• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
GWIJI WA WIKI: Kennedy Opindi

GWIJI WA WIKI: Kennedy Opindi

Na CHRIS ADUNGO

KAZI bora ya uandishi ni zao la bidii, stahamala na utafiti wa kina.

Hakuna mafanikio utakayoyapata bila ya kujituma!

Maamuzi yoyote unayoyafanya ni zao la agano kati ya nafsi na mawazo yako. Jikubali na ukatae maisha ya kujihukumu!

Nidhamu na imani huchangia pakubwa mafanikio ya mtu. Huwezi kabisa kujiendeleza maishani iwapo hujiamini. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta!

Usitamauke kabisa hata unapokosa kufaulu. Mtangulize Mungu, endelea kukazana na hatimaye milango ya heri itajifungua yenyewe!

Huu ndio ushauri wa Bw Kennedy Opindi Ongadi – mwandishi mbobevu, mlezi wa vipaji, mwanasoka stadi na kocha wa tenisi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lugulu Girls, Kaunti ya Bungoma.

MAISHA YA AWALI

Opindi alizaliwa mnamo 1975 katika kijiji cha Museno, eneo la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Museno alikosomea kati ya 1983 na 1990.

Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na kupata fursa ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Ignatius Mukumu, Kakamega. Alisomea huko hadi kidato cha pili kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Kegonga, Kaunti ya Migori alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mnamo 1996.

Opindi alisomea ualimu (Kiswahili na Jiografia) katika Chuo Kikuu cha Maseno kati ya 1998 na 2002. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi kwa ajili ya shahada ya uzamili kuanzia 2011.

Alifuzu mnamo 2014 baada ya kuwasilisha tasnifu “Upole na Utambulisho katika Lugha ya Unyumba” chini ya usimamizi na uelekezi wa Prof Nathan Oyori Ogechi na Dkt Mark Mosol Kandagor.

Anatambua ukubwa wa mchango wa walimu wake wa awali katika kumhimiza kukichapukia Kiswahili na kumpokeza malezi bora ya kiakademia.

Miongoni mwa walimu hao ni Bw Gisiri aliyemfundisha katika Shule ya Upili ya Kegonga na Prof Florence Indede aliyetangamana naye kwa karibu sana katika Chuo Kikuu cha Maseno.

UALIMU

Baada ya kuhitimu ualimu, Opindi alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya St Charles Lwanga Mukumu kisha Shule ya Upili ya Atela, Kaunti ya Homa Bay.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2005 na ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Maranda, Kaunti ya Siaya. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka saba kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Lugulu Girls mnamo 2013.

Akiwa Maranda, aliwaongoza walimu wenzake kuweka historia ya matokeo bora zaidi baada ya watahiniwa wa KCSE 2010 shuleni humo kujizolea alama wastani ya 11.341 katika somo la Kiswahili.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Opindi tangu utotoni. Akiwa Maranda, alianza kuchangia ‘Maoni’ katika gazeti hili la Taifa Leo na kuandaa ‘Miongozo’ ya vitabu teule vya fasihi vilivyotahiniwa katika KCSE Kiswahili.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano mbalimbali na akapata fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili. Dkt Robert Oduori na Bw Timothy Omusikoyo Sumba ni miongoni mwa mikota wa lugha waliompigia Opindi mhuri wa kuwa mwandishi bora wa kazi bunilizi za Kiswahili.

Uandishi wake umeathiriwa pakubwa na kazi za marehemu Profesa Ken Walibora, mlezi na rafiki aliyemshajiisha mara kwa mara kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu.

Kufikia sasa, Opindi anajivunia kuchapishiwa mashairi na hadithi fupi ambazo zimejumuishwa katika diwani mbalimbali kama vile ‘Jela ya Wendawazimu na Hadithi Nyingine’, ‘Mkaguzi wa Shule na Hadithi Nyingine’, ‘Gilasi Iliyovunjika na Hadithi Nyingine’, ‘Mateka na Hadithi Nyingine’, ‘Wosia na Mashairi Mengine’ na ‘Malenga wa Afrika’.

Kazi zake nyinginezo ni ‘Mwangwi wa Sarufi’, ‘Insha Timilifu’, ‘Fuzu Kiswahili (Lugha)’ na ‘Fuzu Kiswahili (Fasihi)’. Amewahi pia kutafsiri makala mbalimbali ya kitaaluma kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

URAIBU

Opindi ni mpenzi kindakindaki wa mchezo wa kandanda na ndiye fowadi tegemeo katika timu yao ya walimu ya Lugulu Girls. Yeye pia ni kocha wa tenisi katika shule yao na timu yake imewahi kutia fora hadi ikafika kiwango cha kitaifa.

JIVUNIO

Ndoto ya Opindi ni kufikia upeo wa taaluma yake, kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili. Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Kadhalika, yeye ni mlezi wa Chama cha Kiswahili cha Lugulu Girls ambacho humpa jukwaa la ziada la kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha, kutoa ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuwahimiza walimu wenzake kuchochea kasi ya kutekelezwa kwa malengo mahsusi katika nyanja za uandishi, utafiti na ufundishaji wa Kiswahili.

Opindi anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea taaluma yake mshabaha na thamani kubwa. Mkewe mpendwa ni Dkt Lilian Ayiro ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha MMUST na Chuo Kikuu cha Kibabii. Ndoa yao imejaliwa watoto watatu – Danoel Baraka, Kevin Ogalo na Elliana Pesi.

You can share this post!

SAUTI YA MKEREKETWA: Wanetu wafanye kozi za teknolojia ili...

Jubilee yacheza ngware chaguzi ndogo