasikitisha kwamba ndoa kwa wanawake hawa wanaocheza soka ni jambo ambalo tayari limezikwa katika kaburi la sahau,” akaeleza.

Katika hotuba yake, Samia alikiri kwamba maisha ya wanamichezo wengi ni magumu na akataka mamlaka husika nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanamichezo hao wanashughulikiwa ipasavyo wanapostaafu.

Aliungama kuwa maisha ya wanawake wanaoshiriki michezo ndiyo huwa magumu zaidi kwa sababu hata “miguu yao huwa imechoka kabisa baada ya kustaafu ulingoni.”

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ruto aidhinisha Ngirici kwa kiti cha ugavana Kirinyaga

Maandalizi ya KCB Machakos Rally yapamba moto