• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Ufugaji wa mbuzi wa maziwa una faida, mfugaji hahitaji nafasi kubwa

AKILIMALI: Ufugaji wa mbuzi wa maziwa una faida, mfugaji hahitaji nafasi kubwa

Na SAMMY WAWERU

IKIWA kuna ufugaji anaouvulia kofia uite wa mbuzi wa maziwa, kutokana na manufaa yake kiafya na kimapato.

Ruth Mburu na mamake ni wafugaji wa ng’ombe, kuku na mbuzi Kaunti ya Kiambu, na anakiri faida za mbuzi ni tele.

“Mama hakuanza ufugaji wa mbuzi, leo, jana wala juzi…alianza kitambo tukiwa wangali wadogo kiumri,” Ruth anasema.

Kulingana na mwanadada huyu ambaye sasa ni mama, mbuzi ni kati ya mifugo waliochangia mamake kuikithi familia yake riziki, kulipia wanawe karo na kuikimu mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

“Alikuwa anafanya mauzo ya maziwa ya mbuzi na wengine anauza,” anaelezea.

Anasema, awali lita moja ya maziwa ya mbuzi ilikuwa Sh100 ila sasa imekwea mara dufu, hadi Sh200. Mbuzi aliyetunzwa vyema ana uwezo kutoa wastani wa lita 3 au 4 ya maziwa kwa siku.

Mamake amekula chumvi, na Ruth amechukua nafasi yake, kuendelea kunogesha ufugaji wa wanyama hao wa nyumbani.

Ni mifugo wenye manufaa chungu nzima, ila ni wachache mno wanaofuga wale wa maziwa nchini.

Kulingana na wafugaji waliofanikisha ufugaji wa mbuzi wa maziwa, wanasema hawahitaji nafasi kubwa.

Zizi la mbuzi wa Ruth lina kipimo cha mita 8, urefu na upana wa mita 6. Aidha, limegawanywa kwa makundi kadha, mbuzi wa kike hasa wanaonyonyesha, wa kiume, vibuli (wana wa mbuzi).

Mbuzi wa maziwa kwenye zizi. Picha/ Sammy Waweru

Vilevile, kuna sehemu ya walioshika ujauzito.

Huku wengi wakidhania na kuamini ufugaji wa mbuzi unafanikishwa maeneo ya mashambani pekee, Joseph Mathenge anakosoa fikra hiyo.

Ni mfugaji wa mbuzi kiungani mwa jiji la Nairobi. Katika kipande chake cha ardhi chenye ukubwa wa robo ekari, ameunda makazi ya mbuzi yenye kipimo cha futi 30 urefu , futi 8 upana na futi 13.7 kuenda juu.

Juu ya zizi lake, ametengeneza hifadhi ya chakula, na anasema zizi hilo lina uwezo kusitiri takriban mbuzi 20.

“Unapounda makazi ya mbuzi, sakafu iwe kuanzia mita tatu kutoka ardhini ili kuzuia viroboto na kupe kuingia,” Mathenge anashauri.

Mkulima huyo anasema angekuwa na mamia ya mbuzi wa maziwa tangu aingilie ufugaji huo 2011, ila upungufu na nafasi ndio kizingiti kikuu.

Chanjo na matibabu mbuzi wanapoonyesha dalili za udhaifu ni muhimu.

Usafi wa mazingira, kuanzia mazizi, chakula, maji na mbuzi wenyewe, unapaswa kuwa wa hali ya juu ili kudhibiti msambao wa vimelea na magonjwa.

Wataalamu wa mifugo wanahimizia haja ya kuwalisha chakula kamilifu kimadini na chenye virutubisho vya kutosha. Mbali na chakula cha maduka, mbuzi pia hulishwa nyasi aina ya Hay, Lucerne na Boma Rhodes.

“Wafugaji wawe makini na waangalifu katika suala la lishe, kuna chakula kingi sana cha madukani ambacho hakijaafikia ubora wa bidhaa,” anaonya Morris Kamau, mtaalamu wa mifugo.

Ufanisi katika ufugaji wa mbuzi wa maziwa pia unategemea chaguo, wafugaji wakihimizwa kuchagua mbuzi bora.

Ili kufanya ufugaji maeneo ya mijini, mkulima anahitaji kupata kibali kutoka kwa serikali ya kaunti na pia Halmashauri ya Mazingira.

Hata hivyo, kaunti zinazojulikana kwa shughuli za kilimo na ufugaji, hazina hatuna hizo.

You can share this post!

BI TAIFA JANUARI 8, 2021

Liverpool hawatasajili mchezaji yeyote muhula huu wa...