• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Yafichuka Messi ana mipango ya kuyoyomea Amerika baada ya Kombe la Dunia 2022 kisha kurejea Barcelona kuwa kocha

Yafichuka Messi ana mipango ya kuyoyomea Amerika baada ya Kombe la Dunia 2022 kisha kurejea Barcelona kuwa kocha

Na MASHIRIKA

BARCELONA wameimarisha juhudi za kushawishi nyota Lionel Messi kutia saini mkataba mpya kabla ya kandarasi yake ya sasa uwanjani Camp Nou kutamatika mnamo Julai 1, 2021.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Joan Laporta ambaye ni rais mpya wa Barcelona ni kushuhudia Messi akirefusha kipindi cha kuhudumu kwake ugani Camp Nou.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, kinara huyo kwa sasa anashiriki mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Messi, Jorge, ambaye pia ni baba yake mzazi. Inaarifiwa kwamba majadiliano kati ya wawili hao yamefikia hatua muhimu na dalili zote zinaashiria kuwa Messi atatia wino kwenye kandarasi mpya atakayopokezwa.

“Mambo yanakwenda vizuri. Uhusiano wetu ni mzuri na Messi pia anaipenda Barcelona. Tungetamani astaafu soka akivalia jezi zetu japo ameeleza wakala wake kwamba ana mipango mingine kabla ya kabla ya kuangika daluga zake,” akasema Laporta.

Laporta aliyemrithi Josep Maria Bartomeu, ndiye alifanikisha mpango wa Barcelona kuajiri kocha Pep Guardiola ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Manchester City nchini Uingereza. Guardiola aliwahi kuwa mkufunzi wa Barcelona kati ya 2008 na 2012 chini ya Laporta aliyekuwa rais wa miamba hao kwa mara ya kwanza kati ya 2003 na 2010.

Ili kumdumisha Messi ugani Camp Nou, Barcelona watatarajiwa kupunguza gharama yao ya matumizi ya fedha kwa takriban Sh26 bilioni bila ya kuhitilafiana na kanuni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kuhusu uhamisho wa wachezaji.

Ilivyo, Barcelona wanatarajiwa kumpa Messi, 34, mkataba mpya wa miaka miwili kabla ya sogora huyo kuyoyomea Amerika kunogesha soka ya Major League Soccer (MLS) mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Barcelona wamefichua mpango wa kumpa Messi majukumu kwenye benchi yao ya kiufundi baada ya kustaafu soka akichezea mojawapo ya klabu za MLS.

Barcelona walianza kushiriki mazungumzo ya kurefusha mkataba wa Messi mnamo Aprili na wasimamizi wao wamekutana na wakala wa mwanasoka huyo raia wa Argentina zaidi ya mara 10 tangu wakati huo.

Mbali na Barcelona walio na kiu ya kumdumisha kambini mwao, maarifa ya Messi yanawaniwa pia na Paris Saint-Germain (PSG) pamoja na Man-City.

Matarajio ya Messi ni kucheza tena pamoja na aliyekuwa mwenzake kambini mwa Barcelona, Cesc Fabregas wa AS Monaco kutoka Ufaransa. Hiyo ni ndoto ambayo huenda ikafaulu tu iwapo Messi atayoyomea MLS baada ya miaka miwili ijayo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

KAMAU: Ni kosa kuwabagua wananchi kwa misingi ya tabaka

Ubelgiji kuonana na Italia kwenye robo-fainali za Euro...