• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:52 PM
Watalii wafurika kupokea chanjo wenyeji wakisusia

Watalii wafurika kupokea chanjo wenyeji wakisusia

Na AFP

BELGRADE, SERBIA

MAELFU ya raia wa kigeni wameanza kuelekea Serbia kupokea chanjo dhidi ya virusi vya corona baada ya raia wa nchi hiyo kuisusia.

Huku mataifa mengi ya dunia yakihangaika kupata chanjo za kutosha za Covid-19, Serbia inakabiliwa na changamoto tofauti ya kuwashawishi raia wake kupokea chanjo hiyo ya kuokoa maisha.

Taifa hilo la eneo la Balkan lina chanjo tele kiasi kwamba linawapa raia wa kigeni wanaoweza kujifikisha humo.

Hii imesababisha kuongezeka pakubwa kwa maelfu ya “watalii wanaosaka chanjo” kutoka mataifa jirani.

Hali hiyo ilitokana na mvutano kati ya mataifa ya Mashariki na Magharibi uliowezesha Belgrade kujishindia kandarasi za karibu dozi 15 milioni kwa raia wake milioni saba.

Huku ikiwa tayari na dozi milioni tatu ambazo ni mseto wa chanjo za Pfizer, AstraZeneca, Sputnik V na Sinopharm, Serbia ambayo ni miongoni mwa mataifa maskini zaidi Uropa, imegeuka ghafla mojawapo wa eneo ambapo watu wanaweza kupokea chanjo haraka zaidi barani humo.

Hata hivyo, kulingana na serikali nchini humo, ni zaidi ya robo tu ya raia wake waliotimiza masharti ya kupokea chanjo hiyo, waliojiandikisha kuipokea.

Baada ya Serbia kuwapa chanjo waliojitokeza, watu waliacha kujitokeza tena huku idadi ikikwama.

Katika wiki mbili za mwisho mwezi Machi, idadi ya watu waliopokea dozi yao ya kwanza ilipungua hadi karibu 12,000 kila siku.

Idadi hiyo ilikuwa sawa na nusu ya idadi ya watu waliojitokeza katika kipindi sawa mnamo Februari,

Huku chanjo zikiwa kwa utele, Serbia wiki iliyopita, ilichukua hatua hiyo isiyo ya kawaida ya kuwapa raia wa kigeni fursa ya kujisajilisha kupokea chanjo hiyo.

Wahamiaji pia wamekaribishwa kupokea chanjo hiyo.

Aidha, serikali nchini humo imewahimiza raia wa Serbia ambao bado hawajapokea chanjo wajitokeze tu hata bila miadi.

“Ninawasihi nyinyi watu, pokeeni chanjo,”

“Tunazo chanjo na tutakuwa na nyingine zaidi, ninawasihi kwa jina la Mungu zipokeeni,” alisema Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic.

Madaktari nchini humo wanahofia kuwa idadi ya watu wanaopokea chanjo hiyo imefikia kilele.

“Ni wazi kuwa hakuna watu wa kutosha wanaotaka kupokea chanjo,” rais wa muungano mmoja wa madaktari Rade Panic alieleza vyombo vya habari.

Kulingana na mtaalam mkuu kuhusu mikurupuko nchini Serbia, Predrag Kon, hali hiyo ya kukataa chanjo ni “matokeo” ya habari za kupotosha kuhusu chanjo, zinazoenezwa na mitandaoni na watu wanaotaka kuzua taharuki.

You can share this post!

Pasaka ya hasara kwa wamiliki hoteli Pwani

MAKALA MAALUM: Tohara yazua utata ikiwa ifanywe kitamaduni...