• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Tshisekedi azidi kuudhibiti usemi wa Kabila serikalini

Tshisekedi azidi kuudhibiti usemi wa Kabila serikalini

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

RAIS wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi anaonekana kupiga hatua katika kudhibiti serikali yake baada ya wabunge kumuunga mkono kwenye nia yake ya kusambaratisha muungano wake na mtangulizi wake Joseph Kabila.

Mnamo Ijumaa wiki jana, wabunge 301 kati ya wote 500 walipigia kura hoja ya kumwondoa Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba ambaye ni mwandani wa Rais Mstaafu Kabila.

Baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Januari 2018 ambapo aliungwa mkono na rais huyo mstaafu, Tshisekedi aliingia kwenye mkataba wa kisiasa na chama chake Kabila ambacho kilikuwa na idadi kubwa ya viti vingi vya ubunge ili kufanikisha uongozi wake bila kutatizika.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisambaratisha muungano wake na Kabila mnamo Disemba mwaka jana, akisema umemweka mateka na hawezi kutekeleza majukumu yake ya Urais ipasavyo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Kufuatia tukio la Ijumaa, Rais huyo sasa amepiga hatua kubwa kumtema Kabila kabisa serikalini kwa kuwa hata wabunge wa chama cha kiongozi huyo aliyestaafu baada ya kuongoza kwa miaka 17, sasa wanaunga mkono ajenda zake kwa raia wa DRC.

“Kila siku tunaendelea kupiga hatua serikalini. Sina uhasama wowote na Rais Kabila ila lazima niendeshe serikali jinsi inavyotakikana kikatiba. Huu uungwaji mkono ambao naupokea hauzingatii mipaka ya vyama au kabila bali ni kwa manufaa ya raia wa DRC,” akasema Rais Tshisekedi mnamo Ijumaa akihutubu bungeni.

Kwenye hoja ya kumtimua waziri huyo mkuu wa zamani, wabunge walisema kwamba alikuwa amefeli kutekeleza majukumu yake inavyotakikana kisheria huku akitumiwa na Kabila kutatiza serikali ya Rais Tshisekedi.

“Kufeli kwa serikali kukamilisha miradi mbalimbali na kukosa kushughulikia usalama na ulinzi kumechangia hoja hii. Hawezi kuendelea kuhudumu ilhali utendakazi wake ni duni pamoja na baraza lake la mawaziri,” ikasema hoja ya kumtimua ikirejelea visa vya ghasia Mashariki mwa DRC.

Kabla ya kutangaza kuwa amesambaratisha ushirikiano wake na Kabila Disemba mwaka jana, Rais Tshisekedi alifutilia mbali mkutano wa baraza la mawaziri uliofaa kufanyika mnamo Oktoba.

Aliendelea kudhihirisha ubabe wake serikalini baada ya kumteua Seneta Modeste Bahati mnamo Januari 1 kuwa Kiongozi wa wengi kwenye Bunge la chini.

You can share this post!

Wandani wa Uhuru wamsuta Ruto kuhusu BBI

Pigo Man-City na Leicester masogora tegemeo De Bruyne na...