• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:17 PM
Haaland afunga magoli mawili chini ya dakika nne na kutambisha Dortmund dhidi ya Bremen ligini

Haaland afunga magoli mawili chini ya dakika nne na kutambisha Dortmund dhidi ya Bremen ligini

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Erling Braut Haaland alifunga mabao mawili chini ya kipindi cha dakika nne na kuwezesha waajiri wake Borussia Dortmund kutoka nyuma na kupepeta Werder Bremen 4-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Matokeo hayo yaliweka hai matumaini ya Dortmund kukamilisha kampeni za Bundesliga ndani ya orodha ya nne-bora msimu huu na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Dortmund waliobanduliwa na Manchester City kwenye robo-fainali za UEFA msimu huu, walijikuta chini baada ya dakika 14 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza mnamo Jumapili baada ya Milot Rashica kuwaweka Bremen uongozini.

Giovanni Reyna alisawazishia Dortmund katika dakika ya 29 kabla ya Haaland kupachika wavuni mkwaju wa penalti kunako dakika ya 34 na kucheka tena na nyavu za wageni wao dakika nne baadaye. Mats Hummels alifungia Dortmund goli la nne dakika tatu kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Mabao mawili yaliyofumwa kimiani na Haaland yalitamatisha ukame wa magoli katika msururu wa mechi saba. Fowadi huyo raia wa Norway anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Man-City mwishoni mwa msimu huu, sasa amefungia Dortmund magoli 23 kufikia sasa ligini.

Ushindi wa Dortmund uliwakweza hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Bundesliga kwa alama 49, nne pekee nyuma ya Eintracht Frankfurt wanaofunga orodha ya nne-bora. Zimesalia mechi tano pekee kabla ya kampeni za Bundesliga msimu huu kutamatika rasmi.

Ni vikosi vinne pekee vya kwanza jedwalini ndivyo vitakavyofuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao wa 2021-22. Kufikia sasa, mabingwa watetezi Bayern Munich wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 68 huku pengo la pointi saba likitamalaki kati yao na nambari mbili RB Leipzig. VfL Wolfsburg wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 54, moja zaidi kuliko Frankfurt.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Tottenham Hotspur wamfuta kazi kocha Jose Mourinho

Barabara mbovu Githurai 44 kikwazo kwa wakazi kutembea