• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
KIKOLEZO: Maji yazidi unga!

KIKOLEZO: Maji yazidi unga!

Na THOMAS MATIKO

BAADA ya miaka sita pamoja, ndoa ya rapa Kanye West na soshiolaiti Kim Kardashian, imekunywa maji.

Tetesi zinadai kuwa mastaa hao walishaamua zamani kutalikiana ila wamekuwa wakijitahidi kufanya mambo hayo chini ya maji.

Vyanzo mbalimbali vinadai kwamba ingawaje wangali wanaishi pamoja na watoto wao wanne, hawalali kwenye chumba kimoja. Imekuwa hivi kwa mwaka mzima sasa huku wakiendelea kusaka ushauri wa kugawana mali.

Kim anasemekana kuchoshwa na mabadiliko ya kimienendo ya mumewe huyo ambaye anahisi hayupo sawa kiakili kwa sasa. Wameshajaribu kukaa vikao kibao vya kifamilia kujaribu kutatua na kurejesha mambo kwenye mstari ila imeshindikana.

Matukio kibao yanadaiwa kuchangia hali hii. Hatua ya Kanye kugombea urais haikumfurahisha Kim. Pia utakumbuka lile tukio la Kanye kuchizi kiasi cha kumpelekea alazwe hospitalini. Kanye anadaiwa kuwa na ugonjwa wa kiakili maarufu ‘bipolar’. Yaani mtu asiyetabirika, mwenye hisia pinganifu. Pia kauli yake kuwa yeye na Kim waliwazia kuavya ujauzito wa mtoto wao wa kwanza North West ilimkera sana Kim.

Stori ya Kim na Kanye hadi inafikia ilikofikia, inacheza kama drama, movie au telenovela.

2004: Mara ya kwanza kukutana

Kim na Kanye walikutana kwa mara ya kwanza kwenye shuti ya video ya wimbo wake nyota mwanamuziki Brandy. Kanye alikuwa akiandaa kolabo na staa huyo mwenzake, huku Kim akiwa mpodozi na mrembaji wa Brandy. Kipindi hicho, Kim alikuwa kwenye ndoa na Damon Thomas aliyeoana naye 2000 naye Kanye alikuwa katika mahusiano na mwanamitindo Alexis Phifer. Mkutano huo ukazalisha urafiki wa kishikaji baina yao.

2006: Kanye amkufia Kim

Walipokutana mara ya kwanza, Kanye alibaki kumuulizia sana Kim kwa watu waliokuwa karibu naye akiwemo Brandy. Miaka ilivyozidi kusonga, Kim akaanza kuvutiwa na msupa huyu. Hii ilichangiwa zaidi na ushikaji wa karibu ambao pia ulikuwepo kati ya Kim na Paris Hilton. Paris alikuwa tayari ni staa na mara kwa mara kwenye mitoko yake alionekana akiandamana na Kim aliyekuwa pia mrembaji wake.

Licha ya Kim kuendelea kuwa ‘crush’ wake, Kanye aliendelea na maisha yake ya mahusiano na Alexis akimchumbia Agosti 2006. Mwaka uliofuatia mambo yakaharibika pale Kanye alipompoteza mamake Donda West. Donda alifariki kufuatia upasuaji kadhaa alioufanya kupunguza uzito na mafuta mwilini na pia kupunguza matiti yake. Kifo cha Donda kilimvuruga Kanye asiye na ndugu wengine wala wanafamilia.

2008: Kanye amtema Alexis

Baada ya uchumba wa mwaka na nusu, Kanye alimpiga kibuti Alexis jambo ambalo lilimuumiza sana mrembo huyo aliyekuwa na matumaini makubwa ya kuolewa na nyota huyo.

Kilichofuatia ni Kanye kuanza kumfuatilia Kim kisnaipa. Alimwalika kwenye shoo yake moja ya Hip hop ya Star Wars ili amsaidie kwenye maandalizi na ufanikishaji wake. Kipindi hiki Kim alikuwa kwenye mahusiano na Reggie Bush. Alikuwa tayari ameshatalikiana na Damon. Naye Kanye kwa upande ule mwingine alikuwa akitesa na Amber Rose.

2009: Kanye amwonea wivu Reggie

Februari mwaka huo, kuliandaliwa shoo ya fasheni mjini New York, Y-3 Show. Kim alihudhuria akiandamana na mpenzi wake Reggie aliyekuwa nyota wa American Football. Kanye naye akasaka kiti kwenye mstari waliokuwa wameketi Kim na ‘bae’ wake. Ila Kanye alijipa ‘social distancing’, kwa kuketi kando yake mwigizaji Milla Jovovich aliyekuwa ameketi sako kwa bako na Kim huku upande wa kulia akiwa ni Reggie. Ni kitu ambacho kilimtesa sana Kanye siku hiyo ambayo alihudhuria tukio akiwa solo. Amber hakuwepo.

Tukio hilo Kanye aliishia kurap kwenye kolabo yake Knock You Down na Keri Hilson ambako alikiri kumwonea wivu Reggie walipokutana huko.

2010: Kanye amalizana na Amber

Taarifa kuwa Kanye alikuwa anatoka na soshiolaiti staa Amber Rose zilivuma sana kwa sababu tayari pia demu huyo alikuwa ni maarufu.

Hata hivyo muda wote mawazo ya Kanye yalikuwa kwa Kim wa wenyewe ambaye nyota yake ilikuwa ikiendelea kujifua.

Baada ya mahusiano ya miaka mitatu waliamua kuachana. Walikuwa tayari wameshatengana kwa muda Agosti 2009 kabla ya kurudiana ila Julai 2010 wakaamua kila mtu akafanye yake. Amber tayari alikuwa ashajua Kim alikuwa akimvurugia mawazo Kanye wake kwani mara tu baada yao kutemana alimkemea. Amber alisema sababu kubwa ya yeye kuachana na Kanye ilikuwa Kim. “Kim ndiye kanivunjia nyumba,” alinukuliwa kwenye mahojiano.

2011: Kim achukua mwanamume mwingine

Reggie naye alikuja na kupita kama upepo. Akaja staa mwingine safari hii nyota wa basketiboli Kris Humphries aliyemchumbia Mei 2011. Walikuwa tayari wameshadumu kwenye mahusiano kwa takriban mwaka mmoja tangu Oktoba 2010. Oktoba 2011, Kim na Humphries wakafunga ndoa bab’kubwa iliyohudhuriwa na watu 450 na kugharimu dola 10 milioni.

Baada ya siku 72, ndoa hiyo ikavunjika na Kim akaomba talaka. Ni ndoa iliyozua utata ikidaiwa kwamba waliifanya kwa ajili ya shoo na kutemana ilikuwa kiki ili kuivumisha. Tayari walikuwa ni mastaa walipoanzisha mahusiano na stesheni nyingi zililipia kupeperusha harusi hiyo. Hata hivyo Kim kasisitiza kwamba ndoa hiyo haikuwa kiki. Baada ya kuachana kwao, Kanye alifichua kwamba alijaribu kumshawishi Kim asiolewe na Humphries. Mara tu baada ya kutemana, Kanye na Kim wakaripotiwa kupeleka ushikaji wao katika levo nyingine.

2012: Kanye amtunga mimba Kim

Baada ya miaka minane akikimbizana na Kim toka alipomwona kwa mara ya kwanza, hatimaye Kanye alifanikiwa kumpata msupa huyo kama demu wake.

Waliweka hadharani mahusiano yao Machi 2012 walipotokea kwenye Paris Fashion Week na kuketi sako kwa bako. Matukio zaidi yaliyothibitisha wanadeti yakafuata ikiwemo kushikana mikono hadharani mitaani. Disemba 2012, Kanye akafichua kwamba anatarajia mtoto wake wa kwanza na Kim.

2013: North West azaliwa, ndoa njiani

Juni 2013, Kim akajifungua mtoto wao wa kwanza binti North West. Miezi minne baadaye Kanye akamposa Kim kwa pete ya almasi yenye ubora wa ‘15-carat’. Taarifa hizi zikapasua tasnia ya burudani. Lakini kunogesha mambo, Kim alitokea uchi wa mnyama kwenye video ya Kanye, Novemba mwaka huo.

2014: Harusi tunayo

Mei 2014, Kim na Kanye wakafanya harusi ya kifahari mjini Italia iliyohudhuriwa na watu 200 wao wa karibu. Miaka iliyofuatia ikawa ni ya kuzaa watoto. 2015, akazaliwa Saint West kisha 2018 akaja Chicago West ambaye ujauzito wake ulibebwa na mwanamke tofauti. Baada ya kupata watoto wawili, Kim hakuwa tayari kushika ujauzito wa tatu kutokana na hali yake ya kiafya kuathiriwa na mimba yao.

2019, wakapata tena mtoto wa kiume Psalm West ambaye vile vile ujauzito wake ulibebwa na mwanamke mwingine kwa njia ya upandikizaji (IVF).

2019: Kanye aanzisha Kanisa lake

Baada ya mtoto wanne, Kim na Kanye walizindua upya ndoa yao. Lakini pia ndio kipindi Kanye alianzisha kanisa lake. Kila Jumapili nyumbani kwake, aliongoza kwaya huku kukiwepo na pasta wa kutoa mahubiri. Wakati huu tayari Kanye alikuwa amewaacha wengi hoi kutokana na twiti zake nyingi za utata. Pia ndicho kipindi alimkashifu swahiba wake Jay Z kwa kumtenga. Nyingi za kauli zake zilikuwa tata na ndicho kipindi alianza kutafutiwa msaada wa wataalamu. Kuanzisha kanisa nyumbani kwake, Kim alikuwa mwingi wa matumaini kwamba kungemsaidia kutuliza mawazo yake lakini wapi.

2020: Maji yazidi unga

Katika miaka michache iliyopita Kim amejitahidi sana kumwelewa na kumvumilia mume wake ambaye kila kukicha hali yake ya kiakili na kimawazo imeonekana kuendelea kuwa mbaya.

Ila kilichomvunja ngamia mgongo ni tukio la Julai 2020 Kanye alipotangaza kuwa atagombea urais wa Marekani. Kim alimsapoti awali. Hata hivyo alibadili msimamo baada ya Kanye kwenye kampeni yake ya kwanza South Carolina kufichua kwamba yeye pamoja na mke wake waliwazia kutoa mimba ya mwanao wa kwanza. Kim alijitahidi kumsakia wataalamu wa afya na baadaye kuachia taarifa ikisema kuwa mume wake ana ugonjwa wa bipolar (Mtu mwenye hisia pinganifu). Hali hii ndio imechangia Kim kuitisha talaka baada ya kujaribu kila mbinu kuokoa hali bila ya mafanikio.

You can share this post!

WASONGA: Ni wazi, Ruto ndiye aliye na nafasi kubwa kumrithi...

KAMAU: Amerika sasa haina shavu kuzungumzia demokrasia