• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 3:45 PM
KIKOLEZO: Penzi lakubali mabosslady!

KIKOLEZO: Penzi lakubali mabosslady!

NA  SINDA MATIKO

KWA miaka na mikaka, suala la mpenzi wa kike kumpiku mpenziwe kipato limeishi kuwa donda ndugu.

Uzunguni kidogo hili sio tatizo ila huku kwetu Barani Afrika, wanaume wengi huhaha sana pale wapenzi wao wa kike wanapowazidi kipato.

Wengi huingiza njeve na kuhisi hawatakuwa na sauti nyumbani au uzito kwenye maamuzi kutokana na hilo.

Lakini majuu kuna mademu wenye mpunga kinoma kuwaliko wapenzi wao wa kiume na bado tu penzi lao lipo juu ya mstari.

RIHANNA (Dola 1.7b)

ASAP Rocky (Dola 10m)

Wamekuwa wapenzi kwa miaka minne sasa na hata wameshabarikiwa kumpata mtoto wao wa kwanza.

Katika umri wake wa miaka 34, hakuna mwanamume aliyewahi kufanikiwa kupanda mbegu Riri hadi alipokutana na Rocky.

Kwa wanaume aliowahi toka nao, ni Rocky tu ndiye pengine hajawahi kumzidi kipato.

Kabla yake, Riri alikuwa akitoka na bilionea wa Saudi Arabia, Hassan Jameel. Aliachana naye 2017 na kuanza kuwa na ukaribu na Rocky kabla ya urafiki wao kuotesha penzi.

Rocky ni mshikaji tu ambaye alimbamba mrembo huyu. Nafikiri hata kama angelikuwa maskini hohehahe, bado tu msupa huyu angempenda.

Riri amegeuka kuwa bilionea akiwa na msela, lakini siku zote wameendelea kuonyesha penzi lao zito. Mara si moja wamevumishwa kutemana lakini wawili hao mwisho wa siku wameishia kuwakomoa mapaparazi. Kwa hawa, ishu ya hela sio kitu, vibe ndio mambo yote.

CARDI B (Dola 42m)

OFFSET (Dola 26m)

Kama kuna rapa wa kike ninayependa vibe lake, ni Cardi B.

Huwa ana ujasiri wa kiajabu. Anapenda kujieleza hata yale mambo ya siri. Kwa mfano kuna siku alipeana mafunzo ya jinsi mwanamke anapaswa kuosha makalio yake.

Pamoja na ukorofi wake, Cardi B ana moyo wa kupenda. Ndio sababu alimkufia rapa mtukutu Offset na hata kuzaa naye mara mbili.

Baada ya ujauzito wa kwanza, walitengana akimshtumu kwa kumchepukia. Mwanamume alijitahidi kumbembeleza demu na kumrudisha tena kwenye himaya yake kisha akamdunga mimba ya pili.

Hapa Cardi B pamoja na hela zake kama njugu hakuwa na uwezo, hakuwa na nguvu, alimwachia baba mtu ale vitamu bila ya kumwonyesha ujeuri. Bado tu wapo pamoja. Kwenye ugomvi wao, hawajawahi kuvurugana, kisa hela.

JESSICA ALBA (Dola 350m)

CASH WARREN ( Dola 20m)

Wamedumu kwenye ndoa yao kwa miaka 14 sasa toka 2008. Hata hivyo, kwa ujumla wamekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa miaka 18.

Alba 41, ndiye mwenye pochi nene nyumbani akimpiku kwa mbali mume wake mwenye jina lenye maana ya pesa. Licha ya kipato kidogo cha Warren, penzi lao lipo pale pale. Kwao mahaba ni zaidi ya fedha na ndio sababu mpaka leo wanaendelea kugandana kama gundi.

OPRAH WINFREY (Dola 3.5b)

STEDMAN GRAHAM (Dola 10m)

Oprah Winfrey ndiye mwanamke tajiri zaidi kwenye tasnia ya burudani akifuatiwa na Riri. Bibiye ana utajiri unaofikia dola 3.5 bilioni.

Amekuwa na Graham toka 1986 akiwa ndio ameanza kusaka utajiri wake. Graham mwenye miaka 71, amepata umaarufu kutokana na kuwa na Oprah. Yeye ni mwalimu na kipato chake ni dola 10 million. Hata hivyo, penzi lao halijawahi kuyumba.

GWEN STEFANI (Dola 100m)

BLAKE SHELTON (Dola 60m)

Wanamuziki hawa walikutana 2014 walipopata kazi ya kuwa majaji kwenye shindano la kuimba la The Voice.

Urafiki ukaota na kisha penzi likafuata. 2021 baada ya kuwa pamoja kwa muda, staa wa Country Music Shelton, 46, akaamua kumuoa staa huyo wa Pop mwenye umri wa miaka 52.

Ukiachana na tofauti ya umri ambayo haikuwajalisha, pia tofauti ya kipato haikuwazuia kuwa pamoja. Hakutishika na utajiri mkubwa wa mpenzi wake, alichotaka sio pesa bali kuwa na Stefani.

JULIA ROBERT (Dola 250m )

DANIEL MODER (Dola 10m)

Mwigizaji Julia Roberts anatengeneza mkwanja wa maana ambao mume wake mtengenezaji filamu hawezi kuunusia.

Kwa kifupi Roberts ndiye anatoa matunzo zaidi lakini hilo halijakuwa kikwazo katika penzi lao. Wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 20 sasa na penzi lao halijawahi kuyumba hata siku moja. Pesa kwao sio hoja, penzi ndio kila kitu.

You can share this post!

Wainaina Anthony Njoroge amshukuru Mungu na wakazi wa Kieni

ODM yapokonywa ubunge Ganze ubingwa ukimwendea Kenneth...

T L