• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Chepkwony, Cheruto na Naibei kufufua uhasama wao kwenye Mbio za Nyika za AK eneo la Magharibi

Chepkwony, Cheruto na Naibei kufufua uhasama wao kwenye Mbio za Nyika za AK eneo la Magharibi

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa zamani wa nishani ya fedha katika mbio za Nelson Mandela Half Marathon, Nancy Chepkwony, atafufua uhasama kati yake na Naomi Cheruto hii leo kwenye kivumbi cha Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kitakachoandaliwa katika Shule ya Upili ya Kapsokwony, eneo la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma.

Kaunti nyinginezo za Kaskazini mwa Bonde la Ufa zitaandaa mashindano yao ya mbio za nyika katika kiwango cha kimaeneo mjini Kapenguria, Pokot Magharibi.

Wanariadha wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet wanatarajiwa kutamba katika mbio hizo ambazo zimevutia pia watimkaji kutoka maeneo ya Samburu, Trans-Nzoia, Turkana na Pokot Magharibi.

Patrick Kipsang ambaye ni mwenyekiti wa AK katika eneo la Magharibi, amesema wanatarajia ushindani mkali ambao umeshuhudiwa katika mapambano mengine ya awali katika kaunti mbalimbali.

“Tutarajie ushindani mkali hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya washiriki ni wanariadha wa haiba kubwa wanaojivunia tajriba pevu na uzoefu mpana katika ulingo wa riadha,” akasema kwa kusisitiza kwamba eneo la Magharibi limevutia washiriki wengi kutoka Kaunti za Bungoma, Vihiga, Kakamega na Busia.

Naibei ambaye aliibuka mshindi wa makala ya mwaka 2020, atatoana jasho na Susan Chebet, Nelly Cherop na Naomi Chebet wa Vihiga kadri wanavyopania kufuzu kwa mchujo wa kitaifa katika mbio hizo za kilomita 10 kwa upande wa watu wazima.

Katika kategoria ya mbio za kilomita sita kwa wasichana, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Naomi Chepkwemoi, Sharon Cheruto, Abigael Chepkwemoi wa Kaunti ya Bungoma na Doris Muhonje, Jessica Mmbone na Anita Kita kutoka Vihiga.

  • Tags

You can share this post!

Chama cha ODM chaunga mgombea wa Wiper katika uchaguzi...

AKILIMALI: Mboga zinaweza kukaushwa zitumike wakati wa...