• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
ODONGO: Badala ya kupigia debe BBI, Raila afaa kuangazia 2022

ODONGO: Badala ya kupigia debe BBI, Raila afaa kuangazia 2022

Na CECIL ODONGO

BAADA ya korti kutoa uamuzi kwamba mpango wa BBI una dosari na kinyume cha katiba, Kinara wa ODM Raila Odinga anafaa afunguke macho na kujisakia uungwaji mkono iwapo kweli bado analenga kuwania kiti cha Urais 2020.

Japo, tayari sekretariati imeelekea katika mahakama ya rufaa kupinga uamuzi wa jopo la majaji watano, Bw Odinga anafaa kutomakinikia rufaa hiyo na badala yake asake mbinu ya kuwarai Wakenya wamuunge mkono 2022.

Kwanza uchaguzi wa 2022 umesalia miezi 14 pekee na wakati huo ni mfupi mno kiasi cha kuangazia kesi iliyoko mahakamani na siasa za marekebisho ya katiba kupitia BBI. Iwapo kesi hiyo itajikokota kortini huenda hata makadirio ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kufikia Julai au Agosti isitimie jinsi baadhi ya wanasiasa wanavyodai.

Si siri kwamba baadhi ya yaliyomo katika mswada wa BBI ndio yangeumiza sana umaarufu wa Bw Odinga na angeerevuka zaidi na kuasi mpango huo, kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta hana cha kupoteza kwa sababu atakuwa anastaafu mwaka ujao.

Suala tata ambalo japo baadhi ya wanaounga Bw Odinga katika chama chake cha ODM walikosoa kuzungumzia sana kwa hofu ya kumkasirisha ni kugawanywa kwa maeneobunge 70. Karibu maneobunge 35 yalikuwa yatwaliwe na eneo la Kati huku ngome za Bw Odinga za Pwani, Nyanza na Magharibi zikipata viti vichache kuliko hata nusu ya idadi ya vile vilivyoelekezwa kwa eneo la Mlima Kenya.

Ingawa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, seneta wa Siaya James Orengo na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo walijaribu kuibua suala hili, walirejelewa kama viongozi wasaliti ambao walikuwa wakimpinga Bw Odinga.

Hata hivyo, uamuzi wa jopo la majaji watano uliwasadikisha na kuwaondolea lawama baada ya kusisitiza kuwa ni jukumu la Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kubuni maeneobunge mapya nchini.

Pia mchakato wa BBI umeharakishwa na baadhi ya wandani wa Bw Odinga wamefumbwa macho na kuona kuwa utamwezesha kinara wao kuingia ikuluni mnamo 2022. Ingawa hivyo, imani hii haina mashiko kwa sababu Rais Kenyatta hajamtaja kiongozi atakayemuunga mkono hadharani mwaka ujao huku viongozi wa One Kenya Alliance pia wakimwania ili wapokee baraka zake 2022.

Kati ya masuala ambayo Bw Odinga anafaa kumakinikia sasa kuliko BBI ni kuvumisha chama chake cha ODM maeneo yote Kenya na kuziba mianya ya migawanyiko katika ngome yake ya kisiasa.

Pia, chama hicho hakifai kuaihirisha uchaguzi wake wa mashinani ila uendelee jinsi ulivyopangwa ili kuwasaka viongozi maarufu ambao watashabikiwa na raia ndipo ODM inyakue viti vingi nchini.

Vilevile Bw Odinga anafaa kuanza mchakato wa kuingia kwenye miungano na viongozi ambao wataboresha nafasi yake ya kuingia ikulu mnamo 2022 na kupenyeza katika ngome za kisiasa za wapinzani wake.

Kupigania BBI kana kwamba mswada huo ni wake na utamkabidhi Urais bila juhudi zozote jinsi ambavyo baadhi ya wafuasi wake wanavyoamini kujidanganya. Amewahi kusalitiwa kisiasa na hilo bado litawezekana tu hata BBI hatimaye ikipitishwa kupitia kura ya maamuzi.

You can share this post!

Idadi ya wateja ingali ya chini katika hoteli kadhaa...

Beki Thiago Silva arefusha mkataba wake kambini mwa Chelsea...