• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
MUTUA: Hivi tunaweza kujilisha au tunaringa bure tu?

MUTUA: Hivi tunaweza kujilisha au tunaringa bure tu?

Na DOUGLAS MUTUA

“HIVI Kenya inaringia nini ilhali haiwezi hata kujilisha?” Ameandika hayo hivi majuzi mmoja wa marafiki zangu wa kufa kuzikana, raia wa nchi jirani.

Alipandwa na hasira pale Kenya ilipopiga marufuku mahindi kutoka Uganda na Tanzania.

Kenya ilisema utafiti unaonyesha mahindi kutoka mataifa hayo huwa na sumu inayotokana na kukaushwa kwa njia isiyofaa.

Pia ilidai kuwa Wakenya wamewahi kufariki baada ya kula mahindi hayo, hivyo kwetu sisi Wakenya hilo ni suala la afya, si biashara tena.

Rafiki yangu pia aliteta kwamba mwaka jana Kenya ilipiga marufuku uingizaji wa kuku, mayai na nyama kutoka mataifa hayo mawili, sikwambii alisema tuna kiburi sana!

Waganda na Watanzania wanaona tu biashara, yaani kule kutiliwa kitumbua mchanga kikawa hakiliki tena, na anayekitia ana njaa na hataki kulishwa.

Ningekuwa Mtanzania au Mganda ningepandwa na hasira kutokana na marufuku hizo. Hakuna anayefurahi nchi yake ikidharauliwa au kuonewa kiuchumi. Ni suala la uzalendo, bila kwanza kujiuliza marufuku yenyewe inafaa au la.

Hata hivyo, ni sharti tukubaliane kwamba Kenya haina jukumu la kuzikuza chumi za majirani zake; jukumu lake kuu ni kuwakinga raia wake dhidi ya madhara yoyote yale.

Ikiwa madhara yatatoka kwa majirani au hata ng’ambo ya pili ya bahari, Kenya ina jukumu la kuyazuia kabisa yasitue kwetu. Huko ndiko kujitambua na kujithamini.

Kelele za majirani wanaosema tunahujumu chumi zao ni dua ya kuku isiyompata mwewe kwa vyovyote vile. Huwezi kula sumu kipumbavu ili mtu atie donge kibindoni. Utakufa!

Hata hivyo, hebu tuambizane kidogo: inawezekana chakula kikatumika kama silaha katika vita vya kidiplomasia au hata siasa? Labda.

Je, unakumbuka ule mvutano kati ya Kenya na Tanzania kuhusiana na janga la corona hapo mwaka jana?

Kenya ilipofunga mipaka yake, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania aliwaagiza wakulima wa Tanzania wasiiuzie maharagwe, vitunguu, tangawizi na viungo vinginevyo.

Agizo hilo lilinuiwa kutumia bidhaa husika kama silaha ya kututia adabu ili tukizikosa tuwaruhusu wagonjwa waingie na kutoka nchini mwetu wajitakiavyo bila tahadhari yoyote.

Tukijichungua wenyewe hapa nchini, tunakumbuka miaka kadhaa iliyopita jinsi mawakala wa kuuza nafaka walivyolidhibiti soko kiasi cha kuweza kuamua vilikavyo na visivyolika.

Upo wakati ambapo kila maeneo makavu kama Ukambani na Kaskazini Mashariki yalipovuna mahindi kwa wingi, wataalamu walizuka na kudai yalikuwa na sumu.

Matokeo yalikuwa wakulima wa maeneo hayo kutoruhusiwa kuuza mazao yao kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPD) hivyo kuondoa ushindani.

Mahindi yaliyodaiwa kuwa sumu yaliharibiwa mara kadhaa, wakulima waliojizatiti kujilisha na kuunda pesa wakawa wa kulishwa kwa chakula cha msaada.

Hujuma hiyo ilitokea mara kadhaa ndipo viongozi wa maeneo yaliyonyanyaswa wakalalamika na kuwashauri wenyeji wasiyaharibu mazao yao, wayale bila wasiwasi.

Ikiwa mahindi kutoka nje yana matatizo, suluhisho si kuyapiga marufuku kabisa bali kuweka masharti yatakayohakikisha yako salama yakiingia ndani ya mipaka yetu.

Si siri kwamba sehemu kubwa ya nchi yetu ni kame, hivyo hatuwezi kujikimu kikamilifu kwa chakula. Lazima tununue chakula nje, na ni heri tununue kwa majirani zetu.

Hatuhitaji kugharamika pakubwa kwa kuagiza mahindi kutoka mataifa ya mbali kama vile Mexico ilhali majirani wakituuzia yatatufikia baada ya siku chache na kwa bei nafuu.

Ikiwa madhumuni ya marufuku ni kuwakinga wakulima wetu dhidi ya ushindani, basi tuambiwe waziwazi ili tafute uga mwingine wa kushindania kama vile teknolojia au umeme.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Klabu za ‘kikabila’ zitastawisha soka

KAMAU: Serikali isaidie HELB kutoa mikopo upesi kwa...