• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
KIKOLEZO: Youtubers kimeumana

KIKOLEZO: Youtubers kimeumana

Na THOMAS MATIKO

HIVI majuzi kampuni ya Google ilitoa tangazo la kuwavunja mioyo vloggers wanaotegemea YouTube kuingiza pesa.

Kupitia barua pepe kwa wengi wanaoishi nje ya Marekani yaliko makao makuu ya Google, iliwafahamisha kutakuwepo na mabadiliko makubwa kwenye malipo.

Tofauti na hapo awali, sasa posho watakalokuwa wakipata litapungua kwa kiwango fulani. Kampuni hiyo iliwafahamisha kwamba kuanzia sasa itakuwa ikilipa makato ya ushuru kwa serikali ya Marekani kutoka kwa chaneli zote za Youtube zikiwemo za wale wanaoishi nje ya taifa hilo.

Kila mwenye chaneli ya Youtube atatakiwa kuwasilisha ripoti yake ya ushuru kutokana na mapato yake kwenye Youtube kufikia Machi 31, 2021. Yule atakayekosa kufanya hivyo, basi Youtube italazimika kukata ushuru wa asilimia 24 kutoka kwa mapato yake ya jumla.

Ifahamike kuwa, malipo ya Youtube hufanywa na kampuni ya Google Adsense. Wenye chaneli za Youtube hulipwa kwa kutegemea na ‘Cost Per Mile (CPM), yaani malipo kwa kila 1,000 ‘views’ au ‘clicks’ katika tangazo. Kwa kawaida huwa yapo matangazo yanayoambatishwa na mzigo aliouposti vlogger. Lakini kingine, ili kuanza kulipwa na Youtube ni lazima posti zako ziwe na ‘views’ zisizopungua masaa 4,000 na angalau ‘subscribers’ 1,000. Youtube hulipa Sh800 kwa kila ‘views’ 1,000.

Sasa basi, kwa taarifa hiyo, baadhi ya watu watakaopata pigo kubwa humu nchini wanaoongoza kwa kuingiza mkwanja mkubwa kupitia chaneli zao za Youtube, watakuwa kwa mfano, wafuatao waliounda listi ya Youtubers 10 bora waliolipwa mshahara mkubwa 2019/20.

NANCIE MWAI

Vlogger Mwai alikamata nafasi ya 10, akiwa na ‘subscribers’ 43,200. Katika kipindi hicho chaneli yake ilivutia ‘views’ 804,000.

Sehemu kubwa ya posti zake zilihusu masuala ya vipodozi, jinsi ya kupaka, aina gani bora na mambo kama hayo.

Kupitia stori zake pia alitumia fursa hiyo kuzipigia debe kampuni mbalimbali za vipodozi ambazo zilimpa dili za matangazo biashara. Kwa maana hiyo aliweza kuongeza kipato chake kando na mshahara wa Youtube.

JOY KENDI

Vlogger Joy Kendi alikamata nafasi ya tisa akiwa na ‘subscribers’ 44,000 ambao sasa wameongezeka hadi 55,600.

Posti nyingi za Kendi zinahusu utalii na maeneo mbalimbali ya kujivinjari hasa ya kifahari anayozuru na kisha kutoa uchambuzi. Pia huposti masuala ya fasheni, vipodozi na afya. Kupitia kazi zake za Youtube, pia ameweza kuzipa shavu kampuni mbalimbali kama vile Colgate na Ciroc. Ni mmoja kati ya wale watakaoumizwa na tangazo la Google hasa ukizingatia namna chaneli yake inavyozidi kuwa kubwa.

MANDI SARRO

Posti za chaneli yake huangazia mambo mbalimbali ikiwemo utalii lakini kubwa zaidi analofahamika nalo ni masuala ya upishi.

Wakati wa ukusanyaji wa data hizi za 2019/20 chaneli yake ilikuwa na ‘subscribers’ 63,000 ambao sasa wamepanda na kufikia 70,900.

Toka alipoanzisha chaneli yake 2013 mpaka kufikia kipindi hiki, imevutia ‘views’ 4.8 milioni kwa ujumla.

Ssaro alipata umaarufu wake mkubwa alipokuwa akifanya kazi ya utangazaji kwenye redio ya Capital FM alikojipigia debe sana na pia kutambulisha utaalamu wake wa mapishi. Posti zake za mapishi mara nyingi huwa ni maujanja ya jikoni. Tangazo la Youtube hakika halitamfurahisha.

SHARON MUNDIA

Chaneli yake iitwayo This is Ess, ina ‘subscribers’ 68,300 ikiwa imepanda kutoka 63K wakati data hizo zilikusanywa.

Toka alipoanzisha chaneli yake 2013, imeweza kuvutia jumla ya ‘views’ milioni sita na kumweka katika nafasi nzuri ya baadhi ya vloggers ambao hupokea mshahara mkubwa kutoka Youtube.

Posti zake huangazia masuala mbalimbali ambayo kwa kawaida huwa yamefungana na maisha yake ya kila siku. Inaweza ikawa ni usafiri, usafi wa nyumbani, tizi na mambo mengine ya dizaini hiyo.

THE GREEN CALABASH

Chaneli hii ni ya wazazi vijana ambao huangazia zaidi malezi ya watoto wao. Chaneli hii imekuwepo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Wakati wa ukusanyaji wa data hizi, ilikuwa na ‘subscribers’ 73,000 ambao sasa wameongezeka hadi 83,600. Kwa ujumla imeweza kuvutia ‘views’ milioni tisa.

OVER 25

Ni chaneli ya mabinti wanne; Ivy Mugo, Julia Gaitho, Lorna Muchemi na Michelle Wanjiku. Chaneli yao ilikuwa na ‘subscribes’ 75,000 wakati wa kufanywa kwa ripoti hii ila sasa imepanuka hadi kufika 91K.

Sehemu kubwa ya posti zao huhusu zaidi mahusiano ya kimapenzi na wanaume, masuala ya chumbani, ujasiriamali na masuala ya fulusi.

RONOH CHEBET

Binti huyu mchekeshaji mwenye miaka 19, alianzisha chaneli yake 2017 lakini tayari kawapita wengi walioanza zao zama zile.

Wakati wa uandaaji wa ripoti hii alikuwa na ‘subscribers’ 104,000 ambao sasa wameongezeka hadi 122K. Chaneli yake imevutia zaidi ya ‘views’ 3 milioni. Posti zake huhusu zaidi maisha yake ya kila siku na matukio ya kila siku yanayotrendi.

JOANNA KINUTHIA

Ni kati ya Youtubers wanaopiga mkwanja wa uhakika kutoka Youtube na hakika tangazo hili litamuumiza. Posti zake huhusu zaidi fasheni na vipodozi na jinsi ya kutunza uso wako.

Wakati wa uandaaji wa ripoti hii alikuwa na ‘subscribers’ 128,000 ambao sasa wameongezeka na kufikia 137K. Brandi nyingi za vipodozi zimekuwa zikimfuata kufanya kazi naye. Tangu alipoanzisha chaneli yake, amevutia zaidi ya ‘views’ 11 milioni.

WABOSHA MAXINE

Mwanafunzi huyu wa ujasiriamali katika chuo kikuu cha Nairobi alikamata nafasi ya pili akiwa na ‘subscribers’ 174,000 ambao sasa wameongezeka hadi 197K.

Chaneli yake imevutia ‘views’ 14 milioni kutokana na posti zake zinazohusu urembo, usafiri, fasheni na maisha ya ujumla.

NJUGUSH

Unaweza kusema ndio msanii wa pekee na tena mhusika wa kiume kwenye listi hii ya 10 bora. Amekuwa akipiga pesa kwa muda mrefu sasa na vipande vyake vya vichekesho hasa akiwa na mke wake Celestine Ndinda al-maarufu Wakavinye. Wakati mwingine vichekesho hivi huwa ni matangazo.

Ni miongoni mwa wachache nchini waliofanikiwa kujitajirisha na Youtube. Wakati wa ukusanyaji wa data hizi, chaneli ya Njugush ilikuwa na ‘subscribers’ 352,000 na sasa imefikia 465k. Kwa ujumla imevutia zaidi ya ‘views’ 58 milioni.

You can share this post!

Mtambue msanii Geerah The Boy kutoka Pwani

DOMO KAYA: Asante ya punda mateke