• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:28 AM
KAMAU: Ni kosa kuwabagua wananchi kwa misingi ya tabaka

KAMAU: Ni kosa kuwabagua wananchi kwa misingi ya tabaka

Na WANDERI KAMAU

KUNA kauli maarufu kwamba huwa ni vigumu kwa watu maskini kupata haki.

Dhana kama hiyo ndizo zimeifanya serikali kuanza mikakati kabambe kutekeleza mageuzi katika Idara ya Mahakama.

Licha ya juhudi hizo, bado kuna pengo kubwa katika kuhakikisha kuwa watu wa tabaka la chini wanapata haki kutokana na dhuluma zilizowakumba.

Hali hii imeibuliwa na mahangaiko yanayoikumba familia ya wakili Willie Kimani, aliyeuawa kikatili mnamo 2016.

Hadi sasa, familia hiyo imekuwa ikilalamika kuhusu kuchelewa kwa mchakato wa kubaini kile kilichosababisha kifo chake.

Bila kuingilia taratibu za mahakama, kilio cha familia hiyo kimeibua matukio ya awali, ambapo juhudi za kubaini vifo vya baadhi ya watu nchini zimegonga mwamba katika hali tatanishi.

Miongoni mwa watu hao ni aliyekuwa mbunge wa Nyandarua Kaskazini, JM Kariuki, mwanasiasa Tom Mboya, Dkt Robert Ouko, wanaharakati Pio Gama Pinto, Oscar King’ara kati ya wengine.

Simulizi ya mauaji ya JM ni ndefu. Ingawa mauaji yake yalifanyika katika miaka ya sabini, hakuna jibu lililopatikana hadi sasa kuhusu yule ama wale ambao walihusika.

Mwili wa mwanasiasa huyo ulipatikana ukiwa umetupwa katika msitu wa Ngong’, na mchungaji wa Kimaasai ukiwa umechomwa vibaya kwa asidi.

Kabla ya kupatikana kwake, serikali ya Mzee Jomo Kenyatta ilisema alikuwa ameondoka nchini kuelekea nchini Zambia.

Baada ya shinikizo kali kutoka kwa umma na mashirika ya kutetea haki za binadamu, serikali ilibuni jopo maalum la uchunguzi lililoongozwa na Bw Elijah Mwangale, aliyekuwa mbunge wa eneo la Kimilili.

Licha ya jopo hilo kuwasilisha ripoti yake Bungeni na kuwataja baadhi ya viongozi maarufu waliodaiwa kuhusika—hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yao.

Hadi sasa, familia ya marehemu imekuwa ikililia haki hadi leo.

Mkwamo huo ndio unawaandama watu wengine waliojipata katika hali kama hizo.

Maswali yanayoibuka ni: Ni lini taratibu za kutafuta haki zitaendeshwa bila kuwabagua wananchi kwa misingi ya tabaka lao? Je, mageuzi ya mahakama ni ahadi tu zisizotimia? Ni nani atawaokoa Wakenya ikizingatiwa serikali inaonekana kushindwa?

Kimsingi, ni vibaya wakati kesi inaendeshwa kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata mwelekeo ufaao huku nyingine zikikamilika kwa miezi ama hata wiki kadhaa pekee.

Lazima taratibu za kisheria zihakikishe kuwa pana usawa kwa wananchi wote bila ubaguzi wala mapendeleo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: TSC sasa iheshimu uongozi wa KNUT

Yafichuka Messi ana mipango ya kuyoyomea Amerika baada ya...