• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MAKALA MAALUM: Wakazi Limuru katika njiapanda kuhusu Ukristo na dini za kiasili

MAKALA MAALUM: Wakazi Limuru katika njiapanda kuhusu Ukristo na dini za kiasili

Na MARY WANGARI

KWA wengi, mji wa Limuru ni sehemu tu ya Kaunti ya Kiambu ambayo ina baridi kali ya mzizimo inayoandamana na ukungu na rasharasha za barafu.

Lakini mji huo umesheheni mengi ambayo wengi hawayafahamu vyema, hasa kuhusiana na imani ya wakazi wa sehemu hiyo.

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, kumezuka wimbi jipya mjini humu linalojumuisha kundi la watu wanaopania kurejelea itikadi, tamaduni na mienendo ya jadi ya jamii ya Agikuyu.

Mjadala kuhusu wafuasi wa kundi hili wanaojiita ‘Kenda Muiyuru” kutokana na chimbuko la jamii ya Agikuyu, umeibua hisia kali, malumbano tata kiasi cha mgawanyiko mkubwa kabisa kutokea miongoni mwa wakazi wa mji huu.

Kuna wafuasi wa ‘mwamko mpya” wanaopigia debe jamii hiyo kurejelea utamaduni wao asilia, juhudi zinazopingwa vikali na upande unaoshikilia imani na mafunzo ya dini ya Kikristo.

Mjadala huu wenye utata vilevile umezua tumbojoto miongoni mwa wanaokumbatia usasa ambao wanashikilia kwamba, tamaduni za jadi hazina nafasi kamwe katika kizazi cha leo chenye maendeleo katika nyanja za mawasiliano, teknolojia, sayansi na dijitali.

Kwa upande mwingine, kuna wale ambao wamejipata katika njiapanda huku ghafla wakianza kutilia shaka ukweli na mafunzo ya kidini waliyolelewa nayo tangu utotoni mwao na kushindwa kuamua ama waendelee na imani waliyofunzwa au wageuke na kuanza kufuata utamaduni wao.

Lakini wimbi hili ni nini na linahusu nini hasa?

Kulingana na Ndeto Gitau, mzee wa Jamii ya Agikuyu, kinyume na madai ya wakosoaji wao kwamba wafuasi wa ngomi wanaabudu wafu, suala lote hili linahusu wanajamii wa Agikuyu kuheshimu chimbuko lao kupitia mababu zao waliowatangulia

“Ngomi ni mababu na mabibi wetu waliolala na kututangulia peponi. Hivyo basi, walilala kwa sababu walifanya kazi ya kutuzaa, kutulea na kutuachia mali ambayo huwa tunarithisha vizazi vyetu,” anaelezea.

Anafafanua kuwa mafunzo ya ‘ngomi almaarufu ‘kirira’ hayahusu kuabudu wafu au mashetani, bali kuheshimu mababu kupitia matambiko mbalimbali kama vile kulipa mahari na itikadi nyinginezo za jamii ya Agikuyu.

Kwa upande wake, Kiarie wa Ndung’u ambaye pia anashikilia mtazamo huo, mafunzo ya ngomi kamwe hayahusu kuabudu shetani bali yanahusu kutetea au kulinda ukweli tangu jadi wa jamii hiyo.

Anafafanua kauli yake kwa kuchambua neno “ngoma (umoja wa ngomi) ambalo ni “ngo” –ngao na ‘ma’ – ukweli.

Kuhusu madai kwamba mafunzo ya ngomi yanampinga Mungu, Kiarie anaeleza kuwa, jamii ya Agikuyu ilikuwa ikimwabudu Mungu na kumtolea dhabihu tangu jadi hata kabla ya wakoloni kuja na kuanzisha dini ya Kikristo.

“Mababu zetu walikuwa wakimwamini na kumwabudu Mungu “Mwenye Nyaga” tangu zamani waliyekuwa wakimtolea sadaka mbalimbali. Kila jamii ina itikadi na matambiko yake mahsusi. Matambiko yetu ndiyo yanayotutofautisha kama jamii ya Agikuyu na jamii nyinginezo,” anasema.

Roho za wafu

Waumini na viongozi wa dini ya Kikristo wakiongozwa na Pasta Yoo Hexeh wamepinga vikali mafunzo ya ngomi wanayodai yanahimiza kuabudu roho za wafu wakionya wakazi dhidi ya kujiunga nayo.

Pasta Hexeh ambaye ni mkazi wa eneo hilo anaonya dhidi ya kufuata mafunzo hayo ya kitamaduni akisema kwamba, wafuasi wake huenda wakajipata mashakani.

“Hizi ngomi zitawajia nyote mnazoziamsha. Mbona uunganishe nafsi yako na watu waliokufa ilhali kunaye ambaye hafariki kamwe? Kuna uhai baada ya kifo na vitendo vyetu vitatufuata,” anaonya mhubiri huyo,” anasema.

Hata hivyo, msomi na mtaalamu wa historia kuhusu masuala ya utamaduni wa Afrika, Kiiru Mugambi, anasema ni kinaya kwa Wakristo kupinga mafunzo ya utamaduni kwa misingi ya Biblia inayoashiria kwamba, kila mtu ana asili yake akidokeza kuwa mwacha mila ni mtumwa.

“Mathayo Sura ya Kwanza inazungumza kuhusu asili ya Yesu. Wewe pia una asili yako inayorudi nyuma kupitia mamilioni ya mababu zako. Ni kupitia urithishwaji huu ambapo jeni zako zitabebwa kwa watoto wako, wajukuu, vilembwe, vilembwekeza na kadhalika.” Anaendelea: “Huwezi ukatoroka asili ya mababu zako. Wakikuyu sawa na Wayahudi walikuwa wakimwomba Mungu wa mababu zetu (Ngai wa Maithe maitu). Sidhani wafuasi wa ngomi wanaabudu wafu.”

Isitoshe, anahoji sababu ya Ukristo kujikita katika madhehebu mbalimbali.

“Kwa nini Ukristo umejikoleza katika madhehebu tofauti ikiwa ulikuwa ni mzuri? Wakatoliki Roma walikusudiwa kuendeleza maslahi ya Waitaliano, wafuasi wa Anglicana maslahi ya Uingereza, PCEA maslahi ya Scotland, Lutehran maslahi ya Amerika na kadhalika. Mbona wasiwe pamoja, Kenya ina madhehebu zaidi ya 900, yote yanayohubiri injili ileile ila kwa ubinafsi,” anahoji.

Huku wafuasi wa ngomi wakizidi kuongezeka, wengi wao katika juhudi za kutafuta tiba ya matatizo yanayowazonga maishani, suala la itikadi kali limeibua wasiwasi na kuzidisha shaka kuhusu azma ya kundi hilo.

Ukeketaji wa kina mama hasa umeibua hasira na kupingwa vikali kwa usawa kati ya wake na waume eneo hilo.

Hii ni baada ya ripoti kadhaa kuhusu visa vya wanaume kuwalazimisha wake zao kutahirishwa pamoja na baadhi ya vijana waliodaiwa kuwalazimisha kina mama zao kutahirishwa.

“Huu ni ushetani kabisa. Jirani yangu majuzi katika kijiji cha Rwacumari alikubali mke wake atahirishwe. Alianza kumpikia bibi yake ili apone na kila mara watoto walipomuuliza, alikuwa akiwaambia eti mama yao ni mgonjwa,” alisema mkazi aliyechelea kutajwa.

Ajabu ni kuwa, idadi kubwa ya wanaojiunga na mafunzo ya ngomi ni vijana chiopukizi wasiofahamu vyema utamaduni asilia wa jamii hivyo na pengine katika juhudi za kutafuta ukweli, wanaishia kupotoka na kuwapotosha wenzao.

Baadhi wameashiria kuwa huenda kuna ajenda ya kisiasa inayolenga kuwagawanya wakazi wa Limuru kwa misingi ya kitamaduni na kidini, na iwapo hilo ndilo lengo, basi limefanikiwa vyema kufikia sasa.

“Kwa wale waliokuwepo enzi za utawala wa (Rais mstaafu) Moi, mnaweza kukumbuka makundi haramu ya Mungiki, Kamjesh na kadhalika. Siasa ni mchezo mchafu chochote chawezekana. Jinsi kundi hili lilivyokua kwa kasi, nimeachwa na maswali mengi

“Kuna mengi ya kuzingatia kabla ya kujiunga na makundi fulani. Wanasiasa ni walewale na hutumia ufukara na kukosa kujua kwa raia kujinufaisha. Kwa sasa, baraza la wazee wa Agikuyu limegawanyika na ndio wangekuwa wanapatia ruriri mwelekeo lakini kutokana na ulafi, wamekubali kutumiwa na wanasiasa,” anasema mzee Danny Mburu.

Huku Katiba ya Kenya ikiwa imemhakikishia kila mwananchi haki ya kuabudu na kujieleza, ni wakati tu utakaodhihirisha ukweli kuhusu mafunzo ya ngomi na nafasi yake katika historia ya jamii ya Agikuyu.

“Si rahisi kuamua hadi historia ya kweli itakapofichuliwa. Ukoloni haukufanyika kwa upole. Ulitekelezwa kwa ukatili, umwagikaji damu, vurugu, vitendo vya kinyama na dhuluma. Sehemu hii ya historia imefichwa kimaksudi ili watu wawe na hisia kama hizo dhidi ya asili zao wenyewe na nafsi zao,” anafafanua mwanahistoria Mugambi.

“Watu waache kukashifiana kuhusu dini. Ikiwa wewe ni Mkristo endelea kumwamini Mungu, ikiwa wewe ni wa Kenda Muihuru, endelea kuamini Ngomi. Wakati umewadia kwa kila mtu kuheshimu uamuzi wa mwenzake,” anasema Mzee Gitau.

[email protected]

You can share this post!

Covid-19: UN yarai mataifa kuanza kufungua shule zao

TAHARIRI: Tuchague viongozi kwa msingi wa sera