• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
KAMAU: Amerika sasa haina shavu kuzungumzia demokrasia

KAMAU: Amerika sasa haina shavu kuzungumzia demokrasia

Na WANDERI KAMAU

SIMULIZI za jadi kuhusu maana halisi ya demokrasia zimekuwa zikiifananisha Afrika na uwanja wa fujo, mapinduzi ya kijeshi na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Ni simulizi ambazo zimekumbatiwa na wasomi wa masuala ya demokrasia, mifumo ya utawala, historia na siasa.

Dhana hizo hata zimeingizwa kwenye vitabu vya historia, kwamba Afrika kamwe haiwezi kujisimamia kiutawala bila ‘usaidizi’ kutoka kwa nchi ‘zilizostawi’ kidemokrasia kama Amerika na mataifa ya bara Ulaya.

Taswira hiyo imeipaka tope Afrika kila wakati mdahalo kuhusu demokrasia unapoibuka kokote duniani—iwe ni katika makongamano au majukwaa ya kiusomi.

Hata hivyo, uhalisia kamili kuhusu unafiki wa Amerika na nchi zingine kuhusu demokrasia umedhihirika wazi tangu 2016, alipochukua uongozi Rais Donald Trump.

Kwa miaka minne ambayo Trump amehudumu kama kiongozi wa taifa hilo, dhana ya Amerika kama taifa komavu kidemokrasia imefutika kabisa.

Vitendo vya Trump vilidhihirisha wazi kuwa Wazungu wamekuwa wakitumia majukwaa yao kuendeleza uwongo kuhusu hali ya demokrasia Afrika na nchi zingine zenye chumi za kadri.

Kwanza, Trump alikataa kutambua ushindi wa Rais Mteule Joe Biden kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 3 mwaka uliopita.

Trump alidai kuwepo kwa udanganyifu kwenye uchaguzi huo, hali iliyomfanya kuanza kutoa kila aina ya malalamishi kuhusu vile “matokeo yalibadilishwa.”

Kile Trump alisahau ni kuwa alidaiwa kusaidiwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi kumshinda mpinzani wake mkuu, Bi Hillary Clinton, kwenye uchaguzi wa 2016.

Ripoti za kijasusi zilidai Trump alisaidiwa na idara ya ujasusi ya Urusi kumwibia kura Clinton, ndipo akaibuka mshindi katika hali tatanishi. Sarakasi za Trump zilifikia upeo wake Jumatano, wakati wafuasi wake walivamia Jengo la Seneti na kuvuruga vikao ambavyo vilikuwa vikiendelea.

Uvamizi huo ulijiri saa chache tu baada ya chama cha Republican, chake Trump, kushindwa vibaya na chama cha Democratic (chake Biden) kwenye marudio ya uchaguzi wa Useneta katika jimbo la Georgia.

Kimsingi, ni nadra sana kwa matukio kama hayo kushuhudiwa katika taifa ambalo ni mojawapo ya yale yamekuwa yakitumiwa kama mfano kuhusu maana ya demokrasia komavu na kamilifu duniani. Tukio la Jumatano linadhihirisha kuwa licha ya kupata uhuru wake mnamo 1776 (miaka 244 iliyopita!), Amerika bado ina changamoto za kimsingi kama mataifa mengine duniani.

Hatari kubwa kuhusu changamoto hizo ni kuwa zimefichika kwa zaidi ya karne moja.

Miongoni mwa matatizo hayo ni ubaguzi wa rangi na chuki kubwa kati ya watu kutoka jamii mbalimbali wanaoishi humo. Chini ya mazingira kama hayo, maswali yanaibuka kuhusu ikiwa Amerika ina haki yoyote kuzikaripia nchi za Afrika kuhusu “ukamilifu wa kidemokrasia.”

Hii ni nafasi yake pia kujifunza kwa nchi za Afrika ambazo zimeandaa na kumaliza chaguzi zake bila matatizo yoyote. Ni nafasi mwafaka kwake kufahamu kuwa badala ya kuzifokea ama “kuzisaidia” nchi zingine, inafaa kulainisha mfumo wake wa utawala kwanza.

[email protected]

You can share this post!

KIKOLEZO: Maji yazidi unga!

Ugavana wa Nairobi wazidi kukanganya