• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
KIKOLEZO: Watoboka maelfu kuzidisha mvuto

KIKOLEZO: Watoboka maelfu kuzidisha mvuto

Na THOMAS MATIKO

DUNIA ya sasa mambo yanakwenda kwa kasi ya 4G.

Ukiachana na utandawazi, pia kwenye masuala ya mionekano wadau hasa hasa maceleb wameamua kwenda kwa kasi hiyo.

Tofauti na miaka ya nyuma, sasa maceleb wengi wanatumia kila mbinu kujiboreshea mwonekano wa mwili.

Wakati wengine wakikesha ‘gym’ na kula vizuri na kunywa maji kwa wingi ili kuwa na umbo la kuvutia, wapo wenzao wameamua kwenda njia za mkato.

Hawa wameamua kutumia maelfu au mamilioni ya pesa kubadilishia mionekano yao. Leo tunashuka na maceleb wa humu nchini waliotoboka maelfu ya pesa kujibadilisha ili waweze kupendeza zaidi.

VERA SIDIKA

(Upasuaji wa matiti)

Miaka michache iliyopita Vera alifichua kwamba alifanyiwa ‘plastic surgery’ ili kuongeza maziwa yake. Alitumia zaidi ya Sh2 milioni kule Beverly Hills, Marekani kunyooshwa matiti yake ili yawe makubwa kidogo.

Kulingana naye, alifanya hivyo ili kujisawazishia maumbile. Kuna tetesi zinazodai kwamba pia aliongeza makalio yake. Hata hivyo ameishi kukana kwa kusema makalio yake ni asili.

Kando na upasuaji huo wa matiti, pia Vera amebadilisha ngozi ya rangi yake na kuwa mweupe zaidi. Tetesi zinadai kuwa kufanikisha utaratibu huu, alidungwa sindano ya kijalizo aina ya glutathione (supplement) ambayo husaidia pakubwa kubadili rangi ya ngozi ya mtu.

HUDDAH MONROE

(Upasuaji wa matiti)

Huddah kama mwenzake Vera, naye alitimkia zake Marekani na kufanyiwa upasuaji kuongeza ukubwa wa matiti yake.

Binti huyo soshiolaiti aliwahi kukiri miaka ya nyuma kidogo kwamba upasuaji huo nusura umletee maafa baadaye kwani aliishia kukumbwa na tatizo la kiafya. Alihitaji upasuaji mwingine ili kurekebisha hali hiyo.

Alidai kutumia zaidi ya Sh1 milioni kuongezwa maziwa yake. Sababu kuu ya kufanya hivyo ikiwa ni kujizidishia mvuto. Lakini pia Huddah kama mwenzake Vera naye kabadili ngozi yake na kuwa mweupe kuliko alivyokuwa zamani.

BIG TED

(Upasuaji wa utumbo)

Mcee na promota wa burudani Big Ted kwa miaka mingi alihangaishwa sana na unene kupindukia. Miaka miwli iliyopita Big Ted alikuwa na uzani wa kilo 168. Nyakati hizo, suti yake yenye ukubwa wa inchi 68, ingetosha kushona mbili za mtu mwembamba.

Afya yake ilikuwa hatarini kutokana na unene. Mwonekano wake ulikuwa wa kiajabu ajabu. Big Ted anasema baada ya kujaribu mazoezi na lishe kwa muda, alihisi hasaidiki.

Hapo akaamua kutumia njia ya mkato ambapo alisafiri zake India alikofanyiwa upasuaji wa utumbo al-maarufu gastric bypass kwa gharama ya Sh700, 000.

Huu ni upasuaji wa kupunguza ukubwa wa tumbo la mhusika hivyo kumfanya kushiba kwa chakula kidogo sana. Upasuaji huu ulimsaidia kupunguza kilo hadi kufikia 95 ambazo zipo vizuri naye ukizingatia kuwa ni jitu la urefu wa futi sita.

Mwonekano wake ukawa bora zaidi, tofauti na zamani. Suti zake zikavutia zaidi, kuliko awali.

RISPER FAITH

(Upasuaji wa kufyonza mafuta)

Alipata umaarufu wake kupitia kipindi cha masoshiolaiti Nairobi Diaries. Umaarufu wake ulichangiwa sio tu na drama zake lakini pia maumbile yake. Risper ni mwanamke wa miraba minne. Ni mkubwa kimaumbile.

Baada yake kujaliwa mtoto wake wa kwanza, aliongeza unene kwa kiwango kikubwa sana. Baada ya kuhangaika kwa muda, alitembelea hospitali moja jijini Nairobi ambapo alifanyiwa liposuction. Huu ni upasuaji wa kufyonza mafuta kutoka maeneo fulani ya mwili.

Risper alifichua kwamba alikamuliwa zaidi ya lita nane za mafuta kutoka maeneo yake ya tumbo na mgongoni. Ilimgharimu Sh450, 000. Kwa sasa mwonekano wake ni wa kupendeza sana kuliko hapo awali.

FASHIONABLE STEP MUM

(Upasuaji wa utumbo)

Catherine Njeri al-maarufu Fashionable Step Mom ni mmoja kati ya ma-vloga wenye followers wengi nchini.

Kwenye mojawapo ya vlog zake, Njeri anasema aliamua kufanya upasuaji wa gastric bypass ili kupunguza unene aliokuwa nao. Ni unene anaosema ulisababishwa na mbinu za kisasa za upangaji uzazi.

Lakini pia wakati huo alikuwa na tatizo la kiafya lifahamikalo kama ‘hiatal hernia’. Alisafiri kwenda India kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha tatizo hilo na ni akiwa huko pia aliomba kufanyiwa gastric bypass uliomwezesha kupoteza kilo tisa ndani ya mwezi mmoja.

RACHEL MARETE

(Upasuaji wa matiti)

Marete ambaye ni Miss Universe Kenya 2005, aliwahi kufichua kwamba alifanyiwa upasuaji kuongeza maziwa yake ili aweze kuwa na mvuto zaidi. Lakini pia anasema alifanyiwa liposuction kufyonza mafuta kwenye maeneo ya tumbo lake ili kumpa shepu na figa.

Hii ilikuwa baada yake kumeza tembe za upangaji uzazi zilizoishia kumsababisha kunenepa gafla. Upasuaji huu ulimwezesha kupoteza kilo 20 ndani ya mwaka mmoja.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Shirk ni dhambi lililo juu kabisa ya...

TAHARIRI: Serikali itoe ushauri nasaha kwa umma