• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Kusaidia masikini kusiwe tu wakati wa Ramadhani

NASAHA ZA RAMADHAN: Kusaidia masikini kusiwe tu wakati wa Ramadhani

Na NUR SAID

RAMADHANI ndio mwezi ambao mayatima hulishwa sana na kuvishwa.

Waislamu wengi hutia sadaka zao ndani ya Ramadhani. Watu hufuturisha zaidi wale waliofungwa na kutoa zaka ya kutokana na mali pamoja na ile ya fitri.

Mtu anaweza kuuliza ni nini tofauti kati ya zaka hizi mbili? Zakatul Fitr ni zaka inayotolewa mwisho wa mfungo wa Ramadhani na huwa kilo mbili na robo za chakula kinacholiwa katika eneo inakotolewa. Nayo Zakatul maal hutolewa kutokana na mali iliyotimiwa mwaka.

Na hapa hutolewa pesa, dhahabu, mazao, wanyama anaowafuga na kadhalika.

Inapokuja katika suala la kuwasaidia mayatima na masikini, Mwenyezi Mungu (SWT) anasema, “Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa punje moja ya mahindi iliotoa mashuke saba, ikawa katika kila shuke pana punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye zaidi (kuliko hivi) Na Mwenyeezi ni mwenye wasaa mkubwa (na) mwenye kujua.’’ – Al Baqara 261.

Angalia namna Mungu anavyomlipa mwenye kutoa kwa ajili yake kuwasaidia wasiojiweza. Na aya hii yazungumzia wakati wowote si katika mwezi wa Ramadhani peke yake. Pia ametaja katika sura Muzammil kwamba “…Chochote unachokitoa (Kuwasaidia watu) basi utaipata mbele ya Mwenyeezi Mungu siku ya qiyama..” Hivyo basi unapojitahidi kuwasaidia wasiojiweza, usifanye tu katika mwezi wa Ramadhani bali endeleza na katika miezi mingine.

Ramadhani itakuja na kuenda zake bali msaada wako kwa waja wa Mwenyeezi Mungu hauishi; inahitajika iwepo kila wakati ilimradi na wewe upate msamaha na neema za Mwenyeezi Mungu. Mtume (SAW) amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wasiojiweza na akawahimiza maswahaba zake nao wafanye hivyo.

Sayyidna Abubakar alikuwa akitoa kuliko maswahaba wengine wote hadi Umar (R. anhu) akawa anamuonea wivu kwa uzuri. Maana kutoa kwa ajili ya mwenyeezi Mungu ilikuwa mashindano. Lini wewe mwisho ulishindana katika kuwasaidia wasiojiweza? Tujitahidi waumini wenzangu.

You can share this post!

KCSE: Matokeo kutolewa Mei

Polisi aliyeua Floyd hatarini kusukumwa jela miaka 40