• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
KIKOLEZO: Bazenga P Diddy

KIKOLEZO: Bazenga P Diddy

NA SINDA MATIKO

HIVI wewe ulizaliwa kuwa nini? Leo ukitangulia mbele za haki tutakukumbuka kwa nini?

Kuna watu walizaliwa kuwa msaada. Watu kama Sean ‘Diddy’ Combs. Mtu aliyezaliwa sio tu kuwa maarufu, lakini pia kuwa mjasiriamali wa kuogopewa.

Tunamzungumzia tajiri bilionea kwenye sarafu za Kimarekani.

Akiwa na miaka 52 sasa, Diddy alianza safari yake ya kuwa sio tu mjasiriamali bilionea ila msanii mkali akiwa na miaka 20 pekee.

Leo kama akifa, hatakumbukwa tu kwa rekodi alizoachia, au kwa wasanii aliowajenga na kuwageuza kuwa mastaa kama yeye tu, atakumbukwa pia kwa kuwa mtu aliyetoa mchango mkubwa kwa jamii kupitia sanaa na katika ulimwengu wa fulusi.

TUZO YA LIFETIME ACHIEVEMENT

Ndio maana mwezi Juni kwenye shamrashamra za tuzo za BET 2022, aliheshimishwa kwa kuzawadiwa tuzo ya BET LifeTime Achievement.

“Diddy siku zote amekuwa mwanzilishi wa jambo kwenye jamii yetu. Amekuwa akijitahidi kufikia levo ambazo watu weusi wanadhaniwa hawezi kuzifikia. Hili limedhibitika sio tu kwenye muziki, ila pia kwenye vyombo vya habari, utamaduni wetu, biashara na huduma kwa jamii. Ni mfano mzuri wa ubora wa mtu mweusi,” alimsifia Afisa Mkuu Mtendaji wa BET, Scott Mills.

Diddy anakuwa staa wa 21 kuheshimishwa kwa tuzo hii ya kutambua mchango wake kwenye tasnia ya muziki na showbiz kwa ujumla.

Mwigizaji Samuel L Jackson ndiye staa wa pekee nje ya muziki kutunukiwa tuzo hii adimu isiyotolewa kwa mtu yeyote. Queen Latifah, Whitney Houston na Prince ni baadhi tu ya mastaa wengine waliopata heshima hii.

Hata kwa kizazi cha sasa cha Gen-Z, iwe unamjua kama Sean Combs, Puff Daddy, Puffy, P Diddy au Love, ni vigumu sana kwako kutotambua mchango wa huyu msela kwenye utamaduni wa tasnia ya sanaa ya Hip hop.

“Huyu ndiye msanii wangu bora katika kila kitu. Siku za nyuma muziki wa Hip hop ulikuwa na sheria nyingi sana ila yeye alizikaidi zote. Alielewa mifumo ya kimkataba kwa uketo zaidi ya wengi wetu ambao hadi sasa bado hatuna huo uelewa. Alielewa namna ya kutengeneza noti kutuzidi sisi na ndio maana mpaka leo hii yupo mbele yetu. Huwa namfuata kwa ushauri, ananitia motisha sana,” ndivyo alivyong’aka Kanye West, alipopewa fursa ya kumpokeza Diddy tuzo hiyo.

BAD BOY RECORDS, MWANZO WA SAFARI

Katika miaka ya 90, Diddy ambaye ameshinda tuzo tatu za Grammy alizindua lebo yake ya Bad Boy Records.

Ndio lebo iliyoishia kutoa mastaa kibao kama vile marehemu Notorius BIG, wakongwe Faith Evans, Mary J Blige, Lil Kim, 112, The Lox, Busta Rhymes miongoni mwa nyota wengine wengi. Mafanikio ya wasanii hawa yaliifanya lebo hiyo kuwa kubwa na ya kusifika. Kila rapa alitamani kupitia pale. Toka alipoibuni, Bad Boy Records imeuza zaidi ya rekodi 100 milioni kote duniani.

Baada ya kufanikiwa kwa lebo hii, Diddy aliamua kupanua himaya yake na kuingia kwenye biashara zingine zilizoendana na utamaduni wa sanaa.

FASHENI, TV NA MVINYO

Mnamo 1998, Diddy alizindua kampuni yake ya fasheni iliyojishughulisha na utengenezaji na uuzaji wa mavazi ya mjini iliyofahamika kama Sean John.

Kampuni hiyo ilipata mafanikio makubwa vile vile. Aliuza asilimia 90 ya hisa za kampuni hiyo kwa Global Brands Group, 2016.

Ilipoyumba kibiashara 2021 na ikalazimika kufunga baadhi ya matawi yake, Diddy aliwasilisha ofa ya kuinunua ya dola 3.3 milioni kabla ya kuongeza dau hadi dola 7.5 milioni kuwapiku washindani wake.

Isitoshe, siku moja 2013, alipata wazo la kuanzisha kampuni yake ya TV na hapo ikachipuka REVOLT Media & TV, stesheni ya kwanza ya runinga inayopeperusha muziki pekee hasa Hip hop huku malengo yakiwa ni kusapoti kizazi kipya cha Hip hop.

Mwaka huu, Diddy aliona isiwe kesi na kuanzisha lebo mpya Love Records. Lebo hii itashugulika zaidi na muziki wa RnB na ili kutoa mfano, atakuwa msanii wa kwanza kwenye lebo hiyo atakapoachia albamu yake ya kwanza ya muziki wa RnB mwishoni mwa mwaka huu.

Katika upande wa mvinyo, 2007 aliingia kwenye mkataba mzito na Diageo, kampuni ya Uingereza na watengenezaji wa mvinyo wa Ciroc Vodka. Dili hiyo ilikuwa ni yeye kupromoti brandi hiyo Marekani huku naye akipokezwa malipo ya asilimia 50 ya faida ya mauzo ya kinywaji hicho. Hii ilikuwa kazi rahisi sana kwake.

Toka 2007 ametengeneza zaidi ya dola 100 milioni kupitia dili hiyo. Mauzo ya Ciroc yaliongezeka kutoka mitungi 50,000 ya lita tisa kila moja kwa mwaka hadi milioni mbili baada ya Diddy kusaini mkataba wa kuipromoti.

2014, baada ya biashara kati yake na Diageo kunoga, waliungana na kununua kampuni ya mvinyo wa tequila, DeLeon.

DeLeon ni mvinyo unaoshabikiwa sana na mastaa wa Hollywood na uwepo wa Diddy pamoja na timu yake ya nzuri ya kibiashara, ulichangia kuzidisha mauzo.

“Kwenye Ciroc, tulikuwa tunachumbiana ila na DeLeon, hapa sasa tumeingia kwenye ndoa. Hii ni dili tamu zaidi,” aliwahi kunukuliwa Diddy.

Kumbuka, biashara zote, hizi hatajiriki tu Diddy, wanakuwepo na mameneja wanaomsaidia kuendesha shughuli pamoja na wafanyikazi wengine walioajiriwa. Kwa nini asipewe tuzo hiyo!

  • Tags

You can share this post!

Pwani ni ngome ya Raila, utafiti wa Infotrak waonyesha

KASHESHE: Eti mtasubiri ndoa sana!

T L