• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
NDIVYO SIVYO: Tofauti katika matumizi ya vikanushi ‘hau’ na ‘hu’

NDIVYO SIVYO: Tofauti katika matumizi ya vikanushi ‘hau’ na ‘hu’

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA makala haya nitapambanua tofauti iliyopo baina ya vikanushi vya hali ‘hau’ na‘hu’.

‘Hau’ hutumiwa kukanusha nomino ambazo hazina uhai na hisia. Neno hisia au hisi ni muhimu sana katika maelezo haya.

Sababu ni kuwa baadhi ya watu huenda wakasema kuwa mimea pia ni viumbe vyenye uhai. Hata hivyo, swali ni iwapo mti unaweza kuongozwa na hisia kama zile zinazomwongoza binadamu na baadhi ya wanyama.

Hu hutumiwa kukanusha nafsi ya pili umoja. Kwa nini nafsi ya pili umoja? Kwa mfano, kwa nini kauli mbili zifuatazo:‘Wewe haukuchelewa’ na ‘Wewe hukuchelewa’ zisichukuliwe kuwa sahihi? Pengine swali kama hili limechochewa na baadhi ya wanasarufi ambao katika kazi zao wanaeleza kwamba matumizi ya ‘hau’ au ‘hu’ kurejelea nafsi ya pili umoja ni mamoja. Kabla ya kulijibu swali hilo na kuthibitisha iwapo madai ya wanasarufi hao ni ya kweli au la, tutayachunguza baadhi ya maneno yaliyotumia ‘hu’ na nafasi ya (hu) katika maneno yenyewe.

‘Hu’ hutumiwa kama kiwakilishi cha hali ya mazoea. Huonyesha kuwa kitendo kinachorejelewa hutendeka aghalabu au hufuata masharti fulani. Mathalan; Wakati wa kiangazi, mti hukauka. Sentensi hii imetumia ‘hu’ kuonyesha masharti ya aina fulani. Kukauka kwa mti hutokana na kuwepo kwa kiangazi. Hata hivyo, sentensi yenyewe ni tofauti na,‘Mwanadamu hufa’ ambayo inaonyesha desturi fulani.

Ni vyema kuzingatia kuwa, ‘hu’ iliyotumiwa katika sentensi ya kwanza, katika hali ya kuyakinisha,haina uhusiano wowote na vikanushi ‘hu’ na ‘hau’ ambavyo nimedhamiria kuvijadili baadaye.

Hata hivyo, iwapo tutaikanusha sentensi hiyo ifuatavyo: Wakati wa kiangazi,mti haukauki, basi uhusiano huo utajitokeza.

Katika sentensi, ‘Mti wenyewe huenda ukakauka kutokana na kiangazi’, ‘hu’ katika neno ‘huenda’ inaleta dhana ya kutokuwa na hakika au hali ya kukisia tu. Ni kawaida kwa neno hilo kutumiwa hivyo kuonyesha hali ya kutokuwa na hakika kuhusu jambo linalorejelewa. Sentensi nyingine zilizolitumia hivyo ni pamoja na: Mradi huu, huenda ukatufaa sana; Mwanafunzi huyu huenda akaadhibiwa kwa kudanganya kwenye mtihani miongoni mwa nyingine. Katika kuzikanusha sentensi tulizozitaja, neno lenyewe haliathiriwi kwa vyovyote na badala yake,kitenzi au vitenzi vinavyolifuata ndivyo huathirika. Hebu tukanushe mfano wa kwanza kuthibitisha maelezo haya: Mti wenyewe huenda usikauke kutokana na kiangazi. Kwa mara nyingine, ni muhimu kuzingatia kuwa kujitokeza kwa ‘hu’ katika sentensi hizi mbili hakuna uhusiano wowote na vikanushi viwili tulivyokwisha kuvitaja.

Hau hutumiwa kukanusha sentensi zilizotumia viumbe visivyokuwa na uhai. Mfano, ukanushi wa ‘Mti umekauka’ ni ‘Mti haujakauka bali si ‘Mti hujakauka’.

Hu hutumiwa kukanusha sentensi zilizo katika nafsi ya pili umoja. Kwa mfano, ukanushi wa “Wewe umejitahidi” ni “Wewe hujajitahidi bali si “haujajitahidi’’!

You can share this post!

NGILA: Kamera za kidijitali zitapiga vita ujangili, ukataji...

KINA CHA FIKRA: Kuteka watoto nyara ni unyama na hatari kwa...