• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
KIKOLEZO: Walivyofungwa na mikataba ya kinyonyaji

KIKOLEZO: Walivyofungwa na mikataba ya kinyonyaji

NA SINDA MATIKO

UKIMTIZAMA rapa mkongwe wa Marekani Birdman na staa wa Bongo Flava Diamond Platnumz, utagundua wanafanana.

Hawafanani kwa kuzungumza, sura, maumbile au nini, ila wanafanana kwenye dunia ya muziki.

Wote ni wanamuziki wakubwa wenye heshima zao lakini pia ni ma-CEO wa lebo kubwa, Diamond akiwa ni mmiliki wa WCB Wasafi naye Birdman akimiliki Cash Money Records.Lebo zote hizi mbili zimewatoa mastaa kadhaa ukizungumzia watu kama Lil Wayne, Drake, Nicki Minaj, Harmonize, Rayvanny, Zuchu miongoni mwa majina mengine tajika.

Sifa za Birdman na Diamond katika kutambua vipaji vinavyoishia kuwa imara, zinashabihiana.

Lakini kando na sifa zao za kujenga lebo za nguvu, pia wameonyesha weledi wa kuongoza biashara hiyo.

Ila usisahau pia, Birdman na Diamond wamejikuta kwenye utata na baadhi ya wasanii waliowatoa wakishtumiwa kuwafunga na mikataba ya kinyanyasaji.

Yanayoendelea sasa kwenye lebo ya WCB, yalishatokea kule New Orleans, Marekani yaliko makao makuu ya Cash Money Records.

LIL WAYNE AZENGUANA NA BIRDMAN

Birdman, 53, alikutana na Lil Wayne, 39, akiwa na umri wa miaka tisa tu mtaani.

Baada ya kukigundua kipaji chake, alimchukua na kuanza kumlea kama mwanawe. Aliishia kumsaini Cash Money Records na taratibu akaanza kumwandaa kwa ajili ya mafanikio ya siku za usoni.

Akiwa na umri wa miaka 18, alilipuka na kuwa staa mkubwa wa Hip hop. Baada ya kuachia albamu kadhaa ikiwemo The Carter III iliyouza kama njugu 2008 na kuongeza umaarufu wa mastaa hao na lebo yenyewe, uhusiano wao waliouita wa ‘mtu na babake’ ulizidi kunoga. 2012, Lil Wayne akasaini mkataba mwingine wa kuendelea kuwa chini ya himaya ya Cash Money.

Mpango ukawa ni kuachia albamu nne, lakini baada ya kuachia moja kukazuka bifu.

Akaomba kuvunja mkataba pamoja na kukabidhiwa hakimiliki ya kazi zake zote alizotoa chini ya lebo hiyo.

Birdman akaganda. Vuta nikuvute ikaendelea. 2014 alipokuwa akijiandaa kuachia albamu ya The Carter V, Cash Money ikamzuia kutokana na vipengele vya mkataba. 2015, akawasilisha kesi akidai fidia ya dola 51 milioni kama malipo ya mapato ya muziki wake aliodai lebo ilikuwa imeganda nao.

Baada ya mvutano wa miaka kadhaa, wakayamaliza nje ya korti 2018, huku Lil Wayne akifanikiwa kupata haki yake aliyokuwa akiililia. Mwaka huo ikatoka The Carter V. Baada ya hapo akaamua kuwa huru ingawaje uhusiano wake na Birdman ulirejea kuwa kama zamani.

HARMONIZE ATIBUANA NA DIAMOND

Picha ya Lily Wayne na Birdman, ilijirudia WCB. Harmonize alikutana na Diamond 2013 kwenye shoo moja.

Kipindi hicho Diamond alikuwa tayari ameshahiti na kuwa msanii mkubwa.

Harmonize kwa upande wake ndio alikuwa anaanza. Baada ya kuonyesha matamanio ya kumfikia Diamond, aliishia kufanikiwa kupata namba yake na akajitetea.

Diamond ambaye tayari alikuwa kwenye pilkapilka ya kuanzisha lebo, alimsikiliza na kuona kipaji. Aliamua kumweka chini ya mabawa yake.

Alimsaini 2014 akiwa msanii wa kwanza WCB ilipozinduliwa. Mwaka mmoja baadaye, akaachia hit yake ya kwanza Aiyola chini ya lebo hiyo iliyofanya vizuri sana hasa ukizingatia ilisukumwa sana na WCB.

Harmonize akaanza kupata shoo na pesa zikaanza kuingia.

Pale WCB alikuwa kasaini mkataba wa miaka 10. Baada ya miaka mitano, utata ukazuka na akaomba kuondoka lakini haikuwa rahisi.

Kwa maneno yake anasema ilifika wakati WCB iliacha kuusukuma muziki wake na akawa anajipambania mwenyewe huku mwisho wa siku lebo ikichukua 60% ya mapato yeye akipata 40%.

Ili kuvunja mkataba wake, Harmonize alilazimika kulipa fidia ya Sh24 milioni ili aweze kupewa hakimiliki ya kazi zake zote alizozifanya chini ya lebo hiyo.

Miezi michache baada yake kuondoka, akafuata Rich Mavoko ikiwa ni mwaka mmoja tu toka alipoikimbia lebo ya Kaka Empire na kutua WCB. Naye kuondoka haikuwa rahisi.

Ilimlazimu kuishtaki WCB kwa Baraza la Sanaa Tanzania-BASATA akilalamikia mkataba wa kinyonyaji. Alishinda kesi na mkataba ukavunjwa.

RAYVANNY NI 100M AONDOKE WCB

Ndio stori inayozungumziwa kwa sasa. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, Rayvanny amekuwa akivumishwa kuihepa lebo hiyo, madai ambayo ameishi kupinga.

Juzi kati safu hii ilipata taarifa kwamba alikusudia kujitoa mwezi uliopita lakini mlango wake ukapigwa kufuli na WCB.

Taarifa hizo zinaarifu kuwa Rayvanny alifanikiwa kupata mdhamini aliyedhamiria kuwekeza kwenye lebo yake ya Next Level aliyoizindua akiwa WCB.

Msanii Rayvanny na bosi wake Diamond Platnumz. PICHA | MAKTABA

Lakini mdhamini akasisitiza kwamba ili awekeze ni lazima awe msanii huru ili kuepusha migongano na menejimenti ya WCB.

Alipowasilisha taarifa hizo kwa WCB, aliambiwa ili kujitoa na akabidhiwe hakimiliki ya kazi zake zote, ni lazima alipe fidia ya Tsh2 bilioni (Sh97 milioni) ili kuvunja mkataba huo.

Kwa kukosa fedha hizo, jamaa ameamua kusalia humo mpaka pale mkataba wake utakapofika mwisho.

“Yamesemwa mengi kuhusu mimi kutoka WCB lakini nataka ifahamike kuwa nipo huku bado. Ikifika wakati Rayvanny ajitoe, basi nitajitoa ila kwa sasa bado nipo WCB,” alisema Rayvanny mwezi Februari wakati akipinga tena tetesi hizo za kujitoa WCB.

You can share this post!

Ulaya yaililia Afrika iiunge kulaani hatua ya Urusi...

Tisa kumteua mmoja awakabili Raila, Ruto

T L