• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Wanawake wataka Taliban iwape vyeo

Wanawake wataka Taliban iwape vyeo

Na AFP

KABUL, AFGHANISTAN

MAANDAMANO makubwa Alhamisi yalishuhudiwa Afghanistan, baada ya wanawake kukaidi amri ya utawala mpya wa Taliban wa kukaa nyumbani, na kulalamikia kubuniwa kwa baraza la mawaziri bila nafasi kutolewa kwa mwanamke hata mmoja.

Mnamo Agosti 24 baada tu kutwaa udhibiti wa nchi hiyo, Taliban iliamuru wanawake wasifike kazini hadi kundi hilo liweke mikakati ya kiusalama ya kuwalinda dhidi ya dhuluma.

Hili lilifasiriwa kama ubaguzi na hali ikawa mbaya zaidi Taliban ilipotangaza mawaziri wapya bila hata mwanamke mmoja kupata cheo chochote.

Kundi hilo lilichukua rasmi utawala wa Afganistan mnamo Agosti 15 baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani waliokuwa wamedumisha usalama nchini humo kwa miaka 20.

Uongozi wa Taliban pia ulipiga marufuku raia kuandamana ila tu wanaweza kufanya hivyo baada ya kupokea idhini kutoka kwa wizara ya haki ambayo inasimamiwa na magaidi hao.

Hata hivyo, sharti la wanawake kutofika kazini liliwakera raia na jana maandamano yalichacha jijini Kabul, watu wakikusanyika katika ubalozi wa Pakistan kueleza kukerwa na kosa jingine la kunyimwa vyeo kwenye serikali mpya.

Wakati wa maandamano hayo, wapiganiaji wa Taliban nao waliwamiminia risiasi wanawake waliokuwa wakilalamikia kutojumuishwa kwenye baraza hilo kama njia ya kuwatimua.

Maandamano hayo hasa yalikolea sana katika mikoa ya Parwan na Nimruz.

Picha za kupigwa na kujeruhiwa kwa wanahabari wawili waliokuwa wakinasa matukio wakati wa maandamano hayo zilienea katika mitandao ya kijamii.

Wanahabari hao walipigwa vibaya na Taliban katika jiji kuu la Kabul.

“Mmoja wa wapiganaji wa Taliban alinikanyaga kichwani kisha akagonga uso wangu kwa jiwe. Walinipiga vibaya kiasi kwamba nilifikiria walitaka kuniua,” akasema mwanahabari kwa jina Naqdi ambaye ni ripota wa gazeti la Etilaat Roz, Taqu Darybai.

“Hakuna atakayetunyamazisha. Tutaendelea kupigania haki zetu,” ikasikika sauti wakati wanawake wakiandamana jijini Kabul pamoja na wenzao waliokuwa katika mkoa wa Kaskazini Mashariki wa Badakhshan.

Mnamo Jumanne, watu watatu waliuawa wakati wa maandamano katika jiji la Herat japo Taliban walikanusha kuhusika na mauaji hayo.

Kutokana na kuchacha kwa maandamano hayo, Taliban, Alhamisi iliamrisha kampuni zote za mawasiliano kukatiza huduma za mitandao, wakihofia ndiyo inaeneza uasi huo.

You can share this post!

Wabunge, maseneta wataka wanajeshi wapelekwe Laikipia...

Museveni akemea mapinduzi Guinea