• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
KIPWANI: ‘Naishi, nalala, nanywa muziki!’

KIPWANI: ‘Naishi, nalala, nanywa muziki!’

NA SINDA MATIKO

“HIDAYA, Hidaya, Hidaya, haki natafuta mwana hidaya… Haki nikikumbuka nikicheza naye ndombolo, haki nikikumbuka nikicheza naye lingala, haki nikikumbuka nikicheza naye chakacha, haki nikikumbuka nikicheza naye Kayamba…”

Hivi unaikumbuka hiti hii? Fataki moja nzito iliyoachiwa na Susumila miaka saba iliyopita kabla mzee baba hajaota kitambi, kabla Chikuzee hajajichubua ngozi. Mastaa hawa wawili kutoka Mombasa, walishirikiana na produsa mkali Hitmaker TK2. Leo mkekani nimeketi naye TK2.

Leo kama ukigombea udiwani, tutakayemlisha tiki ni Hitmaker TK2?

(Haha). Hapana, jina mtakalokutana nalo ni Musa Abdallah Kugotwah. Mimi ni produsa wa muziki lakini pia mwigizaji. Nimezaliwa, kulelewa na kukulia Mombasa.

Hitmaker TK2 lilikujaje sasa?

Hitmaker walinipachika wasanii niliowaandalia kazi na zikaishia kufanya vizuri kutokana na kile walichosema ni ubunifu wangu wa kubadilisha nyimbo za kawaida na kuzifanya hiti. TK2 maana yake ni wa pili, ambalo ni jina langu Kugotwah.

Mishemishe zako za muziki zilianza vipi na lini?

Muziki nilizaliwa nao. Toka utotoni nilipenda sana kujichanganya na makundi ya muziki na hata nyumbani na mpaka sasa hivi popote pale nilipo naishi nalala, nanywa muziki. Riziki yote yangu ipo kwenye muziki.

Kwa wengi wewe ni produsa, ila nahisi haiishi hapo?

Mimi pia ni mwigizaji, fundi mitambo (Sound engineer) lakini vile vile mjasiriamali.

Ulijikutaje kwenye uigizaji?

Muziki ndio ulinisukuma huko kwenye uigizaji. Nilianza kwa kupata tenda za kutengeneza ‘music scores’ (muziki unaotungwa kuendana na filamu) na pia kufanya ‘dialogue editings’ za filamu (usanifishaji wa sauti za waigizaji baada ya filamu kurekodiwa). Kisha fursa za kuigiza zikachipuka. Nimeigiza kwenye Maza kama mwanamitindo, Aziza kama produsa wa muziki na pia Kovu kama muigizaji (Roy Haze).

Kwa haraka nipe hiti zako tano zilizofanya vizuri sana toka umeanza muziki?

Ngoma itambae na Hidaya zote wahusika wakiwa ni Susumila na Chikuzee, Goodtime yake Masauti, Njoo yake Shoo Madjozi na Shekita yake CityBoy (Bawazir).

Mpaka leo utakuwa umeandaa nyimbo ngapi?

Duh! Kwa kweli sijui. Sina uhakika sababu nimeanza zamani shughuli hii. Inawezekana ni zaidi ya ngoma milioni sababu nimeanza kitambo na bado zipo zingine hata bado hazijatoka.

Tofauti na wasanii wengi wa Pwani ambao wamehamia Nairobi kusaka mtonyo zaidi, wewe umeamua kukomalia Mombasa. Kidogo upo tofauti…

Nafikiri ni vizuri tukiwa kila sehemu sababu riziki ipo kokote hata mimi ikitokea dili nzuri itakayonilazimu nihamie sehemu nyingine, sitasita.

Kama produsa, ni changamoto zipi unazopitia kwenye kazi hii?

Changamoto zipo kibao kwanza ishu ya mtaji. Mambo mengi hayaendi ikiwa mzunguko wa pesa sio mzuri. Kingine wawekezaji hawaonekani, unaweza ukawa una wazo nzuri ila ukakosa mdhamini wa kukusapoti hadi kulifanikisha. Ila kinachonivunja moyo na kunisikitisha kila siku ni kwamba sisi kama maprodusa wa muziki, siku zote hatupongezwi wala kuangaziwa kwa staha wakati ni sisi tumewajenga wasanii wengi mastaa. Wengine tuliwafua sisi, tukawatoa kutu kipindi wakiwa hawajulikani mpaka wakawa mastaa. Nafikiri tunahitaji na sisi kupewa heshima kama wao.

Umeanza zamani sanaa, ukirudi nyuma muziki wa Pwani umebadilika vipi?

Muziki kubadilika umebadilika maana kuna staili tofauti zilizoibuka kutoka jamii tofauti. Mitandao ya kijamii pia imekuwa na nguvu na imetoa nafasi kubwa kwa yeyote mwenye kipaji bila ubaguzi.

Kutokana na utandawazi huo, kama produsa nini kimebadilika kwenye utayarishaji wako wa nyimbo?

Kilichobadilika ni kuwa kazi zimefunguka kwa upana ukiachia mbali produsa kumsubiri msanii aje studio kurekodi ndio upate pesa. Leo hii produsa anaweza kupata hela kupitia mitandao kama TikTok, YouTube na Instagram kwa kuanika kazi zake kule.

Kuna baadhi ya watu wanahisi muziki wa Pwani umekwama? Hatuoni mastaa zaidi wakichipuka kama ilivyokuwa nyuma kidogo enzi za Nyota Ndogo, Fat S, Chikuzee na kadhalika?

Muziki upo mwingi sana na haujawahi kukwama na kama ni mastaa, wamekuja wengine wengi pia, wapo kibao wanajulikana. Playlist zimejaa vizuri, Jovial, Otile, Masauti, Kelechi Africana, mbona bado listi ni ndefu?

Kwa mtu kama wewe ambaye upo kwenye kila kona ya burudani, unaundaje hela zako?

Hela natengeneza kutokana na kudumisha uhusiano mwema na watu, washika dau na wateja waliopo kwenye tasnia.

Ni fani ipi unayoitegemea sana kukupa riziki, unayoiaminia haiwezi kukuangusha?

Kaka, fani zote zinaniweka mjini kila mti unazaa matunda yake na ninashukuru maisha yanasonga.

Wanasema muziki ni gharama, kwa mtu anayeanza atahitaji kuwa na kiasi gani cha pesa ili kurekodi wimbo na Hitmaker TK2?

Kwa sasa kwa msanii anayeanza akiwa na elfu ishirini, tunaweza fanya kazi ila waliobobea kiwango kitapanda.

Unaandaa nini sasa hivi?

Kazi nyingi bro, nataka kufanya kufuru, ninaachia albamu yangu hivi karibuni itakayobeba ngoma 30. Kwa hiyo nimebanika kaka.

Ni mtazamo upi hasi unaokukwaza kuhusiana na muziki wa Pwani?

Hiyo kasumba ya kuwa msanii wa Pwani hawezi kufanikiwa mpaka ahame Nairobi. Sio kweli. Ni uwongo huo!

Wakati haufanyi muziki?

Utanikuta nimetulia na familia yangu. Lakini pia napenda sana kusafiri, inasaidia kutuliza mawazo.

Baadaye mwana.

Safi kaka!

  • Tags

You can share this post!

Balala avunja kimya, aidhinisha Mung’aro kwa ugavana...

Msitumie Mumias Sugar kama chambo, wanasiasa waonywa

T L