• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Wabunge, maseneta wataka wanajeshi wapelekwe Laikipia kutuliza hali

Wabunge, maseneta wataka wanajeshi wapelekwe Laikipia kutuliza hali

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na Maseneta wameitaka Serikali kuwapeleka wanajeshi wa Kenya – KDF – katika Kaunti ya Laikipia kupiga jeki juhudi za vikosi mbalimbali vya Idara ya Polisi za kuleta amani eneo hilo.

Kwa upande wao maseneta waliitaka serikali kuwasilisha hoja katika mabunge yote mawili – Bunge la Kitaifa na Seneti – ili waidhinishe kupelekwa kwa wanajeshi Laikipia, wakitaja mapigano yanayoendelea Laikipia kama “ya kikatili”.

“Serikali ilete hoja katika bunge hili ili tuidhinishe kupelekwa kwa wanajeshi Laikipia. Lakini kabla ya hapo, sharti tuelezwe ni kwa nini polisi hawajafaulu kupambana na wahalifu hao,” Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Seneta Maalum Naomi Waqo ambaye alisema japo kazi yao ni kulinda mipaka yetu, ni wajibu wao pia kulinda maisha na mali ya Wakenya.

“Sharti tukomesha hali ya utovu wa usalama Kaunti ya Laikipia. Haya ni maafa na uharibifu wa mali ambao haujawahi kushuhudiwa sehemu yoyote nchini. Huenda hali hii inachangiwa na utepetevu wa maafisa wa usalama katika eneo hilo,” akasema Bi Waqo ambaye pia ndiye Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Sheria na Haki za Kibinadamu.

Bw Wetang’ula na Bi Waqo walikuwa wakitoa kauli zao baada ya Seneta wa Laikipia John Kinyua kuomba taarifa kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Ndani kuhusu hali ya usalama katika kaunti hiyo.

“Kile tunahitaji ni operesheni ya KDF kuondoa majangili. Operesheni hiyo ipangwe kwa uangalifu kiasi ili ionekane kama hatua ya kupiga jeki juhudi zinazoendelezwa na maafisa wa polisi kwa lengo la kurejesha amani Laikipia,” akasema Bw Kinyua.

Kufikia sasa, watu 10 wameuawa na familia kadhaa zikaachwa bila makao katika msururu wa uvamizi ambao umekuwa ukitekelezwa na majangili kwa kipindi cha majuma mawili yaliyopita.

Hali hii imevuruga maisha ya wakazi kiasi kwamba wengi wao sasa wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Kwa upande wao, wabunge wapatao 13 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wakiongozwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome waliunga mkono pendekezo la kupeleka wanajeshi wa KDF Laikipia.

Hata hivyo, walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai wakisema “ameshindwa na kazi”.

You can share this post!

Messi ampita Pele na kuweka rekodi mpya ya ufungaji mabao...

Wanawake wataka Taliban iwape vyeo