• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Spika aliye mwiba kwa Trump kuongoza Congress muhula wa 4

Spika aliye mwiba kwa Trump kuongoza Congress muhula wa 4

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

SPIKA wa Bunge la Congress nchini Amerika, Nancy Pelosi, ni kati ya viongozi mashuhuri zaidi nchini humo na duniani; kutokana na cheo hicho kinachomweka hatua mbili kurithi kiti cha urais wa taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani.

Mwaka 2020 Pelosi aligonga vichwa vya habari mara kwa mara kutokana na mikwaruzano aliyokuwa nayo na serikali ya Rais Donald Trump.

Sasa Pelosi amechaguliwa tena kwa awamu ya nne kama spika wa Congress, katika kura iliyoandaliwa siku ya Jumapili bungeni humo.

Kiongozi huyo alitetea wadhifa wake kwa kuzoa kura 216 zilizopigwa na wawilikishi wa chama cha Democrat, licha ya chama hicho kilipoteza viti 11 vya uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa Novemba – sasa kina wabunge 222 dhidi ya 216.

Wadhifa wa hadhi kuu

Huku Kamala Harris akitarajiwa kuchukua usukani kama makamu wa rais wa kwanza mwanamke wa Marekani, nyadhifa za juu mbili za kisiasa katika taifa hilo lenye uchumi na ushawishi mkubwa zaidi duniani, sasa zitashikiliwa na viongozi wanawake.

Harris na Rais-mteule Joe Biden walishinda uchaguzi mkuu wa Novemba iliyopita kwa tiketi ya Democrat.

Katika muda ambao Pelosi, mwenye umri wa miaka 80, amekuwa Spika wa Congress ameonyesha kuwa ana ufahamu pana wa masuala ya kisheria na uongozi wa bunge hilo.

Wadhifa wa Spika ni kati ya zile zenye hadhi ya juu kulingana na Katiba ya taifa hilo – ni wa tatu baada ya ule wa Rais na Makamu wa Rais.

Spika, manaibu wake pamoja na wenyekiti wa kamati mbalimbali wana afisi za hadhi jijini Washington DC. Kwa pamoja wanahusika katika kutambua hoja zinazowasilishwa na kupigiwa kura katika Bunge la Congress.

Kati ya 2009-2011, Pelosi kupitia afisi yake alipitisha bungeni sheria ya kufadhili bajeti ya Sh91 trilioni ili kuokoa uchumi wa nchi hiyo; ambayo nusura iporomoke mnamo 2008 kutokana na msukosuko mkubwa wa kiuchumi uliokumba ulimwengu wakati huo, ulioanzia Marekani.

Pia alichangia kupitishwa kwa mswada wa huduma bora za afya kwa bei nafuu, almaarufu Obamacare kwani ulipigiwa upato na kupitishwa kipindi cha pili cha uongozi wa rais wa wakati huo Barack Obama.

Wakati wa mijadala kuhusu masuala tata hasa ya uongozi wa Trump, mwanamke huyo aliwaunganisha wanachama wa Democrat kupinga sera ambazo alihisi zinadhulumu raia na kutatiza uchumi wa Waamerika.

Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020 Trump na Pelosi walitofautiana vikali kuhusu kupunguzwa kwa ushuru wanaolipa wananchi ili kuwapa nafuu ya muda, baada ya uchumi na maisha kwa jumla kuvurugwa na janga la virusi vya corona.

Pia, mara nyingi wawakilishi wa chama tawala cha Republican wamemsifu Pelosi kama mwanasiasa mzoefu na mwenye msimamo wa kipekee asiyetikiswa na mawimbi ya utawala ulio mamlakani.

Ndiposa chama cha Democrat kilikuwa na imani na uongozi wake na kuwa shupavu kukashifu au kupinga sera za Trump huku wakipitisha sheria za kuwanasua raia wa Marekani na uchumi wa nchi.

Safari ya Kisiasa

Kifamilia, Pelosi alilelewa katika jamii ambayo ina mizizi ya kisiasa – ndiye mzaliwa wa saba katika watoto saba.

Alizaliwa jijini Baltimore, Maryland, ambako marehemu babake alikuwa akihudumu kama meya.

Akasomea katika taasisi moja inayopatikana jiji kuu la Washington DC ambako alikutana na mwanauchumi Paul Pelosi.

Msomi huyo mwishowe alimuoa wakaanzisha familia ambayo imejaaliwa watoto watano – mabinti wanne na mvulana, ambao wamezamia taaluma mbalimbali.

Safari ya Pelosi katika mawanda ya kisiasa ilianza mnamo 1976 alipotumia mizizi ya kisiasa ya familia yake kumsaidia Gavana wa California, Jerry Brown, aliyekuwa akiwania tiketi ya urais, kushinda mchujo wa chama cha Democrat katika eneo la Maryland.

Alikwea ngazi na kuwa mwenyekiti wa Democrat katika jimbo hilo la California na kufikia 1988 alishinda kiti cha Congress.

Aliwakilisha jamii ya mji huo ambao una watu wengi mashoga ndipo akapigania kuongezwa kwa msaada wa kifedha kwa jamii hiyo.

Mnamo 2001, aliwania cheo cha Kiranja wa Wachache katika Congress na kushinda.

Wadhifa huo ndio wa pili kwa chama chenye wawakilishi wachache bungeni.

Mwaka 2020 alipandishwa cheo na kutwaa nafasi ya Kiongozi wa Wachache na kuongoza Wanademocrats kuendeleza upinzani ndani ya Bunge.

Itakumbukwa kwamba alikuwa kati ya wanasiasa wakuu wenye usemi mkubwa ambao walipinga uvamizi wa Marekani nchini Iraq mnamo 2003.

Kuchaguliwa Spika

Msimamo huo ulichangia kupanda kwa umaarufu wake na baada ya chama cha Democrat kuchukua usukani bungeni mwaka 2006, alichaguliwa kama spika wa kwanza mwanamke katikia historia ya taifa hilo.

Miaka minne baadaye, wadadisi wengi walifikiria mwisho wa siasa za Pelosi ulikuwa umetimia baada ya chama kupoteza uthibiti wa Congress; lakini alionyesha uongozi shupavu na kukisaidia kuendelea kuwika bungeni.

Lakini alirejea kwa kishindo baada ya Wanademocrats kushinda idadi kubwa ya viti vya uwakilishi mnamo 2018.

Akakalia tena kiti cha Spika kwa awamu ya tatu; na huo ukawa mwanzo wa mkwazurano kati ya Bunge hilo na utawala wa Rais Trump.

Mara nyingi miswada iliyodhaminiwa na chama cha Republican katika Congress ilikosa kupitishwa, hali iliyomweka pabaya na serikali tawala pamoja na Kiongozi wa Wengi Mitch McConnell, ambaye ni mwandani wa Trump.

Mwezi mmoja tu baada ya kuchaguliwa Spika mnamo 2018, Pelosi alivuruga hotuba ya Rais Trump kwa kupiga makofi kwa njia ya kejeli, wakati wa kikao hicho rasmi kinachohusudiwa sana nchini Amerika.

Miezi 12 baadaye alirarua karatasi yenye hotuba ya Trump na kushutumiwa kwa kumkosea rais huyo heshima.

Hata hivyo, alikaa ngumu na kujitetea kwamba hotuba hiyo haikuwa na maana kwa Waamerika ambao hawakuwa wanafurahia utawala wake mbovu.

Mwaka 2019 Pelosi aliongoza juhudi za kumuondoa mamlakani Rais Trump kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, sababu ya masuala kadhaa tata yaliyokuwa yakizingira uongozi wake.

Moja ya masuala hayo ni kwamba Trump alijaribu kulishinikiza taifa la Ukraine kupeleleza taarifa za kumharibia sifa Rais-mteule wa sasa Joe Biden.

Inadaiwa Trump alitaka kutumia vibaya mamlaka yake kutishia kuondoa msaada wa kiusalama kwa taifa hilo la kigeni.

Hata hivyo, hoja ya kumtimua Trump haikupita hatua ya mwisho kwani wabunge wa Republican, ambao ndio walikuwa wamedhibiti Bunge la Seneti, waliiangusha.

Changamoto mpya

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 kulikuwa na matarajio kwamba Wanademocrat wangeongeza idadi ya wabunge wao katika Congress, lakini waliishia kushindwa katika maeneo kadha waliyokuwa wakishikilia.

Ingawa hawakupoteza udhibiti wa Congress, idadi yao imepungua.

Wadadisi wa kisiasa wamesema kupungua kwa idadi hiyo kutafanya iwe vigumu kwa Pelosi kuendeleza sera za Rais-mteule Joe Biden kwa kuwa ushawishi wa Trump bado unahisiwa sana katika mabunge ya Congress na Seneti.

Mwanahabari wa shirika la BBC, Anthony Zurcher, anasisitiza hilo akisema ushindi mwembamba wa Pelosi mnamo Jumapili ni ithibati tosha kwamba mambo yatakuwa magumu miaka minne ijayo baada ya Biden kuapishwa baadaye Januari 20.

“Lazima atafute mbinu ya kuwashawishi baadhi ya wawakilishi wa Republican kuunga sera za Biden. La sivyo, huu utakuwa mwisho wake. Uwezekano wa pekee wa kazi yake kufanywa rahisi ni iwapo chama cha Democrat kitadhibiti pia Bunge la Seneti. Lakini hilo pia linategemea matokeo ya kura ya jana Jumanne,” akasema Bw Zucher.

Alikuwa akirejelea uchaguzi wa useneta katika jimbo la Georgia ambapo viti viwili vinavyoshikiliwa na maseneta wa Republican.

Chama cha Democrat kinashikilia viti 48 kwa sasa katika Seneti huku Republican wakiwa na wawakilishi 50.

Iwapo wanademocrat watazoa viti viwili vinavyoshindaniwa Georgia, bunge hilo litakuwa nusu bin nusu (50-50).

Makamu rais-mteule Harris, mwenyewe akiwa ni mwanademocrat, atatakiwa kupiga kura ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu miswada itakayoletwa katika Seneti; kumaanisha wanademocrat watakuwa na kura moja zaidi.

“Kwa kweli ana sifa za kuwadhibiti wawakilishi wa chama chake cha Democrat ili wawe na msimamo mmoja. Hilo ndilo limemsaidia sana wakati huu wa utawala wa Trump. Hata hivyo, uongozi wake unaweza kumfaa sana Rais-mteule Joe Biden kupitisha ajenda zake kwa Waamerika,” alieleza mwanahabari Zurcher kumhusu Pelosi.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Hussein Kassim

Wataalam watarajiwa China kuchunguza kiini cha corona