• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
MITAMBO: Kifaa cha jab planter kupunguza gharama za shughuli za upanzi

MITAMBO: Kifaa cha jab planter kupunguza gharama za shughuli za upanzi

NA RICHARD MAOSI

KUNA changamoto nyingi zinazowakumba wakulima wa mahindi, wengi wao wakishindwa kubaini idadi kamili ya mbegu ambazo zinahitajika katika kila shimo na kiasi cha mbolea.

Hata hivyo, hili huenda likawa rahisi wakulima wakipata mwongozo sahihi, unaozingatia mafunzo ya kufuata katika kila hatua.

Hii ndio sababu shirika la Agricultural Technology Development Centre (ATDC), kwa ushirikiano na wakulima wadogo wameamua kuboresha kifaa cha planter na kuvumbua Jab Planter.

Kifaa cha jab planter kwa kawaida kinaweza kubeba mbegu na mbolea kwa wakati mmoja na mkulima anaweza akakitumia akiwa amesimama bila kuinama sana wala kupata maumivu ya mgongo.

Ingawaje kuna baadhi ya wakulima ambao wamejitengenezea kifaa cha planter kwa matumizi ya nyumbani, jab planter imeboreshwa ili kuzingatia usahihi wa idadi ya mbegu na mbolea wakati wa kupanda.

Na sio tu kupanda bali pia kifaa chenyewe kinaweza kufukia mbegu udongoni ishara tosha kuwa hii ni njia mojawapo ya kuendeleza kilimo kinachosaidia pia kuhifadhi mazingira.

Nancy Macharia ambaye ni mhandisi wa kilimo kutoka Shirika la ATDC Nakuru anasema tayari jab planter inatumika katika maeneo mengi nchini, kuwafaa wakulima wadogo ambao wamekuwa wakitumia gharama nyingi kuajiri vibarua wakati wa kupanda au kuweka mbolea shambani.

Bi Nancy Macharia mhandisi wa Agricultural Technology Development Centre akionyesha jinsi ya kutumia mtambo wa jab planter ambao hutoa maelezo sahihi ya kupanda na kufukia mbegu. PICHA | RICHARD MAOSI

Anasisitiza kuwa uvumbuzi kama huu utawafanya vijana wengi ambao hawana ajira kukumbatia kilimo kwa mikono miwili kutokana na utashi wa chombo chenyewe.

“Hii ni kwa sababu ni vigumu sana siku hizi kuwashawishi vijana kulichukua jembe la kawaida kwenda shambani, ingawa wanaweza kubadili mtazamo wa kilimo endapo kitaendeshwa kidijitali,” anasema.

Anaeleza kuwa matumizi ya kifaa hiki huwa ni mepesi ambapo kimtazamo na matumizi yake huwa kimegawika katika sehemu mbili, sehemu moja huchukua mbegu na ile ya pili ikibeba mbolea.

“Katika sehemu ya juu karibu na anaposhikilia mkulima kuna sehemu wazi ambapo kuna mikondo kama paipu, iliyogawika sehemu mbili. Hapa mbolea na mbegu hujazwa,kisha zikatokea katika sehemu ya chini mkulima anaposukuma jab planter ardhini,” asema, huku pia akielezea kuwa kifaa cha jab planter kina uwezo wa kufukia mbegu ardhini.

Kulingana naye, kifaa hiki mara nyingi hutumika msimu wa kiangazi wakati ambapo wakulima wengi huwa wanasubiri msimu wa mvua kurejea.

“Mkulima anaweza kuendesha shughuli zake huku akisubiri wakati mwafaka wa kuandaa shamba lake, na pia ndege hawawezi kutambua sehemu ambapo mbegu zitakuwa zimefukiwa,” anaeleza.

Vile vile, anafichulia Akilimali kuwa kifaa cha jab planter kinaweza kupanda kila aina ya nafaka kama vile pojo, maharagwe, mahindi mtama na shayiri, kwa gharama nafuuna mazao yake huwa ni tele.

Pili, anasema kutokana na uwezo wa jab planter kupenya katika kila sehemu, kifaa hiki kinaweza kutumika katika maeneo kame ambayo hushuhudia kiwango kidogo cha mvua na ardhi yake huwa imejaa mawe.

Bi Macharia anashauri kuwa mkulima hawezi kuweka mbolea na nafaka katika mkondo mmoja ndani ya kifaa hiki, ikizingatiwa kuwa wakulima wengi wamekuwa wakitumia mtindo huo wakati wa kupanda.

“Kuna uwezekano mkubwa wa zaidi ya asilimia 95 ya mbegu za mkulima kuota kwa wakati unaofaa, ikizingatiwa kuwa mkulima anaweza kutekeleza upanzi katika kipande cha ardhi cha ekari nne kwa siku,” anaongeza.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: IEBC iepuke mapungufu yaliyoandama uchaguzi...

Wanavikapu wa Morans warejea nyumbani mikono mitupu

T L