• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Shirk ni dhambi lililo juu kabisa ya makosa mengine katika Uislamu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Shirk ni dhambi lililo juu kabisa ya makosa mengine katika Uislamu

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Somo la Tawhid haliwezi kuwa timilifu bila ya kusoma na kuchambua kwa kina juu ya Shirk, shirk ni kinyume cha Tawhid na ni dhambi yenye uzito mkubwa mno.

Vile vile ni dhulma kubwa ambayo binadamu anaweza kuifanyia nafsi yake. Kama tulivyoona katika makala zilizopita, Allah (sub-hanahu wa ta’ala) ameahidi kutoisamehe iwapo aliyetenda hakufanya toba hapa duniani. Allah (‘azza wa jall) amesema katika kitabu chake kitukufu kwamba: Hakika Allah hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Allah basi hakika amezua dhambi kubwa (4:48)

Aya hii tukiifafanua zaidi tunapata mafunzo mengi ndani yake kama ifuatavyo: “Hakika Allah hasamehe kushirikishwa” – Katika sehemu hii ya aya, Allah ta’ala anaonyesha hali (mood) ya ukali katika suala la kushirikishwa ili sisi tulioumbwa tupate kulipa suala hili uzito unaostahiki, ikiwa ni wenye kutafakari.

Hili ni onyo la kiwango cha juu kabisa, tukumbuke Allah havunji ahadi yake na kwamba ametumia neno HAKIKA kabla ya kutuambia kwamba hatosamehe. Hili si jambo linaloweza kubadilika au kwamba lina mashaka ndani yake.

“Yaliyo duni ya hilo” inadhihirisha mambo mawili makubwa; Ukubwa wa kosa hili la kumshirikisha Allah ta’ala, kwamba shirk ni kosa lililo juu kabisa na madhambi mengine yapo chini ya dhambi hii. Vile vile maneno haya matukufu yanaonyesha upole wa Allah ta’ala kwani maana nyingine ni kwamba Allah ‘azza wa jall anasamehe yote yaliyo chini ya shirk. Huu ni urahimu wenye kuonyesha anga la upole na huruma wa Allah ‘azza wa jall.

“Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa” – Allah ‘azza wa jall anasisitiza zaidi juu ya uzito wa dhambi hii baada ya kuelezea kwamba madhambi mengine ni duni juu ya hii.

Aya hii ina mtiririko wa ajabu, kwanza imeonyesha uzito juu ya uzito wa dhambi hii; yaani dhambi iliyo juu kisha ni kubwa. Halafu ikatoa onyo kwa wenye kufanya shirk na ndani ya onyo hilo imeonyesha upole wa Allah katika yasiyo kumshirikisha.

Shirk imegawika kama ilivyogawika Tawhid, Yaani kuna shirk katika ar Rubuubiya, shirk katika al Uluuhiya na shirk katika al Asma’ wa sifaat. Inshallah katika makala zijazo tutaelezea maana ya shirk na kisha shirk kama zilivyogawanyika katika ar rubuubiya, al uluuhiya na asma’ wa sifaat.

Kumfanyia ushirika Allah ‘azza wa jall ni kukanusha lengo la kuumbwa kwetu na ndio sababu ya msingi ya kuwa Allah ta’ala hatosamehe kosa hili iwapo iliyelifanya hajatubu.

Katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Hurayra (radhi Allahu ‘anh), Mtume (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) amezitaja dhambi saba kubwa kabisa nazo ni: Kumshirikisha Allah na uchawi, kuua nafsi ambayo Allah ameiharamisha isipokuwa kwa kuifanyia haki (yaani kuua baada ya kuhukumiwa kwa misingi ya kiislamu hii imeruhusiwa), kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia siku ya vita (jihaad) na kumsingizia muumini mwema wa kike asiyejua ubaya (uzinifu) (Bukhari).

Kutokana na hadithi hii ni wazi kuwa shirki si jambo linalohitaji kupewa nafasi kwenye maisha ya Muislamu, na shirk imetajwa mwanzo katika hadithi hii kwa kuwa ndio dhambi kubwa kuliko zote zilizomo kwenye hadithi hii. Vile vile Abdullah ibn Mas’ud (radhi Allahu ‘anh) alimuuliza Mtume (salla Llahu ‘alayhi wasallam) ni dhambi ipi iliyo kubwa kabisa, Mtume (salla Llahu ‘alayhi wa sallam) alisema: Kumpa Allah mpinzani hali ya kuwa yeye pekee ndiye aliyekuumba (Bukhari na Muslim).

Hadithi hii inatutanabahisha juu ya ukweli kwa Allah sub-hanahu wa ta’ala ni pekee aliye Rabb, Mola aliyeumba na kusimamia kila kilichoumbwa, kwa hiyo hata kwa akili zetu iwapo tunalijua hili, ni wizi kwamba si haki kumfanyia Mola wetu mshirika.

  • Tags

You can share this post!

Amerika yatoa tahadhari kuhusu corona Tanzania

KIKOLEZO: Watoboka maelfu kuzidisha mvuto