• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
FUNGUKA: ‘Mapenzi mtandaoni…raha!

FUNGUKA: ‘Mapenzi mtandaoni…raha!

Na PAULINE ONGAJI

UHUSIANO wa mapenzi na hata hatimaye ndoa mara nyingi huwa thabiti ikiwa wahusika wanaishi pamoja.

Ndiposa wapenzi au wanandoa wengi walio katika uhusiano wa mbali watakuambia kwamba changamoto kuu huwa kudumisha penzi.

Lakini kwa Kenneth na Lenah, mambo ni tofauti sana. Wawili hawa ambao wameoana kwa miaka mitatu sasa, na kujuana kwa zaidi ya miaka mitano, hawajawahi kutana ana kwa ana.

Kenneth mwenye umri wa miaka 51 ni raia wa Amerika na hajawahi kanyagisha guu hapa nchini. Yeye ni afisa mkuu mtendaji wa shirika moja kubwa nchini Amerika. Kimasomo amesoma kwelikweli na hata kwa sasa anamalizia shahada yake ya uzamifu.

Kutokana na kazi yake, bwana huyu hana tatizo la kifedha kwani anamiliki mali katika miji kadhaa nchini humo, na hivyo si kosa kumuita tajiri. Hajawahi oa wala kuwa na watoto.

Kimaumbile pia kabarikiwa. Kaka huyu wa asili ya kizungu ana sifa za kuvutia. Kimo chake kirefu kimepigwa jeki na mabega yake thabiti, huku macho yake ya kijani yakimulika uso wake uliosimama wima kwenye mashavu yake yaliyochongwa vikamilifu.

Kwa upande mwingine, Lenah pia ni binti aliyeneemeka kimaumbile. Kipusa huyu wa miaka 45 kaumbwa kaumbika na ni kivutio cha madume wengi wanaopata fursa ya kukutana naye.

Kielimu na kitaaluma, pia hajaachwa nyuma ambapo anafanya kazi kama mkurugenzi wa shirika moja lisilo la kiserikali hapa nchini. Pia yeye hajawahi olewa wala kupata mtoto.

Licha ya kuandamwa na madume kadhaa wa humu nchini, binti anasema kwamba penzi lake kwa huyu kaka wa kizungu ambaye hawajawahi kutana, ni la kipekee.

“Tulijuana, kuchumbiana na hata kuoana mtandaoni. Tulijuana miaka mitano iliyopita kupitia mtandao wa kusaka wapenzi. Tulipendana sana na sababu kuu iliyotukutanisha ni kwamba sote tulikuwa na nia moja, kupendana mtandaoni na kutowahi kutana ana kwa ana.

Tulichumbiana kwa zaidi ya mwaka mmoja, kisha tukatambulishana kwa jamaa zetu, kuandaa harusi na kuoana mtandaoni. Hata mahari, alilipa kwa kuwatumia wazazi wangu pesa.

Tunapendana sana na kila siku uhusiano wetu unazidi kuimarika na hatuna nia ya kukutana wala kuishi pamoja.

Ili kusawazisha hamu ya kuwa na mgusano, sisi huwasiliana mtandaoni kila wakati. Kila siku, mawasiliano yetu ya video katika Facebook, WhatsApp au hata Skypme yanadumishwa, tuwe nyumbani, kazini au hata barabarani.

Pengine unajiuliza je, ashiki twazima vipi? Mahaba pia twalishana na kuridhishana mtandaoni.

Tunahisi kwamba pindi tutakapokutana huenda ulimwengu wa mapenzi tuliojiundia ukapakwa doa na kutusababisha kuachana.

Hii ni mbinu ambayo kila mmoja anapaswa kukumbatia. Nani alisema kwamba mapenzi sharti yahusishe watu kukutana ana kwa ana?

Kuna watu wengi ambao wamo katika mahusiano ya aina hiyo na wameishia kuuana. Sisi hatutaki hayo. Tunaamini kwamba, katika uhusano wa aina hii, uwezekano wa kuchoshana ni mfinyu sana”.

You can share this post!

Pasta atozwa Sh2,000 baada ya kufumaniwa na muumini

TAHARIRI: Ongezeko la ajali linatia wasiwasi