• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
FUNGUKA: ‘Sauti nyororo huniyeyusha mzima’

FUNGUKA: ‘Sauti nyororo huniyeyusha mzima’

Na PAULINE ONGAJI

MABINTI wengi watakuambia kwamba mojawapo ya sifa zinazowavutia kwa wanaume ni sauti nzito, ambayo mara nyingi huashiria ukomavu.

Lakini sio kwake Karen. Kinyume na matarajio ya wengi, binti huyu huvutiwa sana na akina kaka wenye sauti nyororo au ukipenda soprano.

Karen mwenye umri wa miaka 34, ni meneja wa kampuni moja kubwa jijini Nairobi na kama inavyotarajiwa ana mshahara mkubwa ajabu.

Fedha hizi nyingi zimemwezesha kujizatiti na kuwekeza hapa na pale kwani anamiliki jumba kubwa katika mojawapo ya mitaa ya kifahari jijini Nairobi. Aidha, ana nyumba kadhaa za kupangisha katika mitaa mbalimbali jijini.

Mbali na hayo, kipusa huyu huvuka kitaani na magari ya nguvu ambapo inasemekana kila moja ilimgarimu zaidi ya Sh3 milioni.

Lakini pia Karen ni mrembo. Umbo lake la kupendeza huwaduwaza wengi – waume kwa wanawake – kila anapopita. Aidha, ngozi yake ya kupendeza, vilevile sifa mwafaka usoni zimemfanya kuwa kivutio cha yeyote anayekutana naye.

Karen pia anajua kuushughulikia mwili wake kwa kuzingatia lishe bora, kutumia bidhaa za mapambo za ubora wa hali ya juu na kufanya mazoezi kila wakati.

Kutokana na hili, kiumri anaonekana mchanga na wengi hudhani kwamba hajahitimu miaka 30.

Lakini kama wasemavyo kwamba hakuna aliye mkamilifu, Karen ana udhaifu mmoja. Bibiye ana sauti nzito na inayokwaruza ajabu, ambapo ukimsikia akizungumza kwa mbali utadhani kwamba ni dume.

Ni suala ambalo limemfanya kuwa na ladha ya kipekee inapowadia wakati wa kusaka wapenzi. Katika masuala ya mahaba, kivutio chake ni cha kushangaza kwani hana haja na wanaume wenye sauti nzito kamwe. Badala yake anaduwazwa na madume walio na sauti nyororo, na haoni haya kuthibitisha hilo.

“Nawapenda sana madume wenye sauti nyororo kwani naamini sio madume wa kawaida. Kwangu jambo la kawaida hunichosha.

Mbali na hayo, katika utafiti wangu nimegundua kwamba madume wa aina hii ndio weledi hasa katika masuala ya mahaba.

Tofauti na wenzao wenye sauti nzito wanaojigamba kila wakati, hawa hawazungumzii sana ustadi wao katika mambo haya na kwangu hiyo ni ishara tosha wamekolea. Mbali na hayo, nasadiki sauti zao nyororo zinaashiria ubichi.

Isitoshe, sipati ushindani mkubwa kwani madume wenye sauti nyororo sio kivutio cha mabinti wengi. Kwangu hii ni fursa mwafaka kufurahia uhondo bila wasiwasi kwamba nitamfumania na wengine.

Pia tangu utotoni, sijawahi kuwa mtu wa kufuata upepo. Sifurahishwi na jambo au suala linalovutia watu wengi.

Kadhalika, wengi wao ni wanyenyekevu na hawawezi nipiku katika kutawala mada yoyote ile. Sipendi kutawaliwa na wanaume.

Isitoshe, sauti nzito ni kero kwa amani yangu hasa ikizingatiwa kwamba mimi pia nina sauti inayokwaruza”.

You can share this post!

Kilio beste akiponyoka na bebi wake

CHOCHEO: Kumchongoa sawa na kuchongea penzi lenu