• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
MALENGA WA WIKI: Walibora aendelea kukumbukwa kwa mchango wake muhimu kukuza Kiswahili

MALENGA WA WIKI: Walibora aendelea kukumbukwa kwa mchango wake muhimu kukuza Kiswahili

Na HASSAN MUCHAI

JUMAMOSI, ilikuwa siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha mwandishi nguli Ken Waliaula maarufu kama Ken Walibora kutokea.

Ripoti za awali kutoka kwa maafisa wa usalama zilionyesha kuwa Ken alifariki kutokana na ajali ya barabarani eneo la Landhies jijini Nairobi.

Maiti ya Ken ilitambuliwa siku tano baadaye katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali Kuu ya Kenyatta. Kabla ya maiti kupatikana, Ken alikuwa ametangazwa kupotea.

Kifo chake kiliwapata Wakenya na ulimwengu kwa jumla kwa simanzi kuu na hali ya kutoamini. Viongozi mashuhuri nchini akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake na viongozi wengine wa ngazi za juu walituma risala zao wakielezea kusikitishwa sana na mauti hayo.

Kabla ya kufariki, Ken alikua amejizolea sifa kedekede kutokana na kazi zake za uandishi wa vitabu, uanahabari na spoti. Alikuwa msomi wa kujitegemea aliyeipigania nafsi yake kuendeleza masomo yake hadi mataifa ya kigeni ili kukivumisha Kiswahili.

Sherehe za Jumamosi zilitarajiwa kuwa za kipekee na sawia na siku ya mazishi yake, taifa halikuweza kuadhimisha kumbukumbu za kifo chake kwa njia za watu kukutana na kufanya sherehe kutokana na hofu ya msambao wa virusi vya corona ambavyo vimeendelea kuhangaisha mataifa mengi ulimwenguni.

Badala yake, wakereketwa wa lugha ya Kiswahili na wapenzi wake Ken waliandaa makongamano ya mitandaoni. Wengine hata waliungana kupitia makundi ya WhatsApp kutunga mashairi ya kuliwaza na kumsifu Ken kutokana na kazi nzuri aliyoiacha duniani kabla ya mauti yake kutokea.

Mmoja wa waandalizi wa makongamano haya ni Bi Phibian Muthama ambaye kupitia kikundi chake cha The Writers Guild alikuwa ameandaa kikao maalum kuanzia saa kumi jioni hadi saa moja usiku au kuelekea saa mbili. Kikao chake kilichowashirikisha wasomi wa juu katika nyanja ya lugha ya Kiswahili kiliwahusisha Dkt Mosol Kandagor, Bi Aida Mutenyo, Prof F.E.M.K Senkoro na Abdilatif Abdallah.

Waratibu wake walikuwa Bi Muthama, Prof Leonard Muaka na Bi Kawthar Iss-hack. Kipindi kiliwapa fursa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kutunga, kughani au kukariri mashairi yao moja kwa moja kwa njia wanayoifahamu na kuienzi wao wenyewe.

Lau si janga la corona, kijiji cha Bonde kilichoko eneo la Makutano ya Ngozi , Cherangany katika Kaunti ya Trans Nzoia, kingefurika mashabiki wa Ken kutoka pembe zote za Afrika Mashariki.

Kabla ya Rais Kenyatta kutoa masharti mapya ya kufungwa kwa kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru, mipango ya kufika Cherangany ilikuwa ikiendelea. Aidha kusitishwa kwa shughuli zozote zinazohusiana na watu wengi kukutana pamoja kwa shughuli za ibada, mazishi , sherehe au mikutano ya aina yoyote ikiwemo siasa, kuliharibu kabisa mipango ya wapenzi wa Ken.

Kwa mujibu wa Kaka yake, Bw Patrick Lumumba, familia ilitaka sana kuwaalika wageni nyumbani lakini ikalazimika kukatiza sherehe yoyote ambayo ingeenda kinyume na agizo la Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Lumumba alisema wako tayari kuwakaribisha wageni pindi serikali itakapolegeza masharti yake na wakati ugonjwa huu utakuwa umethibitiwa jinsi ipasavyo.

“Mahali alipozikwa Ken pamekuwa kama makavazi, ni kama mnara. Wageni wamekuwa wakija hapa kuona alikozikwa Ken, wengine kupigwa picha kufanya utafiti wao. Wengine ni wanahabari wanaotaka kuandika habari zao. Natumai tutakuwa na shughuli chungu nzima siku za usoni kwani tumekuwa tukipokea maombi mengi kutoka kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kuzuru hapa,”’ Bw Lumumba alieleza.

Kwa sasa, Ken hayuko nasi lakini mbegu aliyoipanda imechipuka na kuzaa mavuno. Kaunti ya Trans Nzoia na Bungoma alikotoka Ken zimekuwa chimbuko la waandishi mashuhuri wa habari na fani nyinginezo za usanii.

Mungu azidi kuilaza roho yake mahali pema penye waja wema. Amen.

You can share this post!

Raila awindwa na Uhuru, Ruto

DINI: Dunia hii ina mitihani mingi, usitamauke, mtafute...