• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
KIPWANI: Kabisha majuzi tu tena kwa mshindo

KIPWANI: Kabisha majuzi tu tena kwa mshindo

NA SINDA MATIKO

KUTOKA Kaunti ya Kilifi, kuna binti wa miaka 20 anayekuja kwa staili tofauti kabisa. Kila unaposkiza muziki wa Nasha Travis, utakutana na vionjo vya Afro Pop na RnB kwenye kazi zake. Wiki jana tulipiga stori na msupa ili kumwelewa zaidi. Huu ndio ubwabwa aliotupakulia.

Hebu tuanzie mwanzo, majina yako kamili, mtaa wako ni upi, umekulia wapi na skuli umesomea wapi?

Majina ni Natasha Mugure Jessy, ila kiusanii ni Nasha Travis. Nimezaliwa na kulelewa Mtwapa, Kilifi na mbali na muziki pia mimi ni mwanachuo ninakosomea Usimamizi Biashara.

Watu wengi wameanza kukutambua majuzi, hivi umekuwepo kwa muda au?

Kama ni muziki nilianza zamani toka nikiwa mdogo ila kuufanya kama pro, nimeanza Novemba 2020 ngoma yangu ya kwanza ikiwa ni Pambana.

Kinachonishangaza ni kuwa umekuja juzi na tayari umeshatoa EP, ‘The Africa Sound Queen’…

Mwanzo ilifanya kuchelewa kutoka sababu kwa muda mrefu nilikuwa nasukumwa nitoe ila nikawa nagoma. Wazo lilikuwa la meneja wangu ila mimi nikawa nahisi bado sipo tayari kuachia EP. Unaachia EP wakati bado hata hujulikani. Ila meneja wangu alikuwa king’ang’anizi sana.

Kwa hivyo ndiye aliyekusukuma?

Ndio na bado pamoja na msukumo wake ilinichukua mwaka mzima kuja kuimalizia na kuiachia Aprili 2022.

Kipi kilikubadilisha mawazo?

Mimi na mamangu ndio tuliokuwa tunapinga sana ila ikafika wakati tukahisi ili niweze kupata shoo, ni muhimu niwe na nyimbo kadhaa.

Ila EP yenyewe mbona haina video, imekufaa?

Ndio sababu watu wamepata kunijua na kunisikia. Ingawaje video hazikutoka, EP imefanya vizuri sana kwenye Boomplay. Ila kwa sasa naendelea na mchakato wa kuzitolea nyimbo zote pale video.

Unahisi ni ngoma ipi iliyokutoa?

Nahisi kila ngoma niliyoitoa mpaka sasa imechangia mimi kutoka sababu kila wimbo una shabiki wake. Kwa hivyo kama kuna wale hawakuipenda Pambana, basi waliipenda Mazoea, au Akitokea na kama wapo walizozichukia, walipenda nyingine.

Kwenye gemu ya Pwani hivi unahisi unapata heshima unayostahili?

Heshima ni msumeno. Inakata mbele na nyuma. Mimi namheshimu kila msanii, najitahidi kufanya hivyo na nahisi watu pia wananiheshimu kwa kazi yangu.

Kwa msanii ambaye ndio mwanzo unaanza, changamoto zipi?

Mwanzo kabisa mimi sio msanii chipukizi, nimekuwepo kwenye gemu kwa zaidi ya mwaka sasa. Lakini kujibu swali lako, changamoto kubwa imekuwa ishu ya fedha. Mdhamini mkubwa wa muziki wangu ni mamangu. Ndiye anayesapoti muziki wangu na wakati mwingine inakuwa vigumu sababu anayo majukumu mengine vile vile.

Mamako ndio mdhamini?

Eeeh! Ndio CEO wa muziki wangu akisaidiana na meneja wangu Nelson Oroni.

Kando na suala la fedha?

Kupata shoo ni kibarua. Sio kwamba sipati shoo ila sio rahisi kuzipata. Mara nyingi panapokuwepo na shoo, huwa tayari kuna wasanii ambao wanakuwa wameshawekwa kwenye listi. Hawa ni wasanii ambao huwezi kuwakosa kwenye shoo zozote zinazoandaliwa huku. Kwa hilo, sisi wengine tunategemea bahati kupewa.

Je, katika kufanya kazi na wasanii wenzako mambo yakoje?

Kufanya kazi na wasanii wakubwa hasa wa kike sio rahisi. Hatupendani sana na pengine ndio sababu nimeishia kufanya kazi na wasanii wengi wa kiume sababu wao ni rahisi kuwafikia na mkaafikiana. Sio wasumbufu.

Sio wasumbufu hata kidogo, kwa hivyo wewe ufisi haujashuhudia?

Wapo wakusumbua, unawafuata mfanye kazi, wao wanajaribu kubadilisha upepo na kuanza kukuandama kwa mambo mengine tofauti kabisa.

Huwa unadili nao vipi?

Sipo kwenye gemu kusaka mapenzi kwa hivyo kama huna nia ya sisi kufanya kazi, basi najiondoa. Sio lazima. Suala lolote nje ya kazi, mimi simo, najitoa. Nipo hapa kusaka mpunga.

Je, ni dili zipi ambazo umefanikiwa kupata mpaka sasa?

Nimepata fursa nyingi na nafikiri ni kwa sababu mimi ni mwanamke ila wakati mwingi zile dili huwa sio nzuri. Huwa ni watu wanataka kunitumia na nimekuwa nikiachia zipite.

Mpaka sasa umejifunza nini?

Nimeshazoea watu kuniangusha. Huwa sikurupuki kufurahia jambo hata liwe zuri namna gani. Nimeshaahidiwa na watu wengi dili nyingi sana na mwisho wa siku wakakosa kutimiza. Hivyo huwa hainishtui tena mtu au mdhamini kuniahidi kitu. Huwa nasema kama ikitokea kheri na kama basi haiwezi pia sawa.

You can share this post!

KIKOLEZO: Cannes Festival ni hivi na hivyo!

Watu 12,000 wakwama penye vita Ukraine – UN

T L