• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
DOMO KAYA: Asante ya punda mateke

DOMO KAYA: Asante ya punda mateke

Na MWANAMIPASHO

WIKI hii, Jacob Obunga al-maarufu Otile Brown alifungua moyo na kuzungumzia mengi kuhusu mahangaiko wapitiayo wasanii wa humu nchini katika mishemishe yao ya kusaka maisha.

Mawazo ya Otile yalikuwa na mengi ya ukweli ila kuna jambo lililonikwaza.

Katika taarifa yake ndefu, Otile alidai kuwa tasnia ya muziki inakuwa kwa kasi ya konokono kwa sababu ya makateli walioiteka. Pia alisema kuwa serikali imeshindwa kuwasaidia wasanii. Katika hili kuna ukweli. Ila kilichonipasua moyo zaidi ni pale alipovishtumu vyombo vya habari vilevile kwa kukosa kusapoti wasanii.

Naomba nisema hivi; toka nilipoanza shughuli hizi za uandishi wa burudani, nimemshuhudia huyu Otile akikua kutoka msanii limbukeni hadi anakuwa staa.

Kwa watu wote wanaoweza kujitokeza na kukashifu vyombo vya habari kwa kutowasapoti, kwa kweli sikutegemea kumwona akijiongeza.

Otile tangu anaanza muziki wake, vyombo vya habari vimemshika mkono. Kila anachokifanya kinaangaziwa. Kuna wakati jamaa aliamua kuchezea umma na kiki za mara kwa mara kisha anaachia ngoma. Kiki hizo nakumbuka zikiangaziwa sana na vyombo vya habari.

Uhusiano wake feki na Vera Sidika tuliandika sana. Nyakati hizi, kila alipoachia ngoma, ziliishia kuwa hiti.

Kwa miaka miwili iliyopita bado vimekuwa vikiripoti mafanikio ya kazi zake. Kwa mfano Boomplay ilipotoa listi ya wasanii walioongoza kwa ‘streams’ na jina lake likawepo miongoni mwa tatu bora, nakumbuka stori kadhaa ziliandikwa kuhusu mafanikio yake.

Kama ni sapoti ya kimatangazo Otile kapata kutoka kwa vyombo hivi bila kulipia hata senti. Kama sio kusemwa, na kuandikwa kwa sanaa yake, muziki wake pekee haungetosha kumfanya ajulikane. Hivi unafahamu ni wasanii wangapi wenye vipaji vikali ila hawajulikani?

Nakumbuka kabisa kipindi akiwa hana chochote wala lolote, ungelimpigia simu ukihitaji kufanya naye mahojiano, angekurupuka fasta na kujitokeza. Hii ni kwa sababu alijua bayana kwamba vyombo vya habari vilitoa nafasi kubwa kumtangaza yeye.

Ila jamaa baada ya kuonja umaarufu na kuwa staa mkubwa, kiburi kimetawala. Sasa hivi huyu hutoa mahojiano kwa kutegemea na mahusiano yake na yule mdau wa habari. Kama hauna ushikaji, jamaa hatakupa muda wake. Ndio kafikia huku. Inakuwaje leo anashtumu vyombo vya habari kwa kutotoa sapoti kwa wasanii? Au sapoti anayozungumiza haswa ni ipi? Alitaka alipwe au alitaka sapoti ya aina gani?

Hakika asante ya punda ni mateke. Ndicho anachokifanya Otile na inasikitisha sana. Kwa kweli binadamu hatuna shukrani. Leo nimeamini kabisa wimbo wake Nyota Ndogo Watu na Viatu. Itakuwa kipindi alipokuwa akitunga mashairi ya wimbo huo, alikuwa tayari kakutana na watu wa sampuli ya Otile. Aisee! Yaani bado siamini. Mwambieni mwenzenu aache ufala, umaarufu huisha!

You can share this post!

KIKOLEZO: Youtubers kimeumana

Jinsi ya kuandaa shawarma ya minofu ya kuku