• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
MAUYA OMAUYA: Amri ya kafyu imegeuka soko la rushwa

MAUYA OMAUYA: Amri ya kafyu imegeuka soko la rushwa

Na MAUYA OMAUYA

JUMAPILI iliyopita, binamu wangu anayeishi mjini Nakuru alinipigia simu kunieleza amesafiri hadi Nyamira kuwasalimu kina yakhe.

Nilishangaa kwa sababu Nakuru ni miongoni mwa majimbo yaliyofungwa ili kuzuia usambazaji wa virusi vya corona – vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Nilimhoji kutaka kufahamu iwapo ziara yake ilikuwa ya dharura lakini aliniambia zii. Tukaanza kupiga gumzo aniarifu iweje amefaulu kukaidi amri ya serikali.

Niliwaza pengine kwa kutumia gari la kibinafsi alisubiri giza; wakati walinzi wamezembea barabarani kisha apenyeze msituni na kuingia Kericho kabla kufululiza hadi Nyamira.

Aliniambia La! Alichukua mkoba wake, akaenda kwenye kituo cha magari ya umma mjini Nakuru na kuabiri matatu ya kawaida akiwa na wasafiri wengine. Isitoshe, walisafiri mchana peupe kupitia barabara kuu ya kuelekea Kericho.

Hata hivyo, aliniambia kuwa nauli ilikuwa imepanda kutoka Sh800 hadi Sh1,200; akidokeza kwamba hizo Sh400 za ziada hutolewa kwa polisi katika vizuizi vya barabarani ili waruhusu safari kinyume cha amri.

Ina maana kuwa kwa kila gari la abiria saba, Sh2,800 hutolewa kama hongo kwa ajili ya kukaidi amri iliyowekwa kwa minajili ya afya ya umma. Yamkini kwa siku basi polisi hao kwenye vizuizi wanavuna kitita si haba.

Hali hii hujirudia giza linapoingia mijini na amri ya kafyu kuanza kutekelezwa. Raia wengi wanaojipata wamebanwa huwa hawana budi ila kutoa hongo kujinusuru makali ya seli au faini kubwa.

Ninafahamu ni rahisi kurusha cheche za lawama kwa walinda usalama. Hata hivyo, wakati umefika tuambiane ukweli kwamba kafyu imefeli, na amri ya Rais kuzima usafiri haizai matunda. Mtoa rushwa na mpokeaji, yao ni mamoja tu.

Rushwa ni kansa kwa taifa lolote sababu inavuruga utendakazi na kuchochea ukiukaji wa sheria.

Inaatua moyo kuona kwamba kampuni za magari na maafisa wa polisi wameafikia kiwango rasmi cha rushwa kutoka kwa kila abiria. Je, Sh400 ndio bei ya kuruhusu usambazaji wa corona?

Ni Wakenya wao hao wanaotoa rushwa utawapata wanakejeli majirani zetu Watanzania eti hawana mikakati ya kukabiliana na janga hili la corona.

Nikitazama jinsi Wakenya wanavyotangamana sokoni, mazishini na kwenye magari, ninaamini amri ya Rais haina maana sasa.

Hiyo kafyu ya usiku haifai kwani gonjwa hili linasambazwa zaidi wakati wa mchana wananchi wakiwa katika pilkapilka za kuchuma riziki.

Taifa maskini kama Kenya haliwezi kuzingatia kwa kina amri hiyo; wananchi watakiuka, upende usipende. Kwa sasa njia ya pekee kukabili corona ni kuhakikisha Wakenya wengi zaidi wanapata chanjo.

Ikiwa Wakenya hawawezi kutii, sioni haja ya Rais Uhuru Kenyatta kujitia hamnazo. Linalofaa ni kupunguza vikwazo na kuelekeza juhudi katika utoaji chanjo.

Ilivyo sasa, kafyu na marufuku ya kutosafiri zimegeuzwa kitega uchumi kupitia rushwa.

Jinamizi hili la ufisadi limekita akilini mwa wananchi na polisi, na linazidi kukwamisha ustawi wa taifa.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Uchaguzi ujao utumiwe kulainisha siasa zetu

BENSON MATHEKA: Serikali itimize onyo la wataalamu kuhusu...