• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
KIKOLEZO: Muziki na siasa: Moto wa karatasi?

KIKOLEZO: Muziki na siasa: Moto wa karatasi?

NA SINDA MATIKO

UHUSIANO kati ya muziki na siasa hapa nchini unaweza ukaufananisha na mahusiano ya wasanii Harmonize au Diamond Platnumz na ma-ex wao.

Huwa ni mahusiano yanayodumu kwa muda mfupi ilimuradi kutimiza mahitaji ya muda fulani kisha yanaisha.

Mwaka huu ukiwa ni mwaka wa uchaguzi, wanasiasa wanafanya kila wawezalo kuhakikisha umaarufu wao unamfikia kila mja. Leo wapo mpaka kwenye nyimbo sasa.

Tayari kiongozi wa Azimio Raila Odinga ameshirikishwa kwenye nyimbo mbili. Moja na msanii Kevin Bahati Fire na nyingine Lelo ni Lelo aliyoshirikishwa na Emmanuel Musindi.

Mpinzani wake, William Ruto naye kafanya remix ya Sipangwingwi wimbo wake msanii Exray.

Hizi ni taswira ambazo tumekuwa tukizishuhudia kwenye chaguzi za hivi karibuni na baada ya hapo wasanii wanatokwa.

Lelo ni Lelo na Sipwangwingwi kwa sasa ndizo nyimbo maarufu kwenye mikutano ya kisiasa, lakini kabla yazo tumewahi kuzishuhudia nyingine zilizovuma kwa kuhusishwa na siasa za uchaguzi.

UNBWOGABLE – GidiGidi MajiMaji

Pengine ndio wimbo wa kwanza kuvuma sana kwenye ulingo wa kisiasa. Ngoma hiyo iliimbwa na lugha ya Kiluo kwa kuwasifia wanasiasa maarufu wa jamii la Waluo kama vile Raila Odinga, Profesa Anyang Nyong’o na Seneta James Orengo.

Ilitumiwa sana na kambi ya Raila kwenye uchaguzi wa 2002 kumshinda mrithi aliyependekezwa na Rais Moi, wakati huo kijana Uhuru Kenyatta. Wimbo huo ulivuma sana na kuongeza umaarufu wa Raila ambaye alishirikiana na Mwai Kibaki kuunda serikali ya National Rainbow Coalition.

LELO NI LELO REMIX – Emmanuel Musindi

Ni ngoma ya zamani ya msanii wa jamii ya Kiluhya Musindi aliyoamua kuifanyia remix mwaka huu kwa kumshirikisha Raila.Ndio wimbo unaotumiwa na kambi ya Azimio katika hafla zao za kisiasa.

Kwenye wimbo huo Raila anahamasisha uwepo wa amani katika kipindi hiki.

Pia anatumia wimbo huo kupigia debe ajenda yake na ahadi atakazowatekelezea Wakenya punde atakapochaguliwa. Ngoma hiyo imeimbwa kwa Kiluhya na Kiswahili. Mapokezi yake yamekuwa mazuri sana hasa kwenye ngome za kisiasa za Azimio.

TANO TENA – Ben Githae

Sifa za Ben Githae kama msanii wa injili zilikuwa kubwa mno lakini nyota yake ya usanii wa injili ilipotea alipoingia studio na kuwatungia Rais Uhuru Kenyatta na naibu William Ruto Tano Tena.

Mwanamuziki Ben Githae. PICHA | MAKTABA

Wimbo huo aliuachia kwenye uchaguzi wa 2017 uliochangia kwa kiasi fulani kumrejesha Uhuru madarakani baada ya muhula wake wa kwanza kumalizika.

Uhuru na Ruto walitumia wimbo huo kujipigia debe kwenye harakati zao za kusaka muhula wa pili.

MAMBO YANABADILIKA – Hellen Ken

Wakati Uhuru wakimtumia Ben Githae kwenye tano tena, Raila alitumia kazi ya Hellen Ken kujipigia debe akiahidi kuleta mabadiliko.

Wimbo huo alitumia kusukuma ajenda ya mrengo wa NASA muungano aliotumia Raila kugombea Urais wa 2017. Aidha, wimbo huo ndio ulimtambulisha vizuri Hellen kwenye gemu na kumpa umaarufu kiasi cha haja.

NASA – Onyi Jalamo

Kuelekea uchaguzi wa 2017, Raila hakuwa na nyimbo moja tu ya kujipigia debe. Nyingine ilikuwa Nasa iliyotungwa na Jalamo ili kuendana na mada ya mrengo wa NASA.

Ngoma hii ilitamba na ndiko mojawepo ya misemo maarufu kama vile ‘Tibim’ ilichipukia.

Mdundo wa nyimbo hii umetokana na mianguko na miinuko ya sauti ya Kiluo Ohangla.

Wakati wimbo wa Hellen ulikuwa wa kuhamasisha kuhusu mageuzi mapya ambayo yangefanywa na Raila, NASA ulikuwa kuonyesha nguvu ya mrengo huo.

You can share this post!

Rais Kenyatta aungana na waombolezaji kwa ibada ya kumuaga...

Mlalamishi aondoa kesi ya kupinga azma ya Sonko

T L