• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
AKILIMALI: Mboga zinaweza kukaushwa zitumike wakati wa kiangazi au kukiwa na baa la njaa

AKILIMALI: Mboga zinaweza kukaushwa zitumike wakati wa kiangazi au kukiwa na baa la njaa

Na SAMMY WAWERU

ANN Wambui ambaye ni mkulima wa mboga tofauti katika Kaunti ya Kiambu nyakati zingine hupitia changamoto kupata soko la mazao.

Changamoto hiyo hasa inatokana na idadi ya juu ya wakulima wa mboga nchini, ikizingatiwa kuwa ni mojawapo ya bidhaa ya kula inayokumbatiwa na wananchi wengi.

Hii ina maana kuwa mazao ya mboga yanapofurika sokoni, bei huwa duni.

Wambui hukuza sukuma wiki, spinachi na mboga za kienyeji kama vile mnavu maarufu kama managu na mchicha (terere) kati ya nyinginezo.

Ukosefu wa soko la mazao nyakati zingine ukiwa kikwazo, ni pandashuka inayotishia kuzima ndoto za Wambui katika safari ya kilimo.

Huku wengi wakidhania mazao mbichi ya kilimo yanayopaswa kuongezwa thamani ni matunda, nyanya, viazi na nafaka pekee, mboga pia zinaweza kuongezwa thamani na ‘kurefusha maisha yake’.

Paul Njeru ambaye ni mkulima wa mboga Kiambu, anaendelea kufanya utafiti namna ya kuongeza mboga thamani kwa kuzikausha.

“Miaka ya kitambo, kina nyanya zetu walikuwa wakikausha mboga zinadumu muda mrefu,” Njeru anasema, akielezea kwamba ukaushaji wa mazao ndiyo njia bora kuongeza mboga thamani.

Ni mkondo ambao ukikumbatiwa na wakulima hasa wanaohangaika kupata soko, utawafaa pakubwa.

Njeru anasema kulingana na utafiti wa kina aliofanya na anaoendelea kufanya, amebaini mboga zilizokaushwa zinaweza kuhifadhika kwa muda wa miezi kadha.

Mboga hupikwa kama kitoweo kinachoandamanishwa na ugali, wali na vyakula vinginevyo.

“Mazao ya kilimo yakiongezwa thamani kama vile kwa kuyakausha yatatumika wakati kuna janga la ukame na ukosefu wa chakula, baa la njaa,” Njeru anasema.

Isitoshe, mazao yanapoongezwa thamani bei yake huongezeka. “Uongezaji thamani ukikumbatiwa, taifa litakuwa na viwanda vingi jambo ambalo litasaidia kubuni nafasi za ajira,” anaelezea Roger Wekhomba, ambaye ni mtafiti wa masuala ya kilimo.

Kwa mkulima kama Ann Wambui ambaye amekuwa akihangaika kupata soko bora la mazao, akitathmini suala la kukausha mboga huenda kilimo chake kikastawi.

You can share this post!

Chepkwony, Cheruto na Naibei kufufua uhasama wao kwenye...

Kiungo wa Santos Soccer aonyesha dalili za kuwa staa wa...