• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:13 AM
Kampuni yawafaa wakulima wa pilipili kwa kuunda bidhaa tofauti

Kampuni yawafaa wakulima wa pilipili kwa kuunda bidhaa tofauti

Na PETER CHANGTOEK

WAKULIMA wengi wanaozalisha pilipili nchini, wamekuwa wakipitia changamoto kadhaa, zikiwemo ukosefu wa soko la kuuzia zao hilo.

Hata hivyo, uongezaji thamani kwa zao hilo huwasaidia mno wakulima kupata soko la zao lenyewe. Kuna kampuni kadhaa zinazoongeza thamani kwa pilipili. Miongoni mwa kampuni hizo ni Voi Farm Limited, iliyoko katika eneo la Mwakingali, Voi, Kaunti ya Taita Taveta.

Kwa wakati huu, hushughulika na uongezaji thamani kwa pilipili aina ya African bird’s eye (ABE chilli), na imewapa wakulima 100 kandarasi ya kuikuza aina hiyo ya pilipili, ili wawe wakiuzia kampuni iyo hiyo.“Kampuni hii iliasisiwa mwaka 2020.

Hii ni kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, ambao ulilazimisha kuwe na haja ya kubuni mbinu mpya za biashara kwa wakati mgumu,” asema Mwanaidi Mohammed, ambaye ni Meneja wa Uzalishaji katika kampuni hiyo.

Kampuni hiyo, iliyoasisiwa na Faustin Mgendi, ambaye pia ni mkurugenzi, imewasajili wakulima wanaozalisha pilipili katika maeneo ya Kishushe, Mbololo, Sisera, Taveta, Kasigau, Mbale, Ngolia, miongoni mwa mengine.

“Sisi hununua pilipili kilo 1,500 kwa wastani kutoka kwa wakulima hao,” asema mkurugenzi huyo wa uzalishaji.Mwanaidi anafichua kuwa wao waliamua kujitosa katika uongezaji thamani kwa pilipili aina ya ABE kwa sababu ina manufaa mengi kiafya na huhitajika mno na wengi.

Kuongezwa thamani kwa pilipili huwa na manufaa. Kwanza, huimarisha bei ya zao hilo ikilinganishwa na kuuzwa kwa zao lenyewe pasi na kuongezewa thamani. Pili, bidhaa zilizoongezwa thamani zinaweza kukaa kwa muda mrefu pasi na kuharibika.

“Huongeza thamani kwa pilipili aina ya ABE kwa kutengeneza ABE Red Chilli Flakes, ABE Chilli Powder, na huongeza thamani pia kwa maembe yaliyokaushwa kwa kutengeneza achari,” afichua Mwanaidi.

Kampuni hiyo hununua pilipili aina ya ABE kutoka kwa wakulima kwa Sh70 kwa kilo. Wao huziuza bidhaa za ABE Red Chilli Flakes kwa bei ya jumla ya Sh130 na pilipili masala kwa bei ya jumla ya Sh150 na bidhaa aina ya Achari kwa Sh100.

Bidhaa zao zimepakiwa zikiwa na uzani tofauti tofauti.Anasema kuwa, wao hupata wateja kwa kuitumia mitandao ya kijamii. Aidha, wateja wao wengine ni wale wanaoelekezwa na wale waliowahi kuzinunua bidhaa za kampuni hiyo na kuridhishwa nazo.

Isitoshe, kuna hoteli kadhaa katika Kaunti ya Taita Taveta, ambazo huzinunua bidhaa zizo hizo.Kampuni hiyo ina mashine maalum za kukausha pilipili pamoja na za kusaga. Mbali na kuongeza thamani kwa pilipili, wao pia huuza zile zilizokaushwa.

Uchakataji wa maembe yanayokaushwa na kutumika kutengeneza achari, hufanyika katika Kaunti ya Kilifi, ambako kuna mashamba yanayokuza miembe.Voi Farm Limited ina wafanyakazi wanne wanaosaidia kuhakikisha kuwa shughuli za uongezaji thamani zinaendelea vyema.

Hata hivyo, kuna changamoto za hapa na pale, ambazo kampuni hiyo imewahi kuzipitia, kama vile ukosefu wa hela za kutosha kuendeleza biashara, kutokuwa na soko kubwa la kuuzia bidhaa na kiangazi ambacho huwakabili wakulima wanaouzia pilipili kampuni hiyo.

Mwanaidi anadokeza kuwa, wakulima waliosajiliwa na Voi Farm Limited, hunufaika kwa njia nyingi, mbali na kuziuza pilipili zao kwayo. Wao hupata mbegu za pilipili aina ya ABE bila malipo, mafunzo kuhusu jinsi ya kuzikuza, ushauri wa jinsi ya kuendesha kilimo pamoja na soko lililo tayari, miongoni mwa manufaa mengineyo.

Anaongeza kuwa bidhaa zao zimeidhinishwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (KEBS). Pia anaongeza kuwa kwa mwezi wao huuza kilo 500 za pilipili zilizokaushwa.Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika uzalishaji wa pilipili kuwa, uvumilivu ni muhimu kwa kilimo hicho.

“Kwa ukuzaji wa mipilipili, jambo muhimu zaidi ni kuwa na maji kwa wingi,” aongeza.“Voi Farm Limited inapania kuwa kampuni ya kuuza bidhaa nje ya nchi na kuuza bidhaa kote nchini,” asema Mwanaidi, akiongeza kuwa, wana mipango ya kuongeza mazao wanayoongezea thamani.

You can share this post!

Agizo watumishi wakumbatie mavazi ya Kiafrika

TAHARIRI: Raia wahimizwe kujisajili kwa kura

T L