• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wanaokodi vyumba chini ya Airbnb wamulikwa kwa kuiba vyombo

Wanaokodi vyumba chini ya Airbnb wamulikwa kwa kuiba vyombo

NA RICHARD MAOSI

WAMILIKI wa nyumba na vyumba vya kukodisha wakati wa likizo chini ya Airbnb wamefichua kwamba wanakadiria hasara kubwa katika biashara zao kwa sababu baadhi ya wateja huiba vyombo na vitu vingine muhimu.

Msimu huu wa likizo, biashara zimenoga kwa sababu ya wateja wengi ambao wanaendelea kumimika Pwani, Naivasha, Machakos na Nakuru kujivinjari.

Bi Florence Nasimiyu ambaye ni mmiliki wa nyumba za kifahari za kukodisha katika mtaa wa kifahari wa Milimani katika Kaunti ya Nakuru, anasema ameanza kuwazia namna ya kuweka kamera za CCTV katika nyumba zake.

Hii itamsaidia kudhibiti wezi na pia kufuatilia mienendo ya wateja wao.

Bi Nasimiyu anasema anamiliki vyumba 13 vya kifahari takriban kilomita saba hivi kutoka jijini Nakuru na wateja wake wengi ni wanafunzi wa vyuo vikuu.

“Wanavunja mifereji au kuiba balbu na hata wakati mwingine wanachukua mapazia ya dirishani,” anasema Bi Nasimiyu.

Anasema aliamua kuwekeza katika biashara hiyo chini ya Airbnb baada ya kugundua wateja wengi wanaozuru Nakuru wanapendelea sehemu ambayo imetulia mbali na usumbufu wa mjini.

Isitoshe, familia nyingi hupenda kujipikia chakula na hata kufurahia uhuru sawa tu na wakiwa majumbani kwao.

Katika eneo la Naivasha, wamiliki wameelezea malalamishi sawa na hayo, baadhi ya wateja wakitoweka na vyombo vya kupikia kama vile vijiko na sufuria.

Wengi wanaoiba vyombo vya nyumba Naivasha, mmiliki mmoja amefichua, huwa ni warembo ambao huwa wamekuja kama kundi kutulia.

Kwa mfano wakati huu ambao wanafunzi wengi wa vyuo vikuu na taasisi, wamehitimu kozi mbalimbali.

Bi Ann Nduta ambaye ni mhudumu wa mojawapo ya Airbnb katika barabara ya South Lake Naivasha, anasema ni tabia ambayo imekuwa ikishuhudiwa kwa siku nyingi.

Mara nyingine yeye hukatwa mshahara ikizingatiwa kuwa baadhi ya wamiliki hudhani ni wahudumu ambao hushirikiana na wateja.

Mhudumu apeleka taulo kwa chumba. PICHA | MAKTABA

Anasema ni jambo ambalo limewafanya baadhi ya wamiliki wa nyumba zilizo chini ya Airbnb kuwaongezea wafanyakazi jukumu la kulinda mali lau sivyo wakatwe mishahara.

Huduma ya Airbnb ilianza kupata umaarufu baada ya biashara za mikahawa nchini kufifia.

Maeneo ambayo biashara ya Airbnb imenoga ni Malindi, Mombasa, na Kilifi ikizingatiwa kuwa wengi wanaotembelea maeneo husika wanapendelea vyumba hivi vya kukodisha kwa muda kwa sababu gharama yake ni nafuu.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaanza ‘kuvuna’ e-Citizen

Uhuru azuru bwawa ‘tata’ la Karimenu,...

T L