• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Maandalizi ya KCB Machakos Rally yapamba moto

Maandalizi ya KCB Machakos Rally yapamba moto

Na GEOFFREY ANENE

MADEREVA matata Baldev Chager, Karan Patel na Carl “Flash” Tundo wameimarisha maandalizi yao kabla ya duru ya tano ya Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) KCB Machakos Rally hapo Agosti 29.

Pia, kuna madereva Eric Bengi, Jasmeet Singh Chana na Issa Amwari pamoja na dereva mlemavu Nikhil Sachania, Paras Pandya, Andrew Muiruri na Aakif Virani, miongoni mwa wengine.

“Duru iliyopita katika maeneo ya Voi ilikuwa nzuri kwangu kwa hivyo naamini gari hili langu la Mitsubishi Evolution X liko tayari kwa duru inayokuja. Mimi na mwelekezi wangu Charan Singh tunaongoza daraja ya pili na tunataka kuendelea kukalia juu ya jedwali katika duru ya Machakos, Mungu akipenda,” alisema Nikhil.

Matayarisho ya KCB Machakos Rally yamepamba moto, huku Agosti 28 ikitengwa kuwa siku ya madereva kufanya majaribio katika barabara zitakazotumika.

Magari na stakabadhi za kushiriki mashindano hayo zitakaguliwa hapo Agosti 28 mtaani South “C” jijini Nairobi.

Mkurugenzi wa KCB Machakos Rally, Jim Kahumbura alisema kuwa mbio zenyewe zitafanyika katika barabara za mawe kwenye shamba la Lisa Farm zikijumuisha kilomita 146.00. Tundo na Chager wanaongoza jedwali la daraja ya juu kabisa kwa alama 79 wakifuatiwa na Onkar Rai (73) na Patel (58).

You can share this post!

Rais Samia Suluhu asutwa kwa ‘kuumbua’ wanasoka...

TAHARIRI: Serikali isidunishe uvaaji sare shuleni