• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Barabara mbovu Githurai 44 kikwazo kwa wakazi kutembea

Barabara mbovu Githurai 44 kikwazo kwa wakazi kutembea

Na SAMMY WAWERU

MTAA wa Githurai 44 ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi ni maarufu kutokana na gharama ya chini ya maisha.

Kuanzia nyumba za kukodi za bei nafuu hadi bidhaa za kula, hususan zile mbichi kutoka shambani, huchochea wengi wenye mapato ya chini kuishi humo.

Kimsingi, kwa wakazi ni mtaa ambao wanaweza kuutaja “ni nafuu kusukuma gurudumu la maisha”, hasa kipindi hiki kigumu taifa na ulimwengu unateswa na athari za janga la Covid-19.

Huku ukitajwa kuwa miongoni mwa mitaa yenye idadi ya juu ya watu, kuwepo kwa barabara mbovu kunazidi kuwatatiza kutembea.

Mvua ikiendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini, shughuli za usafiri na uchukuzi katika vitongoji vya mtaa huo zinalemazwa na hali duni ya barabara.

Kwa mfano, barabara ya Rurii na Mulika Mwizi kipindi hiki cha mvua wakazi wanahangaika kutembea.

“Kwa asiye na viatu virefu vya plastiki ni kikwazo na kibarua kutoka anakoishi. Barabara katika mtaa huu wa Githurai 44 zinazidi kuwa mbovu,” Bw Robert Masinde, ambaye ni mkazi akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya kipekee eneo hilo.

Kwa wanaofanya kazi za ofisi na wanaotakiwa kurauka asubuhi na mapema ili kuwahi saa hulazimika kutumia bodaboda.

Ni gharama ambayo huwalazimu kufukua mfumo zaidi.

“Mvua inaponyesha wahudumu wa bodaboda hupandisha nauli. Isitoshe, bado nitachafuka tu kwa sababu mhudumu huwa kwenye haraka abebe wateja wengi,” akasema mwenyeji mwingine.

Wakazi tuliozungumza nao walisema kilio chao kwa viongozi waliochaguliwa eneo hilo wakitaka waimarishiwe barabara, kimeambulia patupu.

“Huwa tunawaona miaka ya uchaguzi pekee wakija kuturai tuwape kura. Katika uchaguzi wa mwaka ujao, 2022 tunataka viongozi ambao wanajali maslahi ya umma,” akasema Joseph Nduati na ambaye ni mpishi wa mahamri.

Kando na barabara za eneo hilo kuonekana kupuuzwa na serikali, mikondo ya majitaka imefuja na kuchangia hali kuwa mbaya zaidi.

Mtaa wa Githurai 44 uko katika eneobunge la Roysambu, ambapo mbunge wake ni Bw Waihenya Ndirangu.

Licha ya kuwa serikali ya Kaunti ya Nairobi inalaumiwa kwa kupuuza barabara za mtaa huo, ni aibu wakazi kuhangaika kutembea katika eneobunge ambalo hupata mgao wa Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF).

Aidha, mgao huo mbali na kutakiwa kuboresha miradi mingine ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule za umma, hospitali, unapaswa kutumika kuimarisha barabara.

  • Tags

You can share this post!

Haaland afunga magoli mawili chini ya dakika nne na...

Kura ya maamuzi kufanyika Julai, asema Junet