• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
DIMBA MASHINANI: Kipa mahiri michumani kama mwanajeshi vitani

DIMBA MASHINANI: Kipa mahiri michumani kama mwanajeshi vitani

Na PATRICK KILAVUKA

KIJANA Benard Omungala Mumia, 22, ni kipa ambaye ametokea kuwa kizibo tosha kwenye lango la timu ya Lopez FC ambayo inashiriki Ligi ya Kaunti, tawi la Nairobi West. Udakaji na upanguaji wa mashuti ya wapinzani humpa fursa ya kudhibiti lango kama mwanajeshi tosha.

Kwa kujiamini katika kupiga shuguli ya ukipa, kocha Kennedy Osore, humchezesha katika kikosi cha kwanza kuzima makombora ya wakinzani.

Isitoshe, kujipanga kwake na kupanga safu yake ya ulinzi hurahisisha kazi mchumani kwani, huongelesha ngome ya udifenda wakati wa mchakato wa mchuano hali inayomwezesha kuihimili dhoruba ya mchezo na kusawazisha timu ikiwa uwanjani.

Kulingana kocha Osore, alizinasa huduma zake akicheza kama difenda. Lakini yeye kama kocha, alitathmini ubora wa uchezaji wake kama difenda na kuona amjaribu kama kipa wakati wa mechi moja ambayo kipa wao alikuwa ameghafulika.

“Kipa mtangulizi alikuwa ameghafulika kwa ugonjwa na timu ikakosa myakaji wa kujukumika wakati tulikuwa tucheze mechi uwanjani Gachie. Lakini kulingana na vile alivyokuwa anapiga zoezi, kama mkufunzi niliona ukubwa wa utajiri wa kipawa chake na nikaonelea nimtumie kama kizibo cha lango,” alieleza kocha huyo na kuongezea kuwa alionyesha uwezo kuwa mdakaji.

Kipa Mumia anazidi kuchongwa kupitia mkufunzi wa makipa Paul Odhiambo chini ya mwavuli wa Soka Westlands Keeper Academy.

Mchezaji huyu aliyesomea Shule ya Msingi ya Shikomera, Khwisero Kaunti ya Kakamega japo kwa sababu ambazo hangeziepuka hakuendelea ila, aliabiri jijini Nairobi na kwa miaka miwili, alikaa mjini Athi River.

Kipa wa Lopez FC ya Kangemi, Benard Omungala Mumia, 22. Picha/ Patrick Kilavuka

Hali hatihati ilimpelekea kuwa mtoto wa mtaani kwa mwaka mmoja jijini Nairobi akiuza plastiki kisha kuhamia Kangemi na kufanya kazi mbalimbali kuuza mandazi, kuendesha pikipiki kupitia kwa marafiki wake kabla kuajiriwa na akaanza kuona mwanga wa mabadiliko.

Ni akiwa Kangemi katika pilkapilka za kuchapa kazi mtaani humo, aliyazinduka kimawazo kuhusu mustakabali wa kuendelea kupiga ngozi baada ya kuona wachezaji wakijinoa uwanjani Kihumbuini. Hatimaye, aliazimia kuifufua, kuichochea na kuipalilia talanta yake ambayo ni karama tangu akiwa na miaka minane akiwa kiota cha timu ya Shikomera FC mashambani.

Kabla kujiunga na timu ya Lopez, alikuwa amechezea Resource FC kwa miaka miwili kisha kusajiliwa na Kikwetu FC kwa mwaka mmoja.

Omungala hufanya mazoezi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa uwanjani AHITI, Kabete.

Mkamataji boli ambaye humvutia sana ni Bernd Leno wa Arsenal kutoka na saizi yake, mbinu zake za ukipa anazojituma nazo akiwa kwenye shughuli uwanjani haswa upiga mbizi, unyakaji na jinsi anavyopanga safu yake ya ulinzi kuziba nyufa.

Angependa sana kuwa kipa katika vikosi vya Wolves na Burnley ughaibuini ambavyo anavisifu kutokana na nidhamu ya wachezaji.

Kipa Benard anasema boli siku hizi ni kazi. Hivyo basi, wanasoka wanafaa kuwa wa kujituma na kutia Mungu mbele kuinua talanta zao.

Anamshukuru kocha wa makipa Odhiambo kwa kumuongezea ufundi wa udakaji kwani mafunzo yake yamemwezesha kuimarisha mbinu zake za kunyaka boli.

Anashauri wachezaji wawe wasikivu na wazingatiaji wa mawaidha au nasaha wanazopewa kwani hayo ndiyo yatakayowajengea msingi mwema wa vipawa vyao kunawiri katika nyanja zote.

You can share this post!

Joe Willock awabeba Newcastle dhidi ya Sheffield United...

Everton wakung’uta Wolves katika EPL na kujiweka...