• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2024 12:24 AM
Maskwota wataka mahakama ibatilishe kutimuliwa kwao

Maskwota wataka mahakama ibatilishe kutimuliwa kwao

NA RICHARD MUNGUTI

MASKWOTA wapatao 10,000 wamewasilisha upya kesi katika Mahakama ya Upeo wakiomba ibatilishe uamuzi kwamba wafukuzwe kutoka kwa shamba la ukubwa wa ekari 25,000 wanalong’ang’ania umiliki wake na familia ya mwanasiasa marehemu Mark Too.

Maskwota hao wanaodai mababu zao ndio waliotimuliwa kutoka kwa shamba hilo enzi za ukoloni, wanasema walipewa shamba hilo rasmi na aliyekuwa Rais hayati Daniel arap Moi, kisha Kamishna wa Ardhi M Okundu akaratibisha uamuzi huo mwaka 2007.

Katika ombi lililowasilishwa na wakili William Arusei chini ya sheria za dharura, kikundi cha maskwota hao–Sirikiwa Squatters Group–kimeomba mahakama ibatilishe uamuzi huo kwa vile ilitegemea ushahidi ambao haukuwa umewasilishwa katika kesi waliyoshtaki katika Mahakama ya kuamua kesi za mashamba (ELC), Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Pia wameeleza bayana Jaji Mkuu Martha Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaack Lenaola, na William Ouko walitegemea ushahidi wa Afisa wa Ugavi wa Mashamba R J Simiyu kutoa uamuzi wang’atuke shambani.

Maskwota hao wamesema ushahidi wa Bw Simiyu uliowasilishwa mbele majaji hao saba kwa njia ya afidaviti ni mpya na kamwe “haukuwasilishwa mbele ya Jaji Antony Ombwayo aliposikiliza na kuamua kesi hiyo 2017.”

Pia wanasema ushahidi huo haukuwasilishwa Mahakama ya Rufaa iliyosikiliza rufaa iliyowasilishwa na kampuni ya Fanikiwa, familia ya marehemu Mark Too, kampuni ya Lonrho Agribusiness (EA) Ltd, na Bw David K Korir.

Hivyo basi, maskwota hao wanaeleza mahakama hii ya upeo kwamba ni kinyume cha sheria kutegemea ushahidi mpya kutoa uamuzi wa kesi hii iliyo na umuhimu mkubwa kwa umma.

“Uamuzi huu wa Mahakama ya Juu wa Desemba 15, 2023, hauna mashiko kisheria na kamwe hauna nguvu kisheria kuwatimua maskwota hawa kutoka kwa shamba lao,” asema Bw Arusei.

Pia maskwota hawa wanadai kwamba badala ya Mahakama ya Juu kujadili masuala ya kikatiba jinsi ilivyo jukumu lake, majaji hao walianza kufafanua na kutafsiri ushahidi wa watu binafsi na kuelezea maana ya ‘skwota’.

Mahakama hii imeombwa ikague upya uamuzi iliyotoa kwa vile ilidanganywa na walalamishi na pia kutendewa ujanja.

Akinukuu maamuzi ya majaji wastahiki kama vile Lord Dening, Bw Arusei amesema, mahakama ikigundua ilipotoshwa au kudanganywa na upande mmoja, iko na mamlaka na uwezo wa kufutilia mbali uamuzi iliyotoa na kuandika mwingine.

Maskwota hao wanaomba Mahakama ya Juu iwarudishe shambani kama ilivyokuwa imeamuliwa na Jaji Ombwayo na Mahakama ya Rufaa.

Vile vile mahakama hiyo imekosolewa kwa kumshambulia hayati Moi katika uamuzi huo pasi kutoa agizo wasimamizi wa mali yake wafike mbele yao kutoa mwanga kuhusu suala la umiliki wa shamba hili lililorudishwa kwa serikali na kampuni iliyokuwa inakuza miti inayotumika katika viwanda vya ngozi.

Naibu msajili wa Mahakama ya Juu Nelly Kariuki aliwaamuru maskwota hao wawakabidhi nakala za kesi hii yao mpya wahusika wote kabla ya Januari 31, 2024, kesi itakapotajwa tena kwa maagizo zaidi.

Jaji aliyesikiliza kesi hii mpya hakuiratibisha kuwa ya dharura ila aliamuru pande zote ziwasilishe ushahidi katika muda wa siku 14 kuanzia Desemba 21, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Wezi wavunja nyumba za walioenda mashambani kuenjoi

Kero ya rundo la taka sokoni Mamboleo

T L